Mimi siku zote husema si nabii wala mbashiri, sina ujuzi wa
kutembelea nyota, lakini kwa mambo yote ambayo ninayaona kwa sasa,
hakika ni alama mbaya , hatari kwa nchi yangu, Tanzania.
Hakuna shaka, pia ni hakika kwamba ni hatari pia hata kwa uhai na ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa jumla wake.
Inanikumbusha mwaka 1977 ambako EAC ya mwanzo ile
ya kina Jomo Kenyatta, Dk Milton Obote na Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere ilivunjika, ingawa safari hii suala la itikadi zinazokinzana
haliwezi tena kuwa sababu au chanzo.
Kwa waliokuwa vijana au watu wazima zama hizo
wanakumbuka jinsi EAC ya wakati ule ilivyovunjika na kuiacha kila nchi
kati ya Tanzania, Kenya na Uganda ikichukua mali, madeni ya jumuiya hiyo
na kila moja na msimamo wake, ikiendesha pia mambo yake kwa mgawanyo wa
mali ambao haukuwa wa haki. Ni wazi kwamba juhudi za marais waliofuata,
Daniel arap Moi (Kenya), Benjamin Mkapa (Tanzania) na Yoweri Museveni
(Uganda) zikawezesha kurejea na kuzaliwa kwa EAC mpya, yenye makazi yake
Arusha, mahali ambako kwa sasa zimewekezwa fedha lukuki kujenga makao
makuu mapya, ingawa kwa sasa jumuiya hiyo inayumba, inatikisika.
Yaani, EAC ya sasa ambayo pia imejumuisha nchi za
Rwanda na Burundi kama wanachama wake wapya, tayari inazo nyufa lukuki
ambazo kwa mtazamo wangu zinaashiria kuanguka au kuporomoka kwake,
huenda siku si nyingi.
Zipo kila dalili kwamba EAC yetu ya sasa ya
wanasiasa, wasaka tonge wengi ambayo imekuwa na ndoto za kuwa jumuiya
moja kubwa yenye nguvu kibiashara, kisiasa, ndoto zake hizo zimekwisha
na tayari EAC imegawanyika katika makundi.
Makundi hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana
na mitazamo ya kimasilahi zaidi ya viongozi wakuu wa nchi tatu, hasa
Rwanda, Kenya na Uganda, kwa kweli yanaiacha EAC ya sasa katika hatari
ya kufa kabla ya kutimiza malengo yake.
Ni bahati mbaya kwamba Burundi, nchi ambayo
imekuwa katika mizozo mingi ya ndani, vita ya wenyewe kwa wenyewe, haina
habari na kinachoendelea, haina upande katika mzozo huu wa sasa wa EAC.
Mzozo huu kwa macho ya mbali unaweza kuonekana
kuwa baina ya Rais Jakaya Kikwete dhidi ya Rais Paul Kagame wa Rwanda,
wengine wanaingia kama mashabiki, makuwadi.
Inawezekana kuwa mzozo si baina ya wawili hao,
Kikwete na Kagame, kwani huenda hata Kenya ya Rais Uhuru Kenyatta na
Uganda ya Museveni zinaiona Tanzania kama tishio kwa masilahi yao.
Hakuna shaka kwamba matarajio ya wengi kule Kenya kwa mfano kuifikiria
Tanzania kama eneo la kuingia kiholela, kujichotea mali, ardhi, ajira
kama wapendavyo kupitia EAC yanaonekana kukwama.
Uganda ya Museveni, nchi ambayo siku zote ua mara
nyingi imekuwa ikitegemea magendo ya kahawa, maharage, ndizi kutoka
Kagera kupitia njia za panya si vituo halali vya mpakani kama Mutukula
au Murongo.
Huenda nayo inaona kwamba biashara hii kuwa si
endelevu kama ilivyo pengine kwa kufanya biashara au ushirikiano mzuri
zaidi na Kenya kwa njia ya barabara, reli.
Ni dhahiri, Uganda na Kenya kwa sasa zinaelewana vizuri zaidi na hata kuaminiana kuliko ilivyo kwa Tanzania.
Ni vyema Watanzania muelewe kuwa Uganda ambayo
haina bandari na siku zote hutegemea bandari zenu, kwa maana ya Dar es
Salaam, Tanga na hata ile ya Mwanza kupitishia bidhaa zao, inaiona nchi
yenu kama si mshirika mzuri na mwaminifu tena mwenye kuaminika. Huenda
zipo sababu za kwa nini Waganda wamefikia mahali pa kufikiria hivyo
dhidi ya nchi yetu ambayo imejidai kisiwa cha amani, utulivu kwa muda
mrefu, hasa kama idara za umma kama TRA (Mamlaka za Mapato), bandari
(TPA) hazikuwa makini, kuangalia ni nini kinachowakwaza wafanyabiashara
au Serikali ya Uganda hadi wakachagua kuirudia Mombasa, Kenya badala ya
Tanzania. Kama tatizo ni urasimu, uzembe, umangimeza kwenye mamlaka
zetu, hakuna shaka kwamba huenda ndiyo unawafanya pia Wanyarwanda
waichague bandari ya Mombasa, mahali ambako ni mbali zaidi si Dar es
Salaam tena!
Kama kuna mtu anabisha, aangalie mifano hii
michache ya mambo yale ambayo yanaendelea ndani ya EAC kwa sasa na
ambayo yanatoa ishara wazi kwamba hali tena si shwari. Kwa siku za
karibuni, viongozi wakuu wa Kenya, Uganda na Rwanda wamekutana mara
kadhaa, wakizungumzia mambo makubwa kiuchumi, kisiasa lakini wakimwacha
nje Rais Kikwete. Kwa nini?
Kana kwamba hiyo haitoshi, pia wamefanya mkutano
wa uwekezaji kule Entebbe, Uganda, lakini mbona Tanzania ilisahaulika,
jiulize ni nini sababu?
Ninadhani Tanzania kama ina macho itazame, Rais
Kikwete na timu yake wakae chini , waangalie kama ni wema ambao nchi
yetu imetenda kwenye ukanda huu, imetunza wakimbizi, inalinda usalama
kule DRC, mahali ambako Rwanda, Uganda zinadaiwa kuwa na masilahi,
azinduke.
Viongozi wetu, yaani mawaziri wa uchukuzi, ujenzi
au hata mawasiliano, washtuke na kuona watendavyo Kenya, Uganda na
Rwanda ambao wameanza ujenzi wa reli kati ya Mombasa-Kampala-Kigali,
inayotarajiwa kumalizika mwaka 2018.
Tanzania ina nini cha kuendelea kukaa chini na
kujidai kwamba inapigania ushirikiano wa EAC, inapanga reli ya Tanga-
Musoma kwenda Uganda, mradi ambao upo kwenye makaratasi. Reli ya Isaka,
Bujumbura- Kigali imebaki simulizi, tumekwisha! Hakuna shaka kwamba huu
wa sasa ni urafiki wa shaka shaka, hakuna tena ushirikiano wa dhati
baina ya nchi hizi tatu waanzilishi wa EAC.
Hata hivyo, hili la Rais Kagame kuendelea kuchokonoana na Rais Kikwete, pia si dalili njema kwa ustawi wa EAC.
Kenya, Uganda zilizotegemea kuchuma fedha kutoka
kwa abiria wa mabasi waendao Mwanza, Kagera kupitia Nairobi na Kampala,
sasa zinalia baada ya sisi kujenga barabara nzuri za lami kutoka Dar es
Salaam kwenda Kanda ya Ziwa huenda ni wivu ni maendeleo kwa miundombinu
yetu.
No comments:
Post a Comment