TTCL

EQUITY

Thursday, June 27, 2013

KALA JEREMIAH, NEY WA MITEGO WAMTETEA OMMY DIMPOZ


 Msanii Ommy Dimpoz akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo ya KTMA 2013 kwenye Ukumbi wa Mlimani City Juni 8. Kushoto ni Wema Sepetu anayefuatiwa na Vanessa Mdee.
Kala Jeremiah akitoa shukrani baada ya kupokea moja ya tuzo zake tatu za KTMA 2013

DAR ES SALAAM, Tanzania

“Muziki wetu una siasa nyingi sana. Yaani ukikwaruzana na mtu hata kama ana ‘kiblog’ chake utakoma jinsi ambavyo atakuandika na kukuharibia jina. Pole sana Dimpoz, poleni sana mashabiki wa Dimpoz. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Bongo Flava”

WAKALI wa Hip Hop nchini, Kala Jeremiah na Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego,’ wamevunja ukimya na kuzungumzia vurugu alizofanyiwa msanii wa Bongo Flava Omari Faraji Nyembo ‘Ommy Dimpoz,’ kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akiwa jukwaani katika onesho la wateule wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro ‘KTMA 2013,’ Dimpoz alipigwa chupa za maji na kurushiwa vitu mbalimbali yeye na madansa wake, kwa kile kilichoelezwa kuwa nyota huyo kumkashifu marehemu Albert Mangwea.

Wakitumia kurasa zao za Facebook, Kala Jeremiah aliyetwaa tuzo tatu za KTMA na Ney wa Mitego aliyeshinda moja, wamewataka mashabiki kutoendelea kumpa wakati mgumu nyota huyo asiye na hatia, kwani kauli yake imegeuzwa na wenye chuki binfasi kwa maslahi yao.

Kala Jeremiah mkali aliyeibuliwa na shindano la vipaji la BSS, alitumia kurasa yake kuwashukuru mashabiki wake wa Dodoma kwa mapokezi waliyonipa siku ya onesho hilo, ikiwamo kumshangilia kutokana na kukubali kazi zake, ambapo aliwaombea baraka kwa Mungu.

Aliongeza kwa kuandika: “Naomba nitumie fursa hii kuliongelea suala la Ommy Dimpoz. Jamani mashabiki wetu tunawaomba sana muwe makini na habari mnazozipata zifanyieni uchunguzi kwanza, kwani maneno aliyoongea Dimpoz yalikuwa ya kawaida sana.

“Aliongelea suala la wasanii kufa maskini akiwa anailalamikia serikali na makampuni kuwa havitusapoti vya kutosha sisi wasanii, lakini tunapokufa thamani yetu ndio huonekana. Lakini maneno hayo yamegeuzwageuzwa na kuonekana sumu kwa huyu jamaa.

“Kama leo kafanyiwa Dimpoz, kesho atafanyiwa Jeremiah. Kwa hiyo mimi nakemea suala hili kwa nguvu zangu zote, Dimpoz hajamtusi Albert Mangwea na hawezi kufanya hivyo kwa sababu Dimpoz sio mlevi. 

Mashabiki tunawaomba sana msiingilie siasa za kimuziki.

“Muziki wetu una siasa nyingi sana. Yaani ukikwaruzana na mtu hata kama ana ‘kiblog’ chake utakoma jinsi ambavyo atakuandika na kukuharibia jina. Pole sana Dimpoz, poleni sana mashabiki wa Dimpoz. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Bongo Flava.” Mwisho wa kumnukuu Kala.

Kwa upande wake Ney wa Mitego alitumia ukurasa wake kuandika: “Nimesikitishwa sana na vitendo na shutuma zinazoelekezwa kwa msanii mwenzetu Omy Dimpoz. Nimeshindwa kuvumilia na inabidi niliongelee hili suala.

“Kama ulifuatilia alichoongea Dimpoz usiku wa tuzo za Kili, alisema makampuni makubwa yawekeze kwa wasanii kwa sababu kazi tunazofanya ni kubwa lakini matokeo yake tunakufa maskini.

“Lakini kuna watu kwa sababu zao binafsi wamepandikiza chuki kwa kumtumia Ngwea ili kumharibia Dimpoz maisha yake ya muziki. Watanzania tufungue macho, sio kila kinachoripotiwa kina ukweli. Mnaweza kumuhukumu asiyekuwa na hatia, kisa kuna watu wametumia mamlaka na ‘power’ zao kumangamiza.


“Ina maana ndugu zangu mnapenda wasanii wenu tuendelee kubaki na kufa maskini wakati kazi tunayofanya ni nzito? Ni hayo tu,” alimaliza Ney wa Mitego kuhamasisha mashabiki kutafakari kabla ya kuchukua hatua za kuwahukumu watu bila kujali usahihi wa madai dhidi yao.

No comments:

Post a Comment