Mafumu nguli wa ‘midomo ya bata’
Ni moja ya wanamuziki wenye kipaji cha pekee
katika upulizaji wa mdomo wa bata, maarufu Saxephone, pamoja na umahiri
katika chombo hicho, lakini pia ni mpigaji mzuri wa gitaa la solo na
rhythm, kama hiyo haitoshi ni mwimbaji mzuri licha ya kuchelewa kugundua
kipaji hicho.
Alianza rasmi kujiingiza kwenye muziki mwaka 1973,
lakini hadi leo ni moto wa kuotea mbali kutokana na kuwa maahiri wa
kufanya kazi hiyo ambayo kwa mujibu wake atakufa akiifanya.
Hapa namzungumzia mmiliki wa Bendi ya African
Beat, Mafumu Bilal Bombenga ‘almaarufu Super Sax’, alifanya mahojiano na
gazeti hili nyumbani kweke Vingunguti Kiembe Mbuzi, ili kujua au
kusikia kutoka kwake alianza lini muziki na kwa nini yupo hapo alipo
sasa.
Mafumu alianza kueleza safari yake ya muziki
ilivyoanza kwa kusema kuwa kama siyo moyo wa dhati wa kupenda muziki
wala asingefika hapo alipo kwa kuwa baba yake mzazi aliyekuwa mganga
maarufu mkoani Kigoma, Mzee Bilali hakutaka kabisa awe mwanamuziki kwa
kuhakikisha kila akijaribu kujiingiza kwenye masuala hayo anamtoa.
“Mzee Bilal hakutaka kabisa kusikia muziki
alipenda nisome sana dini, lakini nilikuwa kila nikipata nafasi hata kwa
kuchana uwa natoroka na kwenda kwenye muziki,” alianza kueleza historia
yake ya muziki.
Mafumu anasema kuwa alizaliwa mwaka 1958,
Mwanga-Kigoma, Barabara ya Legeza Mwendo, na kupata elimu ya msingi
katika shule ya H.H Aga Khan, kabla ya kuhamia Tabora ambapo alisoma
elimu ya sekondari katika Shule ya Kazima.
Anasema akiwa darasa la sita ndipo alipobaini kuwa
anapenda muziki kwani alikuwa akimwona mjomba wake mwanamuziki Shem
Kalenga, Mkurugenzi wa Tabora Jazz, akipiga gitaa la besi katika bendi
ya Lake Jazz.
“Nilidhamiria moyoni kuwa nitakuwa kama mjomba
licha ya kuwa na vikwazo kutoka kwa baba aliyekuwa hapendi kabisa mambo
hayo, nilikuwa nakwenda anakopiga kwa kupasua ua kwa kuwa ulikuwa wa
nyasi na kurudisha kama ulivyokuwa na nilikuwa nikifanya hivyo mara
nyingi,” anasema Mafumu.
Anaeleza kuwa siku moja aliamua kuchonga ubao
akaweka na kopo la mafuta ‘dumu’ na nyuzi za kuvulia samaki ‘mshipi’
akapata gitaa la solo la kienyeji, lililokuwa linamfanya anakuwa bize
kiasi cha kutosikia hata mtu akiongea pembeni yake hadi amguse.
“Sikufundishwa na mtu nilijifunza kupiga gitaa kwa
kuangalia hasa nilikuwa naweza kukaa hata saa namwangalia mjomba
akipiga na mwisho nikajua bila kuelekezwa kushika wala kuambiwa hiyo ni
nyuzi hii fanya hivi wala nini,” anasema Mafumu.
Anaendelea kueleza kuwa baadaye alikuwa akienda
kwenye bendi ya Kigoma Jazz kwa kutoroka, ili azidi kuongeza ujuzi kwa
kuangalia na wengine wanapiga kama mjomba wake au laa, na kukuta ujuzi
unazidiana na kutofautiana lakini taratibu ni zilezile.
Anasema alijifunza kupiga Saxephone, alipokuwa
Kazima Sekondari ambapo alichaguliwa kuwa mmoja wa wanaopiga Blassband,
“nilijiachia na kupiga vifaa vingi lakini nikanufaika zaidi kwani
niliweza kupuliza sax na hapo umahiri ndiyo ulipoanza,” anasema.
Anasema baada ya kumaliza shule alikwenda Makutupora Dodoma
jeshini kwa mujibu wa Sheria na mwaka 1973, yakatangazwa majina ya
waajiriwa la kwake halikuwepo lakini aliambiwa asubiri orodha nyingine,
hata hivyo akaamua kutoroka kwenda Morogoro kwenye bendi ya Morogoro
Jazz.
“Nilikwenda kujiunga na Moro Jazz bila kuwa na
ndugu katika mji huo, yaani nilikwenda moja kwa moja kwenye bendi na
nikapokewa wakati huo ndio hayati Mbaraka Mwinshehe anaondoka kwenda
kuunda bendi yake ya Super Volcano,” anasema Mafumu.
Anasema hakukaa sana na bendi hiyo kwani alikuta
ndiyo inaelekea mwisho baada ya kuondoka kwa Mwinshehe, akaja Dar kwa
kaka yake na kujiunga na bendi ya Western Jazz waliokuwa wakitumia
mtindo wa ’saboso’ ikiwa chini ya uongozi wa Shamba Ramadhani.
Anautaja mshahara wake wa kwanza kupokea akiwa na bendi ya Western ni Sh.275, ambazo alizitumia zote kununua nguo.
“Nilikuwa naishi kwa kaka yangu kila kitu bure na
nilikuwa napenda sana kuvaa, hivyo nikautumia mshara wote kununulia nguo
wakati huo sikuwa mnene kama leo nilinunua suruali za mtindo wa
bugaluu, viatu vya raizoni na mashati ya kubana ya kutosha kwa kuwa
ndiyo nilianza kuona umuhimu wa kuwa mwanamuziki na jinsi gani natakiwa
kung’aa,” anasema Mafumu huku akicheka.
Anaeleza kuwa wakati huo hakuwa akiimba bali alikuwa anapuliza mdomo wa bata na kupiga rhythm gitaa.
Anasema akiwa Western wapinzani wao wakuu walikuwa
ni bendi ya Dar Jazz ‘majini wa bahari’ ambapo pamoja na muziki bendi
hizi pia zilikuwa ni wapinzani wa jadi katika soka kwani Western Jazz
ilikuwa ni Yanga ingawa yeye hashabikii timu hiyo na Dar Jazz ni Simba,
hivyo bendi hizo zilijigawa katika mtindo huo na ilikuwa marufuku na
haikutokea Western kupiga kwenye tafrija za Simba na Dar Jazz vile vile
kwenye za Yanga.
“Mamluki kama mimi wasiokuwa wanachama au
mashabiki wa timu inayoshabikiwa na bendi husika walikuwepo lakini
mashabiki na wapenzi wa bendi hizi walijigawa katika mtindo huo Western
Yanga na Dar Jazz Simba, ilikuwa wenyewe huwaambii kitu hasa mtajiri wa
Western na ushabiki wa soka wa zamani ulikuwa wa kweli,”anafafanua
Mafumu.
Anazitaja nyimbo ambazo zilitamba wakati yupo na
bendi hiyo kuwa ni pamoja na jela ya mapenzi, Rosa, Vigelegele na
Hakika, huku akiutaja ukumbi mkuu wa bendi hiyo kuwa ni Community Centre
uliokuwepo ilipo sasa Makao Makuu ya Wilaya ya Kinondoni, maeneo ya
Magomeni Mapipa.
No comments:
Post a Comment