HANS POPPE AJIUZULU NYADHIFA ZOTE SIMBA SC
Zacharia Hans Poppe; Amejiuzulu Simba SC |
amejiuzulu wadhifa wa Ujumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Simba SC ya dar es Salaam pamoja na Uenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya klabu hiyo leo.
Kwa mujibu wa habarikutoka ndani ya Simba mida
hii, Hans Poppe amewasilisha barua ya kujiuzulu leo akielezea kusitikishwa kwake
na hali halisi ndani ya klabu.
Alipoulizwa mwenyewe kuhusu hilo, alisema; “Sipo
katika nafasi ya kulizungumzia hilo kwa sasa, wasiliana na Katibu (Evodius
Mtawala) au Mwenyekiti (Alhaj Ismail Aden Rage),” alisema Hans Poppe, ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Friends of Simba na kukata simu.
Mtawala na Rage hawakupatikana kwenye simu zao
mida hii, ingawa BIN ZUBEIRY inaendelea na juhudi za kuwatafuta.
Kwa mujibu wa barua hiyo, pamoja na kujiuzulu,
Hans Poppe ameahidi kuendelea kuwa mwanachama mwaminifu ndani ya Simba SC.
Wazi kujiuzulu kwa Kapteni huyo wa zamani wa
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ni pigo kwa klabu hiyo, kwani alikuwa
akiisaidia mno kwa hali na mali.
Aidha, kujiuzulu kwa Hans Poppe wazi kutachochea
zaidi mgogoro ndani ya klabu hiyo na kuongeza shinikizo la viongozi wa klabu
hiyo kujiuzulu pia.
Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa
Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola
katika raundi ya kwanza tu.
Ubingwa wa
Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi
wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na
Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 36 na Yanga inayoongoza
kwa pointi zake 42, zote za Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment