ELIMUni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia
ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu
ni njia ambayo hutumiwa kimakusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na
maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.
Haki ya kusoma imeweza kuelezwa kuwa haki ya kimsingi ya binadamu
katika kifungu cha pili cha itifaki ya kwanza ya maagano ya haki za
binadamu barani Ulaya kuanzia mwaka wa 1952 ambapo wanachama wote
wanashurutishwa kuhakikisha elimu kwa wote. Katika kiwango cha
kimataifa, Mapatano ya Umoja wa Mataifa ya haki za kiuchumi, kijamii na
utamaduni katika mwaka wa 1966 yanahakikisha haki hii katika kifungu cha
13. Wanafunzi ama vijana waliopo vyuoni ama shuleni pia wanahitajika
kujua umuhimu wa wao kuwa ni sehemu ya jamii ya uongozi katika familia,
jumuiya mbalimbali na pia kwenye mamlaka za taifa na kimataifa. Hayo
ndiyo matokeo ya elimu yanayohitajika. Elimu ya sayansi ya jamii ni somo
muhimu linalounganisha jamii bila kujali rangi, kabila ama elimu yao,
hivyo wasomi wanalo jukumu la kuiunganisha jamii si kujitenga na jamii
tena kwa kujenga kuta ndefu kuzingira nyumba zao!. Hivyo elimu ya
shosholojia ni muhimu kuzingatiwa miongoni mwa wasomi. Sosholojia ya
elimu ni somo linalohusu jinsi taasisi za kijamii huathiri michakato na
matokeo ya elimu, na kinyume chake. Kwa wengi, elimu hueleweka kama
mbinu ya kushinda vizuizi, kufanikisha usawa na kupata amani na hadhi
kwa wote (Sargent 1994). Wanafunzi wanaweza kutiwa motisha na tamaa ya
maendeleo na uboreshaji. Elimu hutambuliwa kama mahali ambapo watoto
huweza kujikuza kulingana na mahitaji yao ya kipekee. Jukumu la elimu
laweza kuwa ni kukuza mtu binafsi hadi kilele. Uelewa wa shabaha na
mbinu za michakato ya utangamano wa kielimu hutofautiana kulingana na
dhana ya sosholojia iliyotumika Hali kadhalika kwa wasomi wenye malengo
ya kuwa viongozi katika mamlaka ama taasisi mbalimbali sharti watambue
elimu ya sayansi ya jamii ni sehemu ya weledi katika uongozi, ingawa
kiongozi si yule tu mwenye madaraka, bali sifa ya kiongozi ni kuongoza
wengine katika njia sahihi. Mwanafalsafa Plato anaamini katika kanuni
yake kwamba binadamu aliumbwa kuishi kijamii na wengine wanaamini jukumu
kubwa la taifa ni kuundwa kwa Serikali sahihi na kamili lenye raia wake
itakayowahakikishia amani na usalama katika maisha yao ya hapa duniani
na ya mbinguni pia. Mintarafu ya uongozi katika taifa lolote sharti
kiongozi mkuu na mwenye sifa za kutawala awe: “mwenye busara na uwezo wa
kutumia akili yake vizuri sana, mwenye kumbukumbu sahihi ya mambo,
mwenye uwezo mkubwa wa kueleza mambo, asiyerukia mambo na kutoa maamuzi
bila kutafiti, mwenye kujirudi na kushaurika, mkarimu na mpole kwa raia
wake, mpenda kutenda na kutendewa haki, mwenye msimamo na asiye dhaifu
katika kutekeleza maamuzi au maazimio yaliyokubalika.” Kama akikosekana
mtu mmoja mwenye sifa hizo zote, hapo itabidi watafutwe watu wawili au
watatu au wengi zaidi, ambao kwa pamoja, kutokana na sifa za mmoja
mmoja, wanaweza kuzikamilisha na hivyo wapewe dhamana ya kuunda Serikali
ya Taifa hilo. Hapo zamani kabla ya kuwepo kwa somo la Sosholojia
(sociology) kama lijulikanavyo hivi leo, kabla hata ya maelezo ya akina
Comte, Vico, Marx na Spengler, inaelezwa kulikuwepo na watalaamu wengine
ambao walishaelezea historia, na hatua za maendeleo ya jamii ya
wanadamu, na walijaribu kutoa maelezo ya kina kuhusu umuhimu wa somo la
Historia na maendeleo yake kwa siku zijazo. Kwa kweli, ni kazi yenye
maelezo kuhusu mambo mengi na yaliyoelezwa kifasaha ambapo historia
yenyewe imeelezewa kuwa ni sehemu ya somo la Falsafa kwa maneno
yafuatayo: “Hebu tutazame undani wa somo la Historia”, anasema Ibn
Khaldun na kwamba; ‘’ni uchunguzi na uthibitisho wa taarifa, uchunguzi
makini wa sababu za kuwepo kwa mambo (kama yalivyo) na werevu wa kina wa
jinsi mambo yalivyoweza kutokea. Hivyo, Historia ni mojawapo ya sehemu
za somo la Falsafa, na inapaswa kutambuliwa kama mojawapo ya elimu ya
sayansi.” Hii ndiyo dhana ya kileo juu ya somo la Historia, kutokana na
kuona umuhimu na nafasi yake katika uchambuzi wa taarifa mbalimbali na
kutafuta chanzo au sababu za mambo. Historia inapaswa kuwa ni elimu ya
kudumu katika ustaarabu wa mwanadamu na saikolojia yake. Ni vigumu
kuweza kuchambua kwa kina kazi kubwa waliyoifanya baadhi ya wachambuzi
ama waandishi wa historia na kwamba huenda si mambo yote yalipata nafasi
ya kuhifadhiwa katika kumbukumbu. Chunguzi za uadilifu juu ya upoteaji
na uharibifu wa staarabu mbalimbali, katika mzunguko, na mchango mkuu wa
wasomi katika uundaji wa mataifa mbalimbali. Kujitambua na kutambua
mambo kwa ajili ya mafundisho ya kizazi kijacho ndio mwenendo muhimu
uliotiliwa maanani na wasomi wa ‘kale’ kama ambavyo wasomi wa sasa
wanavyotakiwa kuwa mfano wa mazao bora kwa msaada wa akili kwa wengine.
Mmoja wa wasomi na waandishi wa historia alipindukia pale alipoainisha
maisha ya taifa lolote na ya watu au ya kiumbe kingine chochote, kwamba
hata mataifa yanazaliwa, yanakua na yanakufa. Pia kwamba mataifa yako
chini ya kanuni ya mabadiliko asilia. Ibn Khaldun anatajwa ni mmoja wa
wahusika na uvumbuzi wa kanuni hii ya mabadiliko ya taifa lolote. Mawazo
yake ya kiuchumi kama ya kisiasa, yameendelea kutumika hata leo.
Mwandishi huyu kutoka iliyokuwa ikiitwa Maghreb (Morocco) anasema:
“Taifa ni sawa na mfanyabiashara mkubwa, kwani ana jukumu la kuhakikisha
kuwa pesa azipatazo kutokana na kodi, zinarudi na kuwazungukia watu.
Kodi za wastani ni motisha tosha ili watu waweze kujituma katika kufanya
kazi. Kwa upande mwingine, kupandisha kodi yoyote tena kiholela holela,
kunaweza kusababisha yasipatikane mafanikio ya malengo ya kodi husika.”
Hivyo elimu ya siasa na sayansi ya jamii haviwezi kutenganishwa,
kwakuwa siasa inahusu watu miongoni mwa watu na sayansi ya jamii ni ule
uhusiano wa jamii yenyewe katika mambo mbalimbali ya kimaisha, kwa
sababu hiyo ni muhimu kwa wanafunzi kuelewa baada ya kuwa wanafunzi
wanatakiwa kuishi kwa sura ipi kadri ya viwango vyao vya elimu, lakini
vyenye matokeo ya elimu ya kuishi kijamii.
No comments:
Post a Comment