TTCL

EQUITY

Tuesday, October 15, 2013

MAKALA

Kisumo: CCM inaweza kung’oka madarakanI

Peter Kisumo akizungumza na timu ya waandishi wa habari wa mwananchi nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Picha na Sulvan Kiwale 
 
Na Waandishi Wetu, unbounderiesnews

Dar es Salaam. Mwanasiasa na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo ameonya kuwa chama hicho kinaweza kuondolewa madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Dar es Salaam kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere inayoadhimishwa leo.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba kimemeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini. Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
Alitoa mfano wa tuhuma za baadhi ya viongozi wa Serikali kuficha mabilioni ya shilingi kwenye benki za Uswisi, kuwa zinaweza kuwa kete muhimu ya kuwaingiza Chadema madarakani, iwapo Serikali ya sasa haitawashughulikia wahusika.
“Wakijitokeza na kuwataja majina wahusika, wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi, na Serikali ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani tutawakamata, wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema na kuongeza: “Wakishinda uchaguzi hata kwa viti vichache tu, watakosa nguvu bungeni, lakini kwa wananchi watakuwa na nguvu sana.
Hii inaweza kuwasaidia kwa miaka mitano ya kwanza. Wanaweza kupata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya pili na wakiingia madarakani watawafunga viongozi wa zamani kweli.”
Mzee Kisumo anasistiza, “Hili linawezekana. Anayesema uwezekano wa CCM kushindwa haupo, anajikana mwenyewe. CCM inabidi ijihami na majibu ya jinsi inavyotumia rasilimali za nchi.”
Alionya kuwa si vizuri kuishia kujinadi kwa mambo mengi mazuri iliyofanya huko nyuma, akitolea mfano kuwa hiyo ni sawa na nguo nyeupe ambao ikiingia doa moja tu inakuwa haitamaniki tena.
“Sisemi kwamba hawajafanya kitu, yapo mengi mazuri waliyoyafanya, lakini ufisadi ni sawa na doa kwenye shati jeupe ambalo huwa linaonekana kuliko weupe na ung’avu wa shati hilo,”alisema Kisumo.
Alisema katika siku za karibuni ufisadi umekuwa jambo la kawaida, hadi umegeuzwa kuwa wa kitaasisi, ambapo aligusia hata Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulioanzishwa na Bunge kuwa ni sehemu ya ufisadi.
Alihoji iweje fedha za umma zitumike kumsadia mtu mmoja kujiimarisha kisiasa, akisema hiyo ni ‘Built in Corruption’.
Mzee Kisumo pia alizungumzia mvutano ambao umekuwa ukijitokeza kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwamba msingi wa mvutano huo ni kuwapo tabaka la wahalifu wasioweza kuguswa na sheria.
“Unapokuwa na mvutano huo una maana mbili, kwanza ni hali kwamba huyo mmoja anajua sabababu za watuhumiwa kutochukuliwa hatua, lakini pili ni kwamba huenda tuna watu wawili katika nafasi hizi, lakini wana nia mbili tofauti,”alisema Kisumo na kuongeza:
“Ni hatari sana unapokuwa na mfumo kwenye nchi ambao unawalinda baadhi ya wahalifu, unakuwa na wahalifu wanaoguswa na wengine hawaguswi, watu wanasubiri pengine itokee siku waone mtu wasiyemtarajia anafikishwa mahakamani na hapo watajua kwamba kweli nchi imeamua kupambana na rushwa na ufisadi.”
…Aonya Zanzibar
Mzee Kisumo pia alizungumzia mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya na kwamba mvutano kuhusu muundo wa Muungano ni matokeo ya upande wa Zanzibar kuachiwa kufanya vitendo vingi vinavyoashiria kutafuta uhuru kamili kama nchi nje ya Muungano huo.
Vitendo hivyo kwa mujibu wa kada huyo ni mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ambayo yalitamka kuwa Zanzibar ni nchi, kurejesha bendera yake, wimbo wake wa taifa na mambo mengine.
“Katika hatua sasa Zanzibar wanajiona kwamba wamekaribia kutimiza azma yao, kuelekea katika ‘uhuru’ kamili, nasema whoever (yeyote) aliyefumbia macho vitendo hivi akiwa Rais, alifanya makosa makubwa,”alisema Mzee Kisumo na kuongeza:
“Ukitafakari hali hiyo, kama tukiwa na mfumo wa Serikali Tatu, ni kitu gani kitawazuia Tanganyika nao wasidai kuwa na Katiba sawa na ile ya upande wa pili? Ikifika hapo mimi sioni Muungano kuwapo.”
Hata hivyo, alionya kuwa masuala yote yanayohusu Muungano ikiwa ni pamoja na lile la mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar, yanapaswa kufanyiwa uamuzi wa busara kwani historia inaonyesha kuwa kuvunja Muungano wowote ule lazima damu imwagike.
“Muungano wa States (nchi) za Marekani uligharimu umwagaji damu, United Kingdom (Uingereza) pia damu ilimwagika, kwa hiyo lazima tujifunze kwamba ikiwa tutafikia hatua ya kuvunja Muungano wetu, hatuwezi kupita salama katika hili,” alisema.
Alisema kinachotokea sasa kuhusu Zanzibar kuwa na mwelekeo wa kujitenga, ilianza katika chaguzi zilizopita, pale ambapo Mzanzibari aliyekaa nje ya visiwa hivyo kwa zaidi ya miaka mitano anakosa haki ya kupiga kura kwa kukosa sifa ya ukaazi.
“Hili nalo ni tatizo kubwa, Mzanzibari ambaye ameamua kuishi Moshi, Morogoro au kwingineko nchini uhalali wake wa kuwa Mzanzibari unawekwa shakani, kwani hawezi kupiga kura kama hajaishi Zanzibar mfululizo kwa kipindi hicho,” alisema Mzee Kisumo na kuongeza:
“Ukiangalia kwa Mtanzania wa Bara, hakutani na kadhia hii, yeye ataishi popote hata kama nje ya nchi kwa muda wowote, lakini akirudi nyumbani haambiwi eti si mkaazi, kama ni Tabora atakwenda kwao au Mbeya”.
Mzee Kisumo alisema kutokana na hali hiyo kuna kundi kubwa la Wazanzibari ambalo linajikuta katika hatari ya kukosa haki zao na kwamba ikiwa kutakuwa na mfumo wa Serikali Tatu na upande wa Tanzania Bara kuanzisha utaratibu kama wa Zanzibar, watajikuta kwenye utata wa uraia wao.
“Tukiwa na Tanzania moja iliyoungana, ambayo watu wake hawana mwelekeo wa kuangalia masilahi yao zaidi, haya mambo hayawezi kutokea. Kimsingi mtu yeyote ambaye ni raia wa Tanzania anapaswa kujivunia uraia wake kama Mtanzania na hapaswi kuishi kwa vikwazo vya aina hii,”alisema Kisumo na kuongeza:
“Kwa hiyo mimi nasema haya mambo lazima… Lazima tuyatizame kwa upana wake….Maana hawa watu wapo wanaathirika, sihitaji kutaja majina ya watu hapa, lakini wapo, wanafahamika na wengine ni wafanyabiashara wakubwa sana nchini, wametoka Zanzibar na wameishi Tanzania Bara kwa miaka mingi.”
Kisumo alionekana kukerwa zaidi na pendekezo la kuwapo kwa Serikali ya mkataba na kusisitiza kuwa wanaotoa mawazo ya aina hiyo wanakusudia kuvunja Muungano kwa masilahi yao binafsi.
... Asema Nyerere alijaa katika mioyo ya Watanzania
Wakati taifa leo linatimiza miaka 14 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Kisumo anasema kuwa kiongozi hiyo alikuwa na sifa nyingi ambazo zilimfanya kujaa mioyoni mwa wa Watanzania.
Akizungumzia sifa za Nyerere kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika iliyokuja kuwa Tanzania baadaye , Kisumo anaeleza kiongozi huyo alikuwa na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake na Bara la Afrika kwa jumla.
Kisumo, ambaye alifanya kazi na kiongozi huyo kabla na baada ya uhuru, alisema sifa nyingine ya Mwalimu Nyerere ilikuwa uwezo wake wa kushawishi na kuongoza.
“Nyerere pia aliamini katika umoja wa taifa na uongozi wa pamoja na ndio maana alifanikiwa katika nyanja nyingi,” anasimulia Kisumo, ambaye alianza siasa kupitia kwenye vyama vya wafanyakazi akiwa na Waziri Mkuu wa zamani, Rashid Kawawa na Marehemu Michael Kamaliza katika miaka ya 1950.
Kisumo anasema bila ya kificho kuwa marais waliomfuatia Nyerere wameshindwa kufikia sifa ya Mwalimu hasa linapokuja suala zima la sifa za uongozi.
Alitoa mfano kitendo cha Nyerere kwa kutumia lugha ya Kiswahili na kuunganisha watu wa Tanganyika kupigania uhuru bila ya kumwaga damu kutoka kwa Waingereza.
“Alipigania uhuru bila ya kuwa na jeshi au silaha unaweza mwenyewe ukamfikiria mwenyewe Mwalimu alikuwa ni kiongozi wa aina gani?
“Nyerere aliunganisha machifu waliokuwa na nguvu sana katika kipindi kile ingawa alipingwa na baadhi yao kama Chifu Thomas Marealle wa Moshi.
“Huyu Chifu Marealle alikwenda mbali zaidi na hata kwenda kwenye Umoja wa Mataifa nchini Marekani na kueleza kuwa Tanganyika haikuwa tayari kujitawala, lakini alishindwa kwa hoja za Mwalimu,” aliongeza Kisumo, ambaye alishika nyadhifa mbalimbali wakati wa uongozi wa Nyerere zikiwamo za Uwaziri na Ukuu wa Mkoa.
Kisumo anaeleza kuwa Mwalimu aliwazidi kete Waingereza kwani alipenya katika asasi mbalimbali za Watanganyika.
“Mwalimu alitumia michezo kudai uhuru, alikuwa karibu sana na klabu ya Yanga pia hata vikundi vya muziki wa dansi na taarabu,” aliongeza Kisumo.
Kisumo anasimulia kuwa baada ya Tanganyika kupata uhuru bado Nyerere alisaidia mataifa mengine katika harakati zao za kupigania uhuru wao na alitaka Umoja wa Afrika na ndio maana akaasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Ukombozi wa Afrika
Alisema Nyerere alikubali Kamati ya Ukombozi ya iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) iweke makao makuu yake jijini Dar es Salaam.
“Kilikuwa kitendo cha hatari kwani mataifa mengi wakati ule hayakukubali kupokea wapigania uhuru kwa kuhofia usalama wa nchi zao.
“Vyama mbalimbali kutoka nchi za Afrika Kusini, Angola, Msumbiji na Namibia vilileta watu wao kwa mafunzo ya kijeshi, jambo ambalo lilitutisha wakati ule,” anaongeza Kisumo.
Kisumo alisimulia kuwa Nyerere alisimamia umoja na ukombozi wa Bara la Afrika na kumfanya ajizolee sifa sawa na marais wengine kama Gamal Abdel Nasser wa Misri, Ben Bella wa Algeria na Kwame Nkrumah wa Ghana.
Kisumo alisema kuwa Mwalimu hakuishia kuunga mkono wapigania uhuru wa Afrika pia aliunga mkono harakati za Wapalestina kujikomboa kutoka kwa Israel, ambayo katika miaka ya mwanzo wa Uhuru ilikuwa kati ya wafadhili wakubwa wa Tanzania.
“Nakumbuka Kiongozi wa Chama cha Ukombozi cha Palestina (PLO), Yasser Arafat alialikwa katika moja ya mikutano ya chama cha TANU iliyofanyika jijini Dar es Salaam,” anaongeza Kisumo.
Sera za uchumi
Kisumo anasema kuwa Nyerere alikuwa anaamini kuwa Tanzania itaendelea kiuchumi kama itawekeza vya kutosha katika kilimo.
“Ndio maana katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru tulikuwa na sera ya `Siasa ni Kilimo’ na baadaye `Kilimo cha Kufa na Kupona’,” alisema Kisumo.
Kisumo alisema kuwa baada ya kampeni ya kilimo, Nyerere aliona umuhimu wa kujenga viwanda ili kutumia malighafi iliyotoka katika kilimo.
“Ndio maana ukaona tukajenga viwanda vya nguo katika Miji ya Dar es Salaam, Arusha, Musoma na Mwanza pia kiwanda cha nyuzi pale Tabora,” alisema.
Pia Kisumo alisema kuwa Mwalimu aliweka mkazo katika elimu ya kujitegemea ili kumwandaa kijana wa Kitanzania.
“Hivi majuzi nilisikitika sana baada ya kusikia ikiwa shule moja huko Kigoma imepokea msaada wa vyoo vya shimo kutoka kwa Wachina! Hivi kweli imefika mahali wanafunzi wetu wanashindwa kuchimba vyoo?” alihoji Kisumo kwa masikitiko.
Kisumo alisema kuwa mambo yalibadilika katika miaka ya 1990 wakati Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Margareth Thatcher alipoanzisha sera za ubinafsishaji na utandawazi.
“Hapo ndio yakabadilika ambapo mataifa makubwa yakazidi kuzikandamizia nchi changa kupitia misaada ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),” alisema Kisumo.
Kisumo alisema Mwalimu alipambana na mataifa hayo makubwa na kutaka kuacha kukandamiza nchi changa. Alipambana na mataifa kupitia Tume ya Kusini 1986, taasisi ambayo ilitokana na uliokuwa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM).
Imeandikwa na Neville Meena, Samson Mfalila na Regnald Miruko.

No comments:

Post a Comment