Ugonjwa wa selimundu unasumbua wengi, umetengua ndoa za wengine, kwa sababu ya kutojua.
Hakuna shaka kwamba umewahi kusafiri nje ya nchi yako na kutakiwa kupata chanjo.
Kwa wengine, chanjo hiyo ikiwamo ya homa ya ini
imeonekana kama usumbufu na udhia mtupu. Hata hivyo, wapo wengine ambao
hawaufahamu ugonjwa huu.
Kwa wanaoujua, wanahofia kuwa ugonjwa huu una madhara makubwa pengine kuliko saratani na Ukimwi.
Homa hiyo au Hepatitis B inapewa uzito mdogo licha ya kuwa ni ya hatari kubwa.
Wataalamu wanaeleza kuwa Hepatitis B au homa ya
ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi, wenye madhara makubwa na wenye
uwezo wa kuambukiza kwa wepesi kuliko Ukimwi.
Kitaalamu, ugonjwa huu, husababishwa na virusi vya
Hepatitis B (HBV) ambavyo huathiri mfumo wa utoaji wa sumu mwilini.
Inaelezwa kuwa robo tatu ya watu ulimwenguni wameathiriwa kwa muda na
homa ya ini na wengine milioni 350 wameathirika moja kwa moja.
Takwimu zinaonyesha kuwa homa ya ini huua watu
600,000 kila mwaka katika sehemu mbalimbali, idadi ya watu inayolingana
na wale wanaokufa kutokana na malaria.
Maradhi haya ya ini yanaelezwa kuwa yanaweza kusababishwa na kunywa kileo kupita kiasi au sumu inapoingia mwilini.
Hata hivyo, mara nyingi ugonjwa huu husababishwa na virusi.
Wanasayansi kwa upande mwingine wamegundua virusi
vitano vinavyosababisha ugonjwa huu na wanasema kwamba huenda kuna
vingine vitatu.
Matokeo yake, sheria zimewekwa katika nchi
mbalimbali ambazo zinamtaka kila raia mgeni anayetaka kuingia katika
nchi husika, kupata chanjo ya ugonjwa huu ili kuepusha maambukizi.
Kila anayechanjwa hupewa kadi maalum itakayomwezesha kuingia katika nchi husika ili kuthibitisha kuwa amechanjwa.
Hata hivyo, ujanja mwingi umekuwa ukifanyika
katika baadhi ya nchi ikiwamo Tanzania ambapo watu hujipatia kadi za
homa ya manjano kwa kutoa rushwa na kukwepa kuchoma chanjo hiyo pindi
wanapotaka kusafiri nje ya nchi bila kujua madhara ya kutopata chanjo
hiyo.
Vilevile, chanjo hiyo iliwahi kukosekana nchini
kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na sababu ambazo haziwekwi wazi na
mamlaka zinazohusika.
Hatari kubwa ya ugonjwa huu inatajwa ni namna ya
uambukizaji wake ambapo, unaposhika damu au majimaji ya mwilini ikiwemo
mbegu za uzazi huweza kuambukizwa.
Wataalamu wanaeleza ubaya wake ni kuwa unaweza
kuambukizwa kwa kufanya ngono na hata kwa kushika majimaji ya mwili wa
mtu aliyeathirika ikiwemo damu, mate, machozi na mkojo.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani(WHO) zinaeleza
kuwa kirusi cha homa ya ini kinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu
kwa siku saba na kwa wakati huu, kirusi hiki kinaweza kusababisha
maambukizi iwapo mtu hajapata chanjo ya kuuzuia.
Watanzania wengi bila kujua wamekuwa wakiugua
maradhi mbalimbali yanayosababishwa na homa ya ini na bila kufahamu ini
limekuwa likiathirika taratibu.
Dk Yuki Mark wa Hospitali ya Parktown North,
Johanesburg, nchini Afrika Kusini anasema kuwa homa ya ini aina ya B
inaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote.
“Huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi
baada ya mtu kuambukizwa. Zinapoonekana, huenda tayari ini limenyauka au
lina saratani na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na virusi
vya HBV,” anasema Dk Mark.
Aidha, mtaalamu huyo anasema, dalili kuu
zinazojulisha kuwa mtu ana homa ya ini ni kutapika, kuchoka kupita
kiasi, kuathirika kwa ini, homa na mkojo kuwa wenye rangi ya njano
iliyokolea sana.
“Unaweza kuharisha na kutapika au kupata maumivu katika eneo fulani la tumbo lako, macho na ngozi kuwa vya njano,” anaeleza.
Homa ya ini aina ya B, inaweza kuingia mwilini mwa
mtu kwa njia ya ngono, kama ilivyo Ukimwi na magonjwa mengine ya
zinaa. Hivyo basi, majimaji katika mwili wa mwanadamu yanaweza kuwa
chanzo cha maambukizi.
“Watu wengi wanaendelea kuambukizwa kwa kutiwa damu yenye
virusi hivyo, hasa katika nchi ambako hakuna vifaa bora vya kuchunguza
virusi hivyo katika damu. Virusi vya HBV vina uwezo mkubwa zaidi wa
kuambukiza kwa kulinganishwa na virusi vya Ukimwi,” anasema Dk Mark
Anaongeza: “Hata kiasi kidogo cha damu yenye
virusi hivyo kama ile inayobaki kwenye wembe, inaweza kupitisha virusi
hivyo na tone la damu iliyokauka kwa juma moja au hata zaidi inaweza
kumwambukiza mtu virusi hivyo.”
Dk Mark anasema, madhara mengi huweza kumkumba mtu
aliyepata maambukizi ya homa ya ini, kwani anaweza kupata shinikizo la
damu, anaweza kuathirika ubongo au hata kupooza sehemu ya mwili wake.
Angalizo ambalo mtaalamu huyo anaeleza ni kuwa
baada ya mtu kuambukizwa homa hiyo, hawezi kupona, kwani dawa kuu ya
ugonjwa huu ni chanjo ya kuzuia homa ya manjano (yellow fever
vaccination).
No comments:
Post a Comment