Dar es Salaam.Shule ya Sheria
katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), imeandika historia mpya baada ya
kutoa wahitimu 200 katika ngazi ya Shahada ya Uzamili kiwango ambacho
ni ongezeko maradufu la idadi ya wahitimu 10 hadi 15 wanaopatikana kila
mwaka kwa miaka ya nyuma.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Mkuu wa Shule hiyo
Profesa Bonaventure Rutinwa alisema idadi hiyo ni sehemu ya utekelezaji
wa mipango ya UDSM ambayo imelenga kuwaandaa wahitimu wa ngazi ya
shahada ya uzamili na uzamivu na ngazi zingine kuviacha vyuo vingine.
“Nchini kuna vyuo vipatavyo 30 na vyote
vimewalenga wahitimu wa ngazi nyingine na siyo hizo mbili, hivyo chuo
kimeona ni vyema kikashughulika na wale ambao ni wa ngazi za juu zaidi
ili kufanya usiwepo upungufu” alisema.
“Ni haki yetu kujivunia mafanikio haya kwa sababu
tunakwenda kutimiza lengo la kutoa elimu kwa wanafunzi wengi katika
masomo ya sheria,” alisema.
Profesa Rutinwa alisema kwa shule ya sheria kutoa
wahihitimu wa ngazi ya juu wa kiwango hicho ni jambo la kihistoria na
wanajivunia hatua hiyo na wamejipanga kuhakikisha idadi hiyo inaongezeka
kila mwaka. Hivyo ni wajibu wa wanajamii kusoma kwa bidii ili kuweza
kutimiza malengo yao kwani inawezekana.
No comments:
Post a Comment