Kona ya Karugendo
NIMESOMA kwenye gazeti (Raia Mwema), Ridhiwani – mtoto wa Rais Kikwete, akilalamika kwamba anasakamwa na kusingiziwa mambo mengi.
“Wakati mzee wangu anaingia kwenye siasa (kuwania urais) nilikutana na Abdallah Mwinyi (mtoto wa Rais Mstaafu, Mzee Mwinyi), akaniambia changamoto nitakazokutana nazo kama mtoto wa rais, na sasa nazishuhudia vilivyo”. Hayo ni maneno ya Ridhiwani yaliyonukuliwa kwenye gazeti nililolisoma. Siandiki makala hii kumsakama Ridhiwani au kumsingizia kwa lolote lile. Nataka kuweka mambo sawa na kuteta na watoto wa marais wetu.
Simkatalii Ridhiwani kwamba ukiwa mtoto wa rais utakumbana na changamoto nyingi. Ni ukweli; maana rais ni kiongozi wa nchi. Kila jicho linaangaza kwa rais, na hivyo ni lazima wote wanaomzunguka waangazwe.
Kwa maana hiyo, ni lazima na ni muhimu kukaa “sawa sawa”. Hata hivyo, sikubali kwamba ukiwa mtoto wa rais na hasa katika taifa letu la Tanzania, ni lazima usakamwe na kusingiziwa! Natetea hoja yangu kama ifuatavyo.
Taifa letu hadi leo hii limeongozwa na marais wanne. Na kwa bahati nzuri marais wetu wana watoto. Na tukianza na Mzee Mwinyi, anayetajwa na Ridhiwani, sijapata kusikia mtoto yeyote wa Mzee Mwinyi akisakamwa na kusingiziwa kwa vile baba yake alikuwa Rais.
Kama kuna mtu alisikia watoto wa Mzee Mwinyi wakisakamwa na kusingiziwa, ajitokeze na kutoa ushuhuda. Nina uhakika watoto hawa wana kazi zao, wana biashara na shughuli nyingine, lakini sijapata kusikia shughuli zao sikuhusishwa na cheo cha baba yao.
Mke wa Mzee Mwinyi, Mama Sitti, alisakamwa na kusingiziwa kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na madai kwamba alitumia jina la mume wake kufanya biashara. Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa kina na kulinganisha na yale yaliyotokea baada ya Mzee Mwinyi, kuondoka madarakani, watu waligundua kwamba Mama Sitti alionewa tu.
Ukweli ni kwamba Mzee Mwinyi, akiwa madarakani, hakuna mtoto wake aliyesakamwa na kusingiziwa kufanya biashara au kuwa na mali nyingi kupindukia. Hata hivyo, nimepata kusikia mitaani mtoto wake mwingine ambaye hivi sasa ni waziri, Hussein Mwinyi, akilalamikiwa ‘kutanua’ barabarani na gari akiwa anakwenda kazini kutokea nyumbani kwake. Watu wakahoji: Waziri akitanua na kushindwa kufuata sheria za barabarani wengine watafanya nini?
Na ukweli ni kwamba ‘akitanua’ na wengine watamfuata nyuma yake. Hata hivyo, tabia hii ya ‘kutanua’ barabarani si kwa vile huyu ni mtoto wa rais mstaafu, bali ni tabia yake yeye kama yeye.
Watoto wa Mwalimu Nyerere, wote bado wako hai. Sikupata kusikia wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere mtoto wake yeyote akisakamwa na kusingiziwa kwa vile tu baba yake ni rais wa nchi.
Aidha, sijapata kusikia madai kwamba watoto hawa wana mali nyingi kupindukia. Kama kuna mtu alipata kusikia, naomba ajitokeze na kutoa ushuhuda.
Hata baada ya Mwalimu kustaafu hadi kifo chake Oktoba 14, 1999, sijapata kusikia mtoto yeyote wa Mwalimu akitajwa kwenye mambo machafu.
Watoto wa Mwalimu Nyerere walisoma shule za kawaida na baadaye kuishi maisha ya kawaida kabisa kwenye jamii. Hata leo hii wanaendelea kuishi maisha ya kawaida kabisa.
Ni imani yangu kwamba hata wao wanaendesha maisha yao kwa kufanya biashara na shughuli nyingine, lakini sijapata kusikia wakisakamwa na kunyoshewa kidole kwa mambo yoyote machafu.
Ni wazi changamoto za kuwa watoto wa rais watakuwa walizipata wakati baba yao alipokuwa madarakani, lakini zile za kusakamwa na kusingiziwa kumiliki mali nyingi kupindukia, au kujihusisha na mambo machafu ya ufisadi, ujangili na mengine ya aina hiyo, sijapata kusikia.
Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa naye ana watoto. Sijapata kusikia wakati wa utawala wake mtoto wake yeyote akisakamwa na kusingiziwa mambo machafu. Kama sikosei kuna Watanzania wengi ambao hawafahamu hata majina ya watoto wa Mzee Mkapa.
Majina yao hayakupamba vichwa vya habari vya magazeti, na wala hawakujiingiza kwenye siasa na pia hawakulitumia jina la baba yao kwa lolote lile. Kama kuna mtu anafikiri ninasema uongo, basi ajitokeze na kutoa ushuhuda wake.
Kama sikosei, mtoto wa marais wetu ambaye amesikika sana kwenye vyombo vya habari, na ambaye amesakamwa na kusingiziwa mambo mengi ni Ridhiwani Kikwete. Sipendi kuamini kwamba anasakamwa kwa vile yeye ni mtoto wa rais.
Siamini hivyo maana, kwa mifano yote niliyoitoa, na hasa ya hapa kwetu Tanzania, inaonyesha wazi kwamba kuwa mtoto wa rais si kigezo cha kusakamwa na kusingiziwa mambo mengi na jamii.
Lakini pia sipendi niamini yote yanayosemwa juu ya Ridhiwani kuwa ni ya kweli. Ningekuwa ni yeye, ningetafuta chanzo cha yote haya badala ya kulalamika tu na kutumia vyombo vya habari kujitetea kwamba anasakamwa kwa vile yeye ni mtoto wa rais.
Kutafuta chanzo na kuhakikisha anaweka mambo sawa ni muhimu sana kwake; maana “urais” una kikomo, lakini yeye kama yeye bado ana safari ndefu katika taifa letu.
Kwa vyovyote vile; mambo mengi yanayosemwa juu ya Ridhiwani ni ya kumsingizia. Swali la kujiuliza ni kwa nini anasingiziwa mambo hayo? Ni wapi kateleza?
Binafsi nimebahatika kutembea mikoa karibu yote ya nchi yetu. Kila wilaya ukienda, kama kuna jumba kubwa jipya, utaambiwa ni la Ridhiwani Kikwete. Kama kuna kituo cha mafuta kipya, utaambiwa ni cha Ridhiwani Kikwete. Ukikutana na magari makubwa ya mizigo, utaambiwa ni ya Ridhiwani Kikwete!
Hata hapa Dar es salaam kila hoteli kubwa na ya kisasa inayojengwa, utaambiwa ni ya Ridhiwani Kikwete. Mwisho mtu unabaki kujiuliza: Ridhiwani, mtoto mdogo hivyo kapata wapi utajiri wote huo? Wengine wanadai kuwa huyu ndiye mtoto wa rais tajiri kuliko watoto wa marais wengine wote wa Afrika!
Ndani ya chama tawala (CCM), na hasa Umoja wa Vijana wa chama hicho ukisikia kuna mtafaruku, jina la Ridhiwani Kikwete litatajwa na kudaiwa kuongoza na kuchochea mtafaruku huo.
Maana yake ni kwamba, jina la Ridhiwani Kikwete linasikika kwenye siasa, biashara, michezo na mambo mengine mengi tu. Hata kwa mambo ya ovyo tu utasikia mtu akisema: “Ngoja nitazungumza na Ridhiwani na mambo yatakwenda sawa”!
Siku moja pale mtaa wa Samora, jijini Dar es Salaam, kuma msichana aliyegonga gari la mtu. Alipoelezwa ukweli wa kosa lake alikuja juu na kusema: “Ngoja nimpigie Ridhiwani simu”.
Mifano kama hii iko mingi mitaani, maofisini, vijiweni, na hata sehemu nyingine ambazo mtu ungefikiri umbea na ujinga usingepenya.
Kwa mfano, kuna habari za mitaani kwamba Rais Kikwete aliteua wakuu wa wilaya ambao wengi wao ni marafiki wa Ridhiwani na wengine wanakwenda mbali kusema kwamba ukitaka mambo ya kunyokee, uongee na Ridhiwani; maana huyu ndiye mshauri wa karibu wa Rais Kikwete.
Kama kuna ukweli wa aina yoyote kwamba huyu kijana ni mshauri wa karibu wa baba yake, Rais Kikwete, yawezekana jina lake likatumika vibaya. Yawezekana pia hata wale wote wanaosingizia biashara zao ni za Ridhiwani watakuwa wanafanya hivyo kujilinda tu.
Lakini pia yawezekana haya makampuni ya yanayouza mafuta na kusakamwa kukwepa kulipa ushuru yanalazimika kutaja jina la Ridhiwani ili kujiokoa tu, na si kwamba ana mahusiano yoyote nayo?
Waswahili wanasema; lisemwalo lipo, na kama halipo basi litakuwa njiani linakuja. Ni muhimu kwa ndugu yetu Ridhiwani Kikwete kutafakari kwa kina na kuchunguza yote yanayosemwa juu yake.
Akiendelea kujiliwaza kwamba anasakamwa na kusingiziwa kwa vile tu yeye ni mtoto wa rais, atashindwa kuwashawishi Watanzania; maana historia yetu haionyeshi watoto wa marais wetu waliopita kusakamwa au kusingiziwa kama inavyotokea hivi sasa kwake.

No comments:
Post a Comment