TTCL

EQUITY

Sunday, May 1, 2016

Wadau wapendekeza wasichana waolewe wakifika miaka 18 na kuendelea

Wadau nchini wamependekeza marekebisho ya sheria ya ndoa ilikumsaidia mtoto wa kike kuondokana na ndoa za utotoni ambapo wametaka umri wa kuanzia miaka 18 ndiyo sahihi na sio kama ilivyo sasa katika sheria ya ndoa ambayo imeonekana kupitwa na wakati kwa dhama za sasa.
Hayo yalisemwa  hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mwanasheria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Januari Kitunsi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kusitisha ndoa za utotoni nchini.
Kampeni hiyo inasimamiwa na Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya watoto ya Save the Children.
Lengo la kurekebisha sheria hiyo ni kupambana na tatizo la ndoa za utotoni ambazo ni changamoto ya muda mrefu, ambayo imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara, Kitunsi alisema.
“Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kifungu namba 13, kinaruhusu ndoa kwa mtoto wa kike kuanzia miaka 15, lakini sasa serikali inataka umri wa kuolewa uanze miaka 18,” alisema.
Aidha, Kitunsi alisema mapendekezo hayo yametolewa kutoka katika maoni yaliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Sheria mwaka 1994 ambayo ilitaka ili mtoto wa kike aolewe lazima awe amefikisha miaka 21.

 ndoa miaka 18
Wakati huo huo, Mwanasheria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Kitunsi alisema wizara hiyo pia imependekeza kuondolewa kwa kipengele cha kutaka mtoto aolewe kwa ridhaa ya wazazi. Badala yake, serikali imetaka muhusika aridhie ndoa hiyo.
“Hayo mapendekezo yote tumeyawasilisha Wizara ya Katiba na Sheria ambapo ndiyo ina uwezo wa kupitisha marekebisho hayo kabla ya kuanza kutumika,” alisema Kitunsi.
Aidha, Mwanasheria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee huyo alisema wizara hiyo inaendelea kufanya juhudi za kupunguza ndoa za utotoni lengo likiwa ni kuhakikisha linamalizika.
Naye Meneja wa mradi huo, Jasminka Milovanic alisema kampeni hiyo itashirikisha mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayopigania haki za watoto, lengo likiwa kupunguza ndoa za utotoni ambazo zinasababisha vifo kwa asilimia 20.
Alisema kampeni hiyo itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini ambayo ina ofisi za Save the Children, inataka kuhakikisha ndoa za utotoni zinakuwa historia katika kipindi cha miaka mitatu.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Baraza la Watoto mkoani Arusha, Raphael Denis alisema ndoa nyingi zinasababishwa na wasichana kuacha shule kutokana baadhi ya walimu kutoa adhabu kali pindi mtoto anapokosa.
Naye Balozi wa kupinga ndoa za utoto Tanzania, Valeria Msoka, alisema anaungana na wadau hao katika vita ya kupambana na ndoa za utotoni kwani itasaidia kumaliza tatizo hilo, ambalo limekuwa changamoto nchini.

No comments:

Post a Comment