UKOSEFU wa usingizi ni tatizo
linalowasumbua wengi maishani, na inakisiwa kuwa zaidi ya humusi ya watu wazima
wamewahi kutatizwa na usingizi wakati mmoja maishani mwao. Ukosefu wa usingizi
hutatiza sana , hasa ikiwa utatokea usiku, na mwathiriwa kuhisi usingizi na
uchovu mchana, wakati ambapo anafaa kuwa akifanya kazi.
Kuna baadhi ambao, licha ya kulala
masaa mengi, miili yao huhisi kwamba haijapata usingizi wa kutosha. Hii mara
nyingi hutokana na kutoweza kupata usingizi haraka, kuamka mapema sana au kuwa na
usingizi unaotatizika, au usio na raha. Hii mara nyingi hutokana na mfadhaiko,
hamu au wasiwasi kuhusu jambo fulani, hisia pamoja na mazingira kwa mfano
kelele, hali ya kitanda au hata watu walio karibu wakati wa kulala.
Kufanya kazi kwa zamu, kwa mfano wakati
mwingine usiku na mwingine mchana huwa pia sababu ya matatizo ya usingizi kwa
kuwa mwili hushindwa kuzoea.
Kufanya kazi zaidi, kunywa pombe kupindukia au
hata kunywa vinywaji vyenye viwango vya juu vya kemikali aina ya kafeine ambayo
hupatikana kwenye kahawa kadhalika huweza kusababisha matatizo haya. Matatizo
ya mwili kwa mfano majeraha, tatizo la maumbile kama vile kusikia kelele ndani
ya sikio tatizo ambalo hujulikana kitaalamu kama tinnitus aidha huweza kutatiza
usingizi wa mwanadamu.
Ukiweza kutambua kwa ufasaha kiini cha
matatizo yako ya usingizi, unaweza kutafuta suluhisho. Kwa mfano, ikiwa kitanda
kiko katika hali mbaya, unaweza kutafuta kingine, au hata kununua godoro na
blanketi mpya. Kuwa na mtindo wa kulala kadhalika husaidia sana . Unafaa kuwa
na masaa fulani ya kulala na kuamka ili mwili uzoee. Ubongo utakuwa tayari kila
wakati huo ukifika kupumzisha mwili, na baadaye kuuamsha katika muda ufaao.
Unaweza kualika usingizi kwa
kutojishughulisha na mambo mengi wakati wa kulala unapokaribia, kuoga kwa maji
moto kiasi au kusikiliza nyimbo tamu. Si ajabu kwamba mama anapotaka mtoto
alale, humwimbia nyimbo tamu, na hii hufanikiwa na hata mtoto aliyekuwa akilia
akiwa amejawa na hasira hatimaye hulala. Jiepushe pia na unywaji wa pombe
kupindukia, au kunywa vinywaji vyenye viwango vya juu vya kafeine. Ikiwa tatizo
lako ni mfadhaiko, tafuta mtaalamu wa matatizo ya fikira au mshauri
atakayekusaidia kutua mzigo wa fikira.
No comments:
Post a Comment