Tiba za nyoka, konokono zashamiri Ulaya
Wakati nyoka akiendelea kuwa adui mkubwa wa
binadamu na konokono kuonekana mdudu anayetia kinyaa kwa baadhi ya watu,
nchi za China na Japan wanyama hawa wamekuwa wakitumika kama mboga na
wakati mwingine wamekuwa ni rafiki wa binadamu kwani wengi wao hufugwa
na binadamu.
Lakini Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni,
kwani katika nchi za Ulaya miezi kadhaa iliyopita watu mbalimbali
wameanza kupokea tiba kutoka kwa wanyama hao ikiwemo huduma ya kukanda
na kupodoa uso (facial) inayotolewa na konokono na kusinga (massage)
inayotolewa na nyoka.
Facial ya konokono
Kwa wengi wetu konokono ni mdudu mpole zaidi
kuliko wadudu wengine wanaopatikana majanini, lakini nchini Japan
wataalamu wamegundua kuwa lami (uteute) anaotoa mdudu huyo ni tiba nzuri
kwa ngozi ya binadamu, baada ya kutumika kwa miezi kadhaa nchini Japan
sasa tiba hiyo imeanza kupendwa barani Ulaya, kama watu wanavyomiminika
katika saluni moja iliyopo East Midland nchini Uingereza.
Matibabu hayo yanahusisha konokono kuanzia watatu
ambao huwekwa juu ya uso wa binadamu na wao huanza kuzunguka maeneo
mbalimbali ya uso huo, yamekuwa yakiongeza uwingi wa watu katika saluni
za maeneo mbalimbali ya nchi za Ulaya.
Wataalamu hao wa facial ya konokono akiwamo Dk
Sunil Chopra wanasema kwamba katika matibabu hayo huwa wanahakikisha
kwamba konokono anatembelea kila sehemu ya uso wa binadamu isipokuwa
maeneo ya mdomo, macho na pua.
Kwa mujibu wa mmiliki wa Simply Divene Saloon
iliyopo Corby katika mji wa Northamptonshire nchini Uingereza, Diane
Gower matokeo ya tiba hiyo inayogharimu kiasi cha dola 50 sawa na
Sh80,000, huonekana papohapo na kwamba wadudu hao hutoa kamasi zenye
protini muhimu kwa ngozi ya binadamu.
Anasema, “Mwanzoni kwa mteja wa kwanza huwa
wanashtuka sana kwani anapokutembea usoni huona kuwepo kwa hali
isiyokuwa ya kawaida, lakini wateja wetu huhisi raha ya ajabu pindi
konokono wanapoendelea kutambaa kwenye nyuso zao kwa matibabu.”
Facial ya konokono ilianzishwa katika saluni
iitwayo Tokyo’s Clinical Saloon nchini Japan na mtu wa kwanza kupatiwa
huduma hiyo alikuwa ni mtu mmoja maarufu nchini humo, Escargot Course
mwanzoni mwa msimu huu na kulipia gharama ya dola 161 sawa na Sh
257,600.
Konokono 60 wanamilikiwa na Gower na wamekuwa wakipewa vyakula maalumu, ikiwemo matunda na mboga za majani.
“Hivi sasa watu wengi nchini Japan wanazalisha
konokono kwa ajili yetu na hata wengine wanazalisha kwa ajili ya chakula
kama utamaduni wetu ulivyo lakini wanatofautiana,” alisema Gower na
kuongeza; “Hii si aina ambayo unaweza ukaipata katika bustani, tumekuwa
tukiwaelekeza tunahitaji wa aina gani, hata hivyo tunawapa majina ya
aina ya konokono tunaowahitaji pia.”
Anasema wafanyakazi wote wa saluni wamepewa
mafunzo maalumu ya kushika konokono wanapomhudumia mteja, wengine
wanajifunzia katika saluni hiyo na baadaye wanakwenda kufanya kazi
sehemu nyingine tofauti.
Hata hivyo kamasi za konokono zinaaminiwa kuwa zina faida kubwa ya kupambana na hali ya kuzeeka.
“Ustawi wa konokono ni muhimu sana kwetu na mara
wanapotumika kwa mteja mmoja tunahakikisha hawatumiwi tena angalau kwa
kipindi cha siku nne, na tunawaangalia kwa kipindi hicho chote kwani
wanakuwa wametoa kamasi kwa wingi mno.”
Gower anasema walihitaji kupata ushauri kutoka kwa
watalamu wa konokono namna ya kuwalisha na kuwatunza, ili wasife na
namna ya kuweza kuwapa chakula kitakachozalisha kamasi kwa wingi na
kusisitiza kwamba wafanyakazi wake wote wameshapatiwa mafunzo hayo.
Baada ya facial
Anasema baada ya kumalizika kwa zoezi la facial
konokono hao hutengwa na wengine ili kupata wasaaa wa kuwapumzisha,
sambamba na kutoa uchafu wote hivyo kuwepo na usalama wa ngozi za wateja
wao.
Hata hivyo, mteja yeyote akishafanyiwa facial hiyo
hushauriwa kutotumia kemikali ya aina yoyote kutokana na ulaini wa
ngozi zao, hivyo iwapo mteja atakaidi agizo hilo hupata madhara katika
ngozi. Gower anasema konokono wana uwezo mkubwa wa kuondoa chunusi
ukilinganisha na mafuta mbalimbali yanayotumika kufanya kazi hiyo hata
bila kuwa na matokeo kwa uharaka.
“Mara baada ya matibabu haya ya asili ngozi ya uso
hubaki katika hali ya uchanga na hupambana na kuzeeka kutokana na
kamasi kuwa na mchanganyiko wa viungo vya aside ya ‘hyularonic.” Anasema
wanapata wateja wengi ambao hawahitaji kutumia kemikali ili kupambana
na kuzeeka kwa ngozi zao.
Dk Chopra ambaye kwa sasa anafanya majaribio ya
kliniki juu ya ufanisi wa kamasi za konokono alisema; “Konokono wana
kamasi zenye antibiotics na asidi ya hyaluronic ambayo huirudisha ngozi
katika uchanga na kuifanya isizeeke kwa urahisi. Tunahitaji kujipanua
zaidi katika hili. Wenzetu Ufaransa wamegundua kwa kuchukua kamasi za
konokono na kuzihifadhi kama bidhaa ya huduma ya facial, lakini sisi
tunatumia konokono halisi.”
Kusinga ‘massage’ ya nyoka
Nchini Tanzania wapenzi wa kusingwa maarufu kama
‘massage’ wamezoea kufanyiwa huduma hiyo na binadamu wenye mikono laini,
lakini hali ni tofauti huko nchini Indonesia ambapo hivi sasa huduma
hiyo imekuwa ikitolewa na nyoka.
Hata hivyo bado wateja si wengi kutokana na woga
wa kung’atwa na nyoka hao. Katika moja ya ofisi zinazotoa huduma hiyo
katika Mji wa Jakarta nchini Indonesia, Feri Tilukay ni mmoja wa wateja
ambaye kutokana na woga amefumba macho huku akiendelea kupata huduma
hiyo kutoka kwa nyoka watatu aina ya ‘enormous’.
Akizungumza na Shirika la Habari la AFP, Tilukay
mwenye umri wa miaka 31 anasema; “Nimejisikia vizuri sana yaani
anatembea huku akikakamaza mwili wangu ni kusinga kwa ajabu kwa kweli.”
Nyoka hao wana majina maalumu, kuna Jasmine, Muscle na Brown
ambao hufanya kazi ya kwanza ambayo itamlazimu mteja kulala chali na wao
kupita juu ya mwili wale. Baadaye hutembea mpaka shingoni na kusinga
kwa muda kisha hushuka mpaka kiunoni.
Kabla ya kuanza kazi nyoka hao hufungwa kwa
mikanda maalumu mdomoni mwao, ili kuhakikisha hawawezi kumdhuru mteja na
hubandikwa plasta maalumu ili kutotoa hata tone la sumu ambayo inaweza
kudhuru ngozi ya mteja.
Matibabu hayo ya dakika 90 hugharimu rupia 480,000 sawa na dola 43 ambapo kwa fedha za Tanzania ni Sh 69,000.
Nchini Indonesia kuna wateja wachache ambapo walio
wengi hutokea bara la Ulaya, Japan au Korea Kusini kwa mujibu wa meneja
wa kituo hicho, Paulus Abraham.
Ingawa watu wengi wanaopata singa katika kituo
hicho cha Bali Heritage Reflexology ni mahiri na wasio na waoga, kituo
hicho kipo katika matangazo ya kuhamasisha watu kusinga hiyo kwani ina
manufaa kwao.
“Nilikuwa na hofu ya nyoka yaani nilikuwa mwoga
sana kwa wanyama hawa lakini baada ya kupata matibabu mara kadhaa
nimekuwa vizuri,” alisema Tilukay ambaye amesingwa na nyoka kwa zaidi ya
mara tatu.
Singa ya nyoka ni moja kati ya matibabu zaidi ya
300 yanayotolewa katika kituo hicho. Huduma hii ilianza kutolewa katika
kituo hicho mwaka mmoja uliopita na imekuwa ikiwavutia wengi.
Nyoka hao wanatunzwa katika nyumba moja
iliyojengwa kwa kutumia mbao katika kisiwa kimoja kilichopo Bali, na
wamekuwa wakilishwa chakula cha sungura ili kuishi.
Hata hivyo haki za wanyama pamoja na watu wa haki
za binadamu wamekuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na tiba hiyo. Watu wa
haki za wanyama wameizungumzia tiba hiyo kama ‘unyonyaji’.
“Tunachukizwa kusikia kuhusu aina yoyote ya
unyonyaji dhidi ya wanyama wakiwamo nyoka,” alisema mmoja wa
wanaharakati hao wa haki za wanyama Benvika.
Hata hivyo, meneja wa kituo hicho Abraham alisema;
“Sisi hatuwachukui kutibu watu kama wafanyakazi, tunawachukulia kama
marafiki zetu au familia,” alisema na kuongeza; “Tunawabusu,
tunawakumbatia na tunawapa huduma nzuri sana.”
No comments:
Post a Comment