Ni siku ya kimataifa ya kukabiliana na dawa za kulevya
Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na dawa za kulevya na biashara
haramu ya dawa hizo. Umoja wa Mataifa umeitenga siku hii kuuhimiza
ulimwengu kupambana na janga hili ambalo linaathiri hasa vijana kote
duniani.
Afisi ya Umoja wa Mataifa inayokabiliana na dawa za kulevya na uhalifu,
UNODC, imesema hapo jana mjini Vienna, Austria, kuwa kuna aina mpya ya
dawa za kulevya ambazo zinaepuka marufuku zinazotambulika na
zinatengezwa kwa kiwango cha juu mno kiasi ya kukipiku kiwango cha dawa
za kulevya zilizoharamishwa.Ripoti inayotolewa kila mwaka na shirika hilo la UNODC imesema athari za dawa hizo mpya zinafanana na zile kama za amphetamine, bhangi na miraa lakini zinaweza kuwa hatari zaidi kwani hakuna taarifa za kutosha kuhusu madhara na uraibu wake.
Mraibu wa dawa za kulevya akijidunga sindano
Nchi kadhaa zimeripoti kwa shirika hilo aina 251 za dawa mpya kufikia katikati ya mwaka jana ambayo ni zaidi ya zile zilizopigwa marufuku chini ya mikataba ya kimataifa ambazo idadi yake ni 234.
Kuibuka kwa dawa mpya kwazua wasiwasi
Ripoti hiyo inasema kuwa imekuwa vigumu kwa serikali kote duniani kuzipiga marufuku hizi dawa mpya kwa sababu utaratibu unaotumika kuzitengeza si kama ule wa dawa zinazojulikana. Nyingi ya dawa hizi zinatengezwa barani Asia na Ulaya.
Katika nchi za Umoja wa Ulaya, mmoja kati ya vijana 20 ameshazijaribu dawa hizi mpya za kulevya ambazo mara nyingi huuzwa kama dawa za mitishamba au chumvi za kuogea.
Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii ya kukabiliana na dawa za kulevya, Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban ki Moon, amesema dawa za kulevya kote duniani zinatishia afya na maslahi ya vijana, watoto familia na jamii kwa ujumla na mabilioni ya fedha zinazotokana na biashara hii haramu zinakuza ufisadi, na kuyapa mitandao ya wahalifu nguvu zaidi na hivyo kuzua hofu na misukosuko.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon
Ni jukumu la kila mmoja kupambana na dawa
Bado kiwango cha matumizi ya dawa kama vile Heroin, cocaine na amphetamine hakijashuka lakini mtindo huu wa kuwepo kwa aina mpya za dawa za kulevya unatia wasiwasi.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu walioambukizwa virusi vya HIV kupitia kujidunga sindano miongoni mwa waraibu wa dawa za kulevya ilikuwa milioni 1.6 mwaka 2011.
Shirika hilo la kukabiliana na dawa za kulevya la Umoja wa Mataifa UNODC limeanzisha kampeini kote duniani ya kufikisha ujumbe kuwa dawa za kulevya ni tisho kwa jamii na kuwa ni jukumu la kila mmoja kuwalinda vijana dhidi ya dawa hizi hatari huku kauli mbiu ya kampeini hiyo ikiwa acha afya yako iwe kichoche cha maisha yako na si dawa.
No comments:
Post a Comment