
Profesa
Idris Rai, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na
Dkt Said Bourhani, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Komoro wakisaini
Mkataba wa makubaliano ya mashirikiano baina ya vyuo vyao.
Chuo Kikuu
cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimetiliana saini mkataba wa makubaliano
juu ya mashirikiano na Chuo Kikuu cha Komoro mjini Moroni katika hafla
maalum iliyofanyika tarehe 19 Januari, 2016 na kuhudhuriwa na uongozi
wote wa Chuo Kikuu cha Komoro, Balozi wa Komoro nchini Tanzania Dkt.
Ahmada El Badaoui Mohamed na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini
Komoro, Bw Mudrik Ramadhan Soragha.
Makubaliano
kati ya vyuo hivi ni moja ya matokeo ya ziara ya nchini Komoro ya
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi aliyoifanya hivi karibuni.
Katika
hotuba yake kwenye hafla hiyo, Profesa Idris Rai, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar aliwaeleza wahudhuriaji kwamba ametembea
nchi nyingi duniani lakini Komoro ni nchi ya kwanza ambayo amekuwa
akijisikia kama kwamba yuko nyumbani tokea alipoingia nchini humo.
Alisema kwamba kuna uwiano mkubwa sana baina ya watu wa Zanzibar na watu
wa visiwa vya Komoro katika kila nyanja za maisha.
Makamu Mkuu
huyo wa SUZA aliwaeleza wana Chuo hao kwamba makubaliano baina ya vyuo
hivyo viwili ni tofauti kabisa na mashirikiano ambayo SUZA imekuwa
ikiweka saini na vyuo vingine mbali mbali kwani hayo yanahusisha vyuo
vya nchi ndugu ambazo zinashabihiana kihistoria, kimazingira, kidini na
kiutamaduni. Aliwahakikishia wanachuo waliohudhuria hafla hiyo kwamba
SUZA kwa upande wake itahakikisha mashirikiano ya makubaliano
yaliyofikiwa yanapewa kipaumbele na yanatekelezwa kama yatakavyopangwa.
Mkataba huo wa mashirikiano umeainisha mambo ya mashirikiano kama ifuatavyo:
-kusaidiana
kuendesha mafunzo ya lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa upande wa
Komoro na lugha ya Kifaransa katika ngazi ya Shahada kwa upande wa SUZA.
-Kufanya
tafiti za pamoja kwenye maeneo ya sayansi jamii na historia, tamaduni,
lugha, dini kwa upande mmoja na masuala ya mazingira, rasilimali asilia
na bahari kwa upande mwingine.
-Kubadilishana walimu na wanafunzi baina ya SUZA na Chuo Kikuu cha Komoro.
-Kusaidiana kujenga uwezo wa wanataaluma wa vyuo viwili hivi kwa maeneo ambayo Chuo kimoja kina uwezo zaidi.
-Kuandaa mapendekezo ya kuazisha taasisi ya pamoja inayohusu masomo ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Komoro.
Ilibainika
kwamba moja ya kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa mashirikiano haya
kitakuwa ni lugha ambapo lugha kuu ya taaluma inayotumika katika Chuo
Kikuu cha Komoro ni Kifaransa wakati lugha inayotumika SUZA ni
Kiingereza na Kiswahili. Mafunzo ya lugha katika makubaliano haya
yataweza kuondosha kikwazo hicho hivyo kuwawezesha wanafunzi na
wafanyakazi wa vyuo hivi kutembeleana kwa masomo na kushirikiana katika
kufanya tafiti za pamoja.
Kwa upande
wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Komoro, Dkt Said Bourhani aliwaambia
wanachuo wa Chuo Kikuu cha Komoro kwamba utekelezaji wa mashirikiano
haya ni tofauti na mashirikiano na vyuo vingi kwani safari ya Tanzania,
Zanzibar kutoka Moroni ni fupi na rahisi. Pia aliwashukuru marais wa
Zanzibar na Komoro kwa kufikiria na kutaka Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Komoro kuanzisha mashirikiano haya.
Chuo Kikuu
cha Komoro na SUZA ni vyuo vichanga lakini vimekuwa kwa kasi kubwa
katika miaka ya karibuni. Wakati Chuo Kikuu cha Komoro kilianzishwa
mwaka 2003 na kikiwa ni Chuo Kikuu pekee nchini Komoro kikiwa na
wanafunzi karibu 9,500 katika masomo ya fani mbali mbali, Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar kilianzishwa mwaka 2001 na sasa kina wanafunzi
karibu 4,000 waliojiunga na masomo kwenye karibu fani 40 katika ngazi za
cheti hadi shahada ya uzamivu.
Mara tu
baada ya ziara yake nchini Komoro, imekuwa ni hamu kubwa ya Dkt. Ali
Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kuona Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kinashirikiana kwa karibu sana
na Chuo Kikuu cha Komoro.
No comments:
Post a Comment