Waendesha bodaboda 13 wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuendesha mauaji dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wezi wa pikipiki katika mtaa wa Kivule Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Mbali ya waendesha bodaboda hao, pia pikipiki 17 zilikamatwa na polisi kwa tuhuma kama hizo jana.
Hata hivyo, kazi hiyo haikuwa rahisi kwani polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi pamoja na risasi za moto kukabiliana na waendesha pikipiki zaidi ya 100, hali iliyozua mtafaruku mkubwa kwa wakazi wa mtaa huo na viunga vya jirani.
Kabla ya tukio hilo, madereva wa bodaboda walijikusanya kwa ajili ya kuendesha msako wa nyumba kwa nyumba baada ya kupata majina ya mtandao wa wezi wa pikipiki katika mtaa huo na maeneo ya jirani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Minangi, alisema kuwa hatua kali zimechukuliwa na jeshi hilo baada ya waendesha bodaboda hao kujichukulia sheria mkononi ya kuwaua watu waliokuwa wakiwakamata.
Kamanda Minangi alisema msako huo utaendelea kwa kuwa waliojitokeza katika mauaji hayo ya kinyama walikuwa ni wengi.
“Nawasihi waendesha pikipiki kama wanahitaji biashara wafanye biashara, vinginevyo waache mara moja vitendo vya kihalifu kwa kuwa tunaendelea kuwasaka hadi kieleweke,” alisisitiza Kamanda Minangi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule, Joseph Gassaya, alisema kuwa mtaa wake ulivamiwa na vitendo vya uhalifu yakiwamo mauaji ya vijana wawili.Gassaya alifafanua kuwa vijana hao waliuawa na madereva wa bodaboda kutokana na kuwahisi kuwa ni wezi.
"Nikiwa kiongozi wa mtaa huo, nafahamu kuwa matukio ya mauaji yamekuwa yakitokea mara kwa mara ikiwamo waendesha bodaboda wanne kuuawa na kuporwa pikipiki zao na taarifa zinatolewa polisi," alisema.
“Pengine vijana hao wameamua kuchukua sheria mkononi baada ya kuona taarifa zao hazifanyiwi kazi ipasavyo, bila kujua kuwa jeshi hilo linachukua hatua baada ya kuthibitisha,” alisema.
Naye mmoja wa waendesha bodaboda hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa wameshangazwa na kitendo cha polisi kutumia nguvu kupita kiasi.
Alisema taarifa za kuporwa pikipiki na kunyongwa kwa wenzao wanne, alitoa taarifa katika kituo cha Polisi Stakishari, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kuwasaka wahalifu hao.
“Sielewi kama waendesha pikipiki waliokufa hawakuwa watu. Kwa nini hao wezi waonekane kuwa wana haki zaidi...Jeshi lipo kwa ajili ya raia wote si kwa baadhi ya watu,” alisema.
Alisema kabla ya kutekeleza zoezi hilo, waliweka mtego kwa mtu waliyemhisi kuwa ni mwizi na aliponaswa mmoja wao, aliwataja wenzake wote aliokuwa akishirikiana nao kuiba pikipiki.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi halipendi kutoa ushirikiano kwa kuwa matukio ya mauaji yameripotiwa lakini hakuna hatua zilizochukuliwa, jambo lililowaudhi na kuamua kujichukulia sheria mkononi ili kujihami.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment