Ingawa mara nyingi husemwa kuwa hakuna
usalama wa asilimia mia moja kwenye ulimwengu wa teknolojia ya kompyuta,
ila kinga ni bora kuliko tiba.
Umewahi kujiuliza kwa nini watu wengi wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ya makazi?
Ndivyo ilivyo, tembelea hata katika makazi ya watu
wa kawaida, madirisha yamejaa nondo, nyumba zimezungukwa na kuta
ndefundefu. Wengine wamefikia hatua ya kufuga mbwa kwa ajili ya
kuwalinda.
Nimeanza kwa kutoa mifano hii kuonyesha umuhimu wa
kuzilinda kompyuta zetu. Ingawa mara nyingi husikika ikisemwa kuwa
hakuna usalama wa asilimia mia moja kwenye ulimwengu wa teknolojia ya
kompyuta, ila kinga ni bora kuliko tiba.
Cha msingi ni kufuata tu kanuni, kwani kwa kufanya
hivyo unaweza kwa kiasi kikubwa kuepukana na mambo mengi yanayoweza
kuhatarisha usalama wa kompyuta yako kama vile athari za virusi.
Makala haya yanataja baadhi ya kanuni za msingi unazopaswa kufuata ili kutunza usalama wa kompyuta yako.
Tumia programu unazozihitaji
Watumiaji wengi wa kompyuta tumekuwa waathirika wa
matatizo ya kompyuta zetu ama kwa kujua au kwa kutokujua. Kwanza
ieleweke kuwa kompyuta nyingi zimekuwa zikiathiriwa kiusalama kwa
makosa yaliyomo kwenye kompyuta husika.
Hizi ni zile kompyuta zenye programu ambazo
hazijaandikwa kiusahihi. Tuchukue mfano wa nyumba inayovuja, kwa kuwa
tu paa lake halikuezekwa ipasavyo. Au ukuta wa nyumba unavyoweza
kuanguka, kwa kuwa haukutengenezwa kwa kufuata taratibu za ujenzi.
Kama kompyuta yako ina programu ambayo
haikuandikwa kwa usahihi, matatizo mengi hutokea yanayoweza kuhatarisha
kifaa hicho. Programu hizi sio tu zitahitilafiana na mtambo endeshi (OS)
wa kompyuta yako, pia zinaweza kutoa mianya kwa wavamizi kuingia
kwenye kompyuta yako kupitia kwenye mianya iliyopo kwenye programu
hizi.
Cha kufanya: Mosi, ondoa programu usizotumia.
Tuache tabia ya kuweka programu nyingi katika kompyuta zetu ambazo kwa
hali ilivyo hatuzitumii kabisa. Kwa kawaida programu hujaza nafasi,
kuweka uchafu na hatimaye kuiweka kompyuta matatani.
Kumbuka unapoweka (install) baadhi ya programu
katika kompyuta yako, nazo huweka programu nyingine zinazoambatana nazo
bila ya wewe kujua. Hatimaye unajikuta umelundika lundo la programu.
Tumia programu halisi
Tumia programu za uhakika
Tuangalie mfano huu; unapoweka programu ya Microsoft office,
tafiti zinaonyesha watumiaji wengi hutumia programu kubwa tatu ambazo
ni Word, Excel na Power Point.
Ieleweke kwenye kila bunda la programu ya
Microsoft kuna programu nyingine zaidi ya kumi ndani yake ambazo zote
huwekwa pamoja, lakini hazitumiwi kabisa au zinatumiwa mara chache mno.
Wataalamu wanashauri tunapotaka kuweka programu
tuchague kile kwa kuzingatia kile kinachojulikana kama ‘custom
Installation’. Uwekaji wa aina hii siyo tu unaweza kukuelekeza wapi
uweke programu, bali pia utaweza kuchagua aina ya programu unazotaka
kuweka kwenye kompyuta yako.
Pili, hakikisha unatumia programu zinazokwenda na
wakati. Fanya uboreshaji wa matoleo mapya ya programu unazotumia
(update)unapohitajika. Tuache hofu ya kutumia uboreshaji kwa hofu ya
kufutiwa usajili wa programu au labda yataathiri kompyuta yako.
Cha muhimu kuzingatia ni kuwa kila yanapotoka matoleo mapya, wahusika wanalenga kutusaidia watumiaji na siyo vinginevyo.
Tumia programu halisi
Hakikisha unatumia programu halisi au kuichukua
moja kwa moja kutoka kwenye wavuti ya watengenezaji au sehemu salama
kama ilivyoelekezwa na mtengenezaji.
Kuwa na programu halisi sio tu itaiwezesha
kompyuta yako kuwa imara, bali pia itakuwezesha kupata maboresho pindi
yanapotoka kama tulivyoelezea hapo juu. Kiuhalisia, programu nyingi
bandia (siyo zote) huvunja mfumo asili wa programu na kuifanya iwe
dhahifu, huku nyingine zikipandikiza minyoo kwa mtindo wa viraka (patch)
inayokwenda kuharibu mwendendo wa programu halisi.
Kwa mtindo huu unarahisisha kifaa chako
kushambuliwa. Hivyo, matumizi ya programu bandia hasa kwa mitambo
endeshi ni hatari kwa usalama wako.
Leo hii katika baadhi ya ofisi, wataalamu wa
Tehama huweka mitambo endeshi bandia bila uongozi kufahamu, hivyo
kuiweka kampuni kwenye hatari ya uvamizi.
Ushauri kwa wenye kampuni, wahakikishe wanatafuta
Mkaguzi wa Tehama (IT Auditor) afanyie tathmini ya vifaa vyote ili
kubaini dosari kama hizi.
Tumia programu za uhakika
Umewahi kujiuliza kwanini natumia programu hii badala ya ile?
Ukuaji wa teknolojia umesababisha kila mtu kuja na programu yake. Kwa
mfano, kuna zinazotolewa bure au zinazouzwa kwa bei ya chini. Kumbuka,
programu ya uhakika siyo lazima iwe inauzwa, kuna programu nyingi
zinauzwa kwa bei ya juu, lakini zimekuwa na matatizo mengi kuliko
zinazotolewa bure.
Kuhusu programu zinazotolewa bure, siyo kama
hazina ubora, natoa rai kwa watumiaji kufanya utafiti kabla ya kuamua
kutumia programu fulani.
Tena siku hizi ‘mtandao wa google’ unaweza
kukusaidia kwa kiasi kikubwa kufanya utafiti na hata kujua maoni ya
watumiaji wa programu husika.
Nitoe mfano dhahiri. Niliwahi kutumia Windows XP
siku za nyuma. Nilipotaka kubadilisha mtambo, nikagundua watu wengi
walikuwa wakilalamika kuhusu Windows Vista.
Baada ya kufanya utafiti nami nikabaini kuwa
Windows Vista ingenisumbua, hivyo nilighairi kuitumia ingawa ilikuwa na
mwonekano mzuri. Jambo la kushukuru ni kwamba kampuni husika (Microsoft)
nayo ilibaini tatizo hivyo ikaiondoa Windows Vista sokoni na kuingiza
Windows 7 ambayo imekuwa ikipendwa na watumiaji wengi.
Fahamu unachokifanya
Utafiti wangu unaonyesha watumiaji wengi wa
kompyuta tumekuwa waathirika kutokana na kukubali kiholela au kufanya
mambo tusiyoyajua.
Nitoe mfano kuhusu hili. Jamaa yangu wa karibu
aliwahi kuvamiwa na programu za matangazo (adware).Alipofungua tovuti
fulani akakumbana na tangazo lililomwelekeza kubonyeza mahala fulani kwa
kuwa tangazo lilimwambia kompyuta yake ilikuwa katika hatari.
Bila kujua anachokifanya akabofya na kujikuta
ameshaingiza madudu kibao katika kompyuta yake. Hivyo kuwa makini kila
unapokabili ujumbe wowote. Hakikisha unasoma na unajua unachokifanya na
wala si kubonyezabonyeza.
Haya ni mambo machache unayotakiwa kuzingatia ili kuhakikisha kompyuta yako iko katika mazingira salama na yenye kinga.
No comments:
Post a Comment