|
Afrika kusini ya jangwa la Sahara, ndilo
eneo lililoathiriwa zaidi na janga la Ukimwi. Eneo hili lina asilimia 10
tu, ya jumla ya idadi ya watu kote duniani, lakini ndilo lenye idadi
kubwa zaidi ya watu waishio na virusi vya HIV.
Yaani – theluthi mbili (2/3) za watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kote duniani.
Ukimwi husababisha vifo vya watu takriban watu 6,000 kila siku barani Afrika.
Pindi mtu anapoambukizwa virusi vya HIV, huishi
navyo kwa maisha yake yote kwani hakuna tiba, lakini siku hizi yapo
madawa speshei ya kupunguza makali ya ukimwi hivyo basi kusaidia walio
ambukizwa kuishi kwa muda mrefu.
HIV na Ukimwi barani Afrika
Ukweli ni kwamba: Zaidi ya watu milioni mbili nchini Kenya wameambukizwa virusi vya HIV vinavyosababisha Ukimwi.
Ukweli ni kwamba: Nchini Uganda Ukimwi ndio unaoongoza kwa kusababisha vifo kwa wale wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49.
Ukweli ni kwamba: Ukimwi umewaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume hasa vijana walio kwenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24.
Ukweli ni kwamba: Maambukizo
ya virusi vya ukimwi miongoni mwa watu wazima katika sehemu za mijini
ni karibu mara mbili zaidi kuliko sehemu za mashambani.
Ukweli ni kwamba: Karibu wakenya 150,000 hufa kwa ukimwi kila mwaka.
UNAIDS report 2004
|
HIV ni nini?
ni ufupisho wa Human Immunodefeciency Virus yaani virusi vinavyoua kinga ya mwili. Ni HIV ni kirusi kinachoharibu uwezo wa mwili wako wa kujihami dhidi ya maambukizo.
ni ufupisho wa Human Immunodefeciency Virus yaani virusi vinavyoua kinga ya mwili. Ni HIV ni kirusi kinachoharibu uwezo wa mwili wako wa kujihami dhidi ya maambukizo.
Watu wengi hufikiria kwamba watu ambao wana virusi
hivyo, wana Ukimwi, ukweli ni kwamba virusi vya HIV ndivyo
vinavyosababisha Ukimwi, yaani yawezekana mtu akawa na virusi vya ukimwi
kwa muda mrefu bila ya kuugua ukimwi. Hii inamaanisha anaweza kuwa na
HIV bila kujua, wala kuona dalili zozote – Wakati huo iwapo tahadhari
hazitachukuliwa anaweza kumwambukiza mtu mwengine .
Ukimwi ni nini?
Neno Ukimwi lina maana ya Ukosefu wa Kinga Mwilini. Hapa virusi vya HIV huwa vimeshambulia kinga ya aliyeambukizwa kiasi kuwa, mwili wake wauwezi tena kujipa ulinzi dhidi ya maambukizo.
Neno Ukimwi lina maana ya Ukosefu wa Kinga Mwilini. Hapa virusi vya HIV huwa vimeshambulia kinga ya aliyeambukizwa kiasi kuwa, mwili wake wauwezi tena kujipa ulinzi dhidi ya maambukizo.
Hivyo huonyesha dalili za magonjwa tofauti tofauti
na hata saratani, hapo ndipo wanasemekana kwamba wana ukimwi. Wakati huo
ndipo kinga yao ya mwili huwa ni dhaifu sana, na magonjwa alo nayo
yanakuwa vigumu kuyatibu na ndipo hapo ukimwi unasababisha kifo.
Fahamu kuwa kila mtu hukumbana na viini ambavyo
husababisha magonjwa, lakini kama kinga yako ni imara si rahisi kupata
maambukizo na hata ukipata ni rahisi kuyatibu lakini kwa wale waishio na
virusi vya ukimwi kinga yao huwa imedhoofishwa sana kiasi kuwa
akikumbana na viini ni rahisi kwake kupata maradhi na hata akitibiwa
inachukua mda kupona.
Lakini ni vyema kufahamu kuwa siku hizi kuna dawa
spesheli kwa watu wenye virusi vya HIV ambazo hupunguza makali ya
ukimwi. Dawa hizi husaidia kuzuia kuzaana kwa virusi vya HIV mwilini.
Hata hivyo hadi kufikia sasa kwa hakika hakuna chanjo dhidi ya virusi
vya ukimwi, na hakuna dawa ya kutibu Ukimwi.
Lakini kwa jinsi matibabu yalivyoimarika katika
miongo michache iliyopita, inamaanisha kwamba maisha ya baadhi ya watu
walio na virusi vya Ukimwi yanaweza kurefushwa kwa miaka kadhaa.
Jinsi maambukizo ya HIV yanavyotokea.
Virusi vya HIV husambazwa kwa njia zifuatazo:
- Kufanya ngono bila kinga.
- Kuchangia sindano.
- Mama aliyeambukizwa anaweza kumwambukiza mwanawe wakati wa uja uzito, kuzaa au kunyonyesha.
- Kutangamana kwa damu au majimaji mengine ya mwili – mfano damu iliyo na virusi ikipenya kwenye jeraha au mchubuko.
- Kuongezewa damu iliyo na virusi.
Huwezi kuambukizwa virusi kupitia:
- Kupigana busu, kugusana, au kuamkiana kwa mikono.
- Kutumia kwa pamoja vifaa vya kulia chakula.
- Kukohoa au kwenda chafya.
- Kuumwa na wadudu kama kunguni au mbu au wanyama.
- kupitia Vidimbwi vya kuogelea.
- Kula chakula kilichotayarishwa na mtu aliye na virusi vya ukimwi.
Dalili za virusi vya Ukimwi?
Watu wengi walioambukizwa virusi vya HIV, huwa
hawafahamu kama wameambukizwa, kwa sababu hakuna dalili zinazotokea mara
moja baada ya kuambukizwa.
Watu wengine hupata homa, vipele, maumivu ya viungo
na uvimbe mgumu, lakini dalili hizi zinaweza kutokea kati ya wiki sita
na miezi mitatu, baada ya kuambukizwa.
Hii ni kusema mara nyingi mtu aliyeambukizwa virusi
vya ukimwi huenda asionyeshe dalili zozote, lakini tahadhari
isipochukuliwa wanaweza kuwaambukiza watu virusi hivyo.
Matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi
Bado hakuna tiba ya ukimwi, lakini kuna dawa
spesheli ambazo zinaweza kusaidia waishio na virusi kwa kuimarisha afya
hivyo basi kuongeza umri.
Nifanyeje kama nahisi nimeambukizwa virusi vya HIV?
Njia ya pekee ya kugundua kama una virusi vya hiv ni kwa kufanyiwa uchunguzi wa HIV.
Kufanyiwa uchunguzi wa virusi vya HIV si vigumu.
Unachotakiwa kufanya ni kutembelea kituo cha afya
ya uzazi au (VCT). Hapa utapata ushauri – Kisha kama uko tayari
kuendelea na uchunguzi huo, Utatoa damu ambayo inapelekwa kufanyiwa
uchunguzi, kuona kama ina virusi. Matokeo hayachukui muda mrefu
kutolewa, na waweza kuyasubiri.
|
Pengine itahijitaji uchunguzi kama mara mbili tatu
hivi kubainisha kwa yakini iwapo mtu ameambukizwa au la. Hii ni kwa
sababu inachukua kipindi cha kama miezi mitatu kuanzia siku ya
kuambukizwa kwa virusi kuweza kuonekana wakati wa uchunguzi.
Pengine swala la kusubiri kwa mda huu ndiyo sehemu
ngumu zaidi ya utaratibu wa kuchunguza virusi vya ukimwi, lakini
kusubiri kuna maanisha kwamba utakuwa na uhakika wa matokeo.
Huduma za uchunguzi wa virusi vya ukimwi
zinapatikana kwa urahisi. Wasiliana na daktari wako au tembelea tu kituo
cha huduma za afya ya uzazi kwa vijana kama vile VCT. Kama una wasi
wasi kuhusu kuhifadhiwa kwa siri zako, usiwe na hofu.
Katika kliniki nyingi kuna utaratibu kabambe wa
kuhifandhi siri za wateja. Haya yote utafahamishwa na mshauri wako,
ikiwemo ni vipi uchunzguzi huo unafanywa, vipi utapokea majibu na hata
kupata ushauri zaidi wa jinsi ya kuishi na virusi iwapo kwa bahati mbaya
itabainika kuwa tayari umeambukiza.
Kumbuka Kama umefanya mapenzi bila kinga, ama
unafikiria kuna uwezekano wowote kwamba umeambukizwa virusi vya HIV ni
vyema kufanyiwa uchunguzi huo.
Usiendelee kuhatarisha maisha yako na ya wengine –
Uamzi wa kwenda kufanyiwa uchunguzi wa virusi vya HIV unaweza kuwa
mgumu, lakini ni busara kwako na kwa wengine kutafuta usaidizi na
ushauri wa kitaalam mapema iwezekanavyo.
Jinsi ya kuepuka maambukizi ya HIV.
- Usijihusishe na ngono isiyo salama. Tumia kinga kila mara unapofanya ngono. Ukweli ni kwamba hakuna tendo la ngono lililosalama kwa asilimia 100. Kutumia kinga ni kupunguza hatari ya kuambukizwa virusi vya HIV ukimwi, na magonjwa mengine ya zinaa. Kwa hivyo daima tumia kondom na uyafuate maagizo kikamilifu.
- Usichangie sindano.
Jinsi mtu anavyoambukizwa virusi vya HIV.
Mtu huambukiwa virusi vya HIV kama kirusi cha HIV
kitaingia kwenye mishipa yake ya damu, wakati majimaji yake ya mwili
yatatangamana na yae ya mtu ambae tayari ameambukizwa.
Virusi vya HIV hupatikana kwa wingi kweye majimaji haya ya mwili wa mtu ambae tayari ameambukizwa.
- Damu
- Manii/ Shahawa
- Majimaji ya ukeni, ikiwa ni pamoja na hedhi
- Maziwa ya matiti
Kwa kawaida majimaji mwengineyo ya mtu
aliyeambukizwa kama mate, jasho na mkojo huwa hayana idadi kubwa ya
virusi, kutosha kumwambukiza mwingine.
Ndio sababu maambukizo ya virusi vya HIV hutokea
zaidi kupitia ngono na aliyeambuzwa, kuongezwa damu iliyo na virusi,
mama aliyeathirika kumnyonyesha mtoto, au kuchangia sindano na
mwathirika nk. Na hali yenginezo kama hizo.
Wakati wa kufanya ngono virusi hivyo huweza kupenya
na kumwingia mtu mwengine kupitia maeneo nyororo ya ukeni, uumeni,
sehemu ya kupitisha haja ndogo na hata njia ya kupitisha haja kubwa kwa
wale wanaotumia njia hiyo kufanya ngono.
Kufanya mapenzi katika hali ya kuwa sehemu za siri
ni kavu huongeza hatari ya kuambukizwa virusi vya HIV pamoja na magonjwa
mengine ya zinaa.
Ngono kavu
Hii ni katika ile hali ya kufanya ngono ilhali eneo
la ukeni halina ule unyevu nyevu wake wa kawaida. Hali hii huongeza
hatari ya kuambukizwa virusi vya HIV na pia magonjwa mengine ya zinaa.
Baadhi ya watu, wana itikadi kwamba wanawake wenye unyevu unvyevu mwingi
ukeni, wanapenda mno kufanya ngono hivyo basi ni mzinzi.
Ukweli ni kwamba wanawake kimaumbile hutoa majimaji
hayo wakati miili yao inajitayarisha kufanya mapenzi. “Kuwa tayari kwa
mapenzi” hakumaanishi kwamba uko tayari kufanya ngono na mtu yeyote tu!
Na kama wanamke hayuko “tayari kufanya mapenzi”, na akaendelea na
kufanya ngono kavu, (iwe kwa kulazimishwa au kwa hiari) husababisha
maumivu makali kwa mwanamke, na kumsababishia pia kupujuka hali
inayozidisha hatari ya kupata maambukizo.
Kuwa na Virusi vya HIV ilhali u-mja mzito
Hatari kwa mtoto wako
Imekadiriwa kwamba asilimia kati ya 25 na 45 ya
wanawake wenye virusi vya ukimwi, na wamepata pia mimba, wanaweza
kuwaambukiza watoto wao ambao hawajazaliwa. Kwa hivyo wanahitaji ushauri
wa kitaalam na dawa spesheli ili kupunguza hatari kuwaambukiza watoto
wao.
Virusi vya ukimwi vinaweza kusambazwa kutoka kwa mama mja mzito aliyeambukizwa, hadi kwa mtoto tumboni kwa njia tatu:
- Wakati mtoto yungali tumboni mwa mama, ambapo virusi vinaweza kusambaa kutoka kwa mama hadi kwenye nyumba ya uzazi.
- Wakati wa kujifungua, ambapo mtoto anaweza kuingiwa na majimaji ya ukeni au majimaji mengine kutoka kwa mama.
- Wakati wa kunyonyesha, ambapo virusi vinaweza kuambukizwa kupitia maziwa anayonyonya.
Uwezekano wa kumwambukiza mtoto, wakati wa
kujifungua ni mkubwa zaidi kama mama ana ujazo mkubwa wa virusi mwilini
mwake na kinga yake tayari ni dhaifu. Kabla ya wanamke aliyeambukizwa
kupewa usaidizi wowote wa kimatibabu kwanza atafanyiwa uchunguzi wa damu
kuona kima cha virusi ndani ya mwili na hali yake ya kinga kwa ujumla.
Kama kinga yake itakuwa thabiti na idadi ya virusi
ni ndogo mwilini, huenda hatahitaji dawa mpaka kipindi cha mwisho mwisho
cha uja uzito yaani baada ya wiki ya 24.
Lakini kama ujazo wa virusi ni mkubwa na kinga
mwili ni dhaifu, huenda italazimu kutumia madawa spesheli ya kupunguza
makali ya ukimwi, mapema ili kupunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto.
Hatari ya kumwambukiza mtoto virusi vya ukimwi
inaweza kupunguzwa hadi kufikia kati ya asilimia, moja na asilimia mbili
tu kama hatua zifuatazo zitazingatiwa.
Kupata matibabu ya kupambana na virusi vya Ukimwi
- Kwa sasa hivi hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba kutumia madawa ya kupambana na makali ya virusi vya HIV (ARV), kunamletea madhara mama na mtoto ambaye hajazaliwa.
- Madawa ya kupambana na virusi vya ukimwi haswa AZT, yamethibitishwa kupunguza kwa asilimia kubwa, hatari ya mama kumwambukiza virusi hivyo mtoto wake wakati wa uja uzito .
- Kama tayari unatumia madawa hayo ya ARV, kisha ukagundua kuwa u-mja mzito, mfahamishe daktari wako haraka iwezekanavyo. Kwa kawaida huwa ni vyema kuendelea na matibabu, lakini huenda ikakulazimu kubadilisha madawa. Kwa vyovyote vile, usisite kutumia madawa hayo bila ya ushauri na daktari.
- Siku hizi inawezekana kupewa madawa ya ARV, ili kukabiliana na virusi vya ukimwi, kupitia kwenye mishipa ya damu wakati wa uchungu wa kujifungua. Inaaminika kwamba kufanya hivyo kunapunguza hatari ya kumwambukiza mtoto virusi hivyo wakati wa harakati za uchungu wa kujifungua.
- Pia, ni kawaida mtoto wako kupewa madawa ya kupambana na virusi vya ukimwi ili kuzuia uwezekano wowote wa kuambukizwa.
Kuzaa kwa njia ya upasuaji
- Ukichagua njia ya kuzaa kupitia upasuaji, yaani caesarean section kwa kimombo, kwaweza kupunguza kwa asilimia kubwa, hatari ya mama kumwambukiza mtoto wake virusi vya ukimwi.
- Utaratibu huu humkinga mtoto asiingiwe na damu ama majimaji mengine ya mwilini na pia inamaanisha kwamba hutapata maumivu yanayoandamana na uchungu wa mda mrefu wa uzazi, hali inayoaminika kuchangia uwezekano wa mama kumwambukiza mtoto.
Kutonyonyesha
- Inapendekezwa kwamba wanawake wenye virusi vya ukimwi wasiwanyonyeshe watoto wao bali watumie maziwa mbadala, kama ya ngo’mbe au maziwa maalum ya unga kwa watoto.
- Hilo pekee linasadikiwa kupunguza hatari ya mtoto kuambukizwa virusi kwa kati ya asilimia 10 hadi 20.
No comments:
Post a Comment