Wimbo
wetu wa Taifa unaanza na Mungu Ibariki Afrika kabla ya Mungu Ibariki
Tanzania katika ubeti wa pili. Hii iliwekwa kwa kusudio. Afrika
ilitangulia kwanza. Wakati Raila Odinga aliponyimwa nyaraka za kusafiri
na serikali ya kikoloni ya Kenya, nchi yetu ilimpa pasi ya kusafiria, ya
nchi yetu. Mifano kama hii ipo mingi kuonyesha utayari wa siku zote wa
Tanzania kutanguliza mbele ushirikiano na umoja na nchi nyingine za
Afrika. Wakati taifa lilipokuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi
miaka ya 1970 bado nchi yetu ilitoa fedha kusaidia wapiganaji wa
ukombozi Zimbabwe na Msumbiji. Mojawapo ya mkutano muhimu katika
historia ya chama cha ANC cha Afrika Kusini wa kuamua mwelekeo mpya wa
mapambano ya uhuru wa kutumia silaha pia ulifanyika hapa Tanzania,
Morogoro mwaka 1969, kadi ya chama cha FRELIMO ya mpigania uhuru wa
Msumbiji, hayati Samora Machel alipewa kwa mara ya kwanza akiwa Dar es
Salaam, tarehe 22 Februari 1965. Mwalimu Julius Nyerera alikuwa tayari
kuahirisha uhuru wa nchi yetu ili kusubiri Kenya na Uganda, tupate uhuru
siku moja na kutangaza nchi moja ya Afrika Mashariki siku hiyo. Suala
la msingi ni kwamba kizazi cha vijana wa sasa Afrika kina jukumu na
nafasi ya kuifanya Afrika kuwa moja.
No comments:
Post a Comment