KUTOA MIMBA INAWEZEKANA KUZIBA KWA MIRIJA YA KIZAZI
Mirija hii ndiyo inayosaidia kushusha yai kutoka kwenye kokwa na
kupandisha mbegu ili vikutane humo ndani ya mirija na kuumba binadamu.
Tulisema kuwa mirija hii ikiziba baada ya kutoa mimba basi huyu mama au msichana hatapata mimba tena.
Haya ndiyo yaliyomtokea msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja
la Jasinta baada ya kutoa mimba kama anavyotuhadhithia katika stori hii
ya kweli na ya kusikitisha.
Jasinta anajuta kutoa kwake mimba alipokuwa msichana mdogo wa umri wa
miaka 18. Anasema hakujua utoaji mimba unaweza ukawa na matatizo mengi
kama aliyo nayo sasa.
Alipokuwa sekondari alikuwa na rafiki yake wa kiume na mara akapata
mimba. Rafiki yake kusikia ana mimba alimwambia kuwa hana habari naye
tena na baada ya muda hakuonekana tena.
Alijisikia vibaya kuwa ataishije na hiyo mimba, kuilea na kuzaa na
kumtunza mtoto. Ilikuwa ni mimba yenye matatizo, shida na tabu kama zile
12 nilizokusimulia na ukazisoma miezi miwili iliopita.
Jasinta aliishi na wazazi wake na hakuthubutu kuwaambia hata kumwambia
mama yake kwamba ana mimba. Hakukuwa na kliniki ambapo angeweza kwenda
na kujieleza kuwa ana mimba na kupata ushauri juu ya mimba hiyo.
Alimweleza shangazi yake na kumwambia kuwa alitaka kuitoa hiyo mimba.
Shangazi alimwambia kuwa kuna hospitali moja anayoifahamu iliyokuwa
inatoa mimba.
Kwani mwanawe alikuwa na mimba na akaenda kuitoa hapo.
Jasinta anahadithia kwa uchungu yaliyompata.
‘Nilienda hapo asubuhi nikiwa na rafiki yangu. Rafiki yangu hakuruhusiwa
kukaa na mimi wakati wa ‘procedure,’ yenyewe kwa hiyo aliona ni heri
arudi nyumbani na kunifuata baadaye.
“ Nilikuwa peke yangu na waganga (madaktari) wawili wa kiume. Palikuwa pasafi, kila kitu kikionekana kama kina rangi nyeupe.
“Nikawa na matumaini kuwa kila kitu kitakuwa sawa lakini mambo hayakuwa
sawa. Waganga walinilaza kitandani wakanipima na kuniambia kuwa nilikuwa
na mimba inayokaribia miezi minne.
“Walichukua kidonge cheupe cha kuua mimba yenyewe, yaani cha kuua mtoto,
wakakiingiza kwenye kizazi changu. Niliambiwa nipumzike kitandani.
“Baada ya saa nne niliambiwa nihamie kwenye kitanda cha upasuaji ili
mimba itolewe. Nilikuwa mimi na madaktari hao wanaume wawili.
“Walinipiga sindano ya kunifanya nisisikie maumivu lakini wakati wote
nilikuwa macho kabisa nikiona na kusikia kila kitu. Yote niliyoona
yalitisha.
“Damu, uchafu uchafu, vipande vipande vya mwili wangu na vya mwili wa
mtoto wangu vikiwa na damu kila pahala, ilikuwa ni hali ya kutisha.
“Kama ningejua kuwa ‘procedure,’ yenyewe ya kutoa mimba ni yenye maumivu
na matatizo kiasi hicho ni heri tu ningeiacha mimba yangu ikue, nizae
na kulea mtoto.
“Baada ya muda nikaanza kusikia maumivu. Wakaniambia nivumilie maana ilikuwa lazima kuharakisha na kumaliza shughuli yenyewe.
“ Baada ya kumaliza maumivu yalizidi, nafikiri ni ile dawa ya ganzi
iliisha, walinipa kidonge cha Panadol nikaendelea kuumwa huku damu
ikinitoka.
“Wakati wote nilifikiria kuwa hospitali hii haikuwa inanipa huduma
nzuri. Kwa nini hawakunipa dawa ya kutosha kuua, kumaliza au kupunguza
maumivu? Walinirudisha kitandani nipumzike.
“Saa 12 jioni nilipopewa ruhusa mwenzangu alinifuata lakini waliponiruhusu kwenda nyumbani niliwaambia bado damu inatoka.
“Wakaniambia nisiwe na shaka, itaisha baadaye. Baada ya siku mbili bado
damu ilikuwa inatoka nyingi na nilikuwa naumwa tumboni sana. Nilikuwa
najisikia kama nina homa, nilirudi hospitalini pale wakanifanyia CT
scan.
“Waliona bado kulikuwa na vitu yilivyobakia ndani ya kizazi changu.
Wakaanza tena upya kutoa vilivyobakia ndani. Walinilaza kitandani na
kunipa sindano ya kupunguza maumivu.
“Nikiwa macho kabisa wakaendelea kutoa yaliyobaki humo ndani. Nakwambia
niliumwa, niliumwa sana. Maumivu yalikuwa makubwa kuliko ya siku ile ya
mwanzo. Niliwasikia wakiambiana kuwa sihitaji kuongezewa damu.
“Ukweli kama nilihitaji huduma ya kuongezewa damu ingebidi wazazi wangu
waambiwe nimetoa mimba na nahitaji kuongezewa damu. Aibu! Aibu! kwenye
familia. Sijui ningeweka uso wangu wapi hapo nyumbani kwa baba yangu.
Matatizo ya utoaji mimba niliofanya nikiwa na umri wa miaka 18 sasa
yamenifuata nikiwa na umri wa miaka 28. Sasa nimeolewa na kwa muda wa
miaka miwili natafuta mtoto. Wenzangu nilioolewa nao tayari wameishabeba
mimba na wengine wamekwisha kuzaa wakati mimi bado nahangaika,”
anasema.
“Nilienda Hospitali ya Marrie Stopes...nilikuwa na wasi wasi labda wale
waganga wakati ule nilipotoa mimba walinitoa kizazi changu.
“Huko Marrie Stoppes wamenipima vizuri sana na kuona bado kizazi changu
kipo. Lakini basi, mirija ya kizazi imeziba. Imeziba kwa sababu ya ile
shughuli niliyofanya miaka 10 iliyopita.
Anasema daktari wa Marrie Stoppes alimuuliza kama ameshawahi kutoa mimba
na alipomjibu ukweli alionekana kama anatingisha kichwa chake, akasema,
“Kumbe ndiyo sababu mirija imeziba.”
“Siwezi nikapata mimba tena. Hakuna habari ya mimba tena kwangu. Ile
mimba niliyotoa ilikuwa ni mimba yangu ya kwanza na ya mwisho. Ningejua
kuwa kuna uwezekano wa kutopata mimba tena nigeiacha ile mimba tu wakati
ule.
“Ningeilea kwa njia yoyote tu. Niliitoa na sasa sipati nyingine tena.
Mtoto aliyeuawa na kutolewa kwenye mimba ile angekuwa na miaka 10 sasa.
Sijui hata alikuwa wa jinsia gain, sijui wa kiume au wa kike.
Anasema hawezi kupata mtoto na hajui ndoa yake itakuwaje bila mtoto.
Hajui mume wake atajisikiaje akijua kuwa hataitwa baba watoto na yeye
haitatokea aitwe mama watoto.
Jasinta anaendelea kusema: “Kinachonifanya kujisikia vibaya ni kwamba
sikuweza kupata habari popote juu ya utoaji wa mimba kuwa inatolewaje na
kuna matatizo gani yanayoweza kutokea.
“Ningejua kunaweza kutokea matatizo haya na yale ningeweza kufikiria vizuri na kuamua kutoitoa,” anasema.
Jasinta anasikitika kuwa alikwenda kutoa mimba bila kujua kuwa wanafanya
nini katika shughuli hiyo na utoaji mimba una madhara gani.
Baada ya kujua kuwa utoaji mimba unaambatana na matatizo makubwa kama
yale tuliyoandika kwenye makala mbili zilizopita na hili kubwa
alilotuhadithia Jasinta, inabidi tuseme kuwa utoaji mimba ni kitu
ambacho kisingepaswa kufikiriwa kabisa katika kutatua tatizo la mimba
ambayo haikutarajiwa.
Wengine wanasema ni kitu ambacho hakipo kwenye listi mojawapo ya vitu
vya kufanya kama mimba haikuwa kwenye mpango,” kwani madhara yanayotokea
ni makubwa mno.
Acha mimba ikue, uzae utakuja kuona baadaye faida uliyopata kwa kuicha
ikue na kuzaa. Ukiitoa kama hutapata matatizo ya kifo baadaye utakuja
kuona hasara zinazotokana na kutoa hiyo mimba.
Wanawake wengi wanaona kutoa mimba kama ni jambo la kawaida sana. Huenda
kwenye vihospitali vya mitaani wanapotoa mimba na kujipatia huduma hiyo
bila kujua matatizo yanayoweza kutokea wakati wa kutoa na baada ya
kutoa mimba.
Wengine huenda kwenye hospitali nzuri tu kama alivyoenda Jasinta lakini
ukweli ni kwamba hata kwenye hospitali kubwa na nzuri kuna hatari wakati
wowote kupata matatizo wakati wa kutoa mimba na baada ya kutoa mimba.
Utoaji mimba kwa kweli si vizuri. Ni ‘procedure,’ yenye matatizo mengi.
Ni heri uiache mimba yenyewe ikue na uzae hata kama umeipata bila
kukusudia.
Wiki ijayo tuzungumzie juu ya kifo na kupoteza maisha wakati wa kutoa mimba.
No comments:
Post a Comment