TTCL

EQUITY

Monday, January 25, 2016

Manji: Tiboroha alificha barua za Niyonzima

manji 
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.
 
*Atangaza kugombea tena, asema wanaomtaka wampe kura awe mwenyekiti
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, amesema yeye na kamati ya utendaji walifanya uchunguzi na kugundua kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha alikuwa akificha mawasiliano yake na kiungo Haruna Niyonzima ili afukuzwe klabuni.

TIBOROHA
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha.

Manji amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana, kwamba Dk Tiboroha alifanya mambo mengi likiwemo hilo la kuhakikisha Niyonzima anatimuliwa na kusisitiza alikuwa anafanya mambo mengi kwa ajili ya maisha yake binafsi na si kwa faida ya Yanga huku akitaja kuwepo kwa hali ya kutoelewana kati yake na msemaji, Jerry Muro.
 
“Niliamua uchunguzi wa ndani ufanyike katika suala hilo zima na mwisho, Jonas Tiboroha alibainika kuwa hakuwasilisha ushahidi wa mawasiliano sahihi kwa Kamati ya Nidhamu kuhusiana na Haruna Niyonzima, hali iliyosababisha kamati kuchukua uamuzi ambao haukuwa sahihi kwa sababu yake,” alisema Manji.
“Mfano barua za Niyonzima kutoka kwa Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) ambazo zilitumwa kwa TFF na kupokelewa kama ambavyo Azam FC walipokea ya mchezaji wao kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wao. Lakini barua ya Niyonzima kuja Yanga, ilionekana haikupokelewa kama ilivyokuwa kwa barua yake ya utetezi na ile ya kuomba radhi alizoandika, nazo zilipokelewa lakini hazikuwasilishwa kwenye kamati ya nidhamu na hili, mhusika ni Tiboroha,” alisema Manji na kuongeza:
 
“Kamati ya Utendaji (EXCOM), baada ya kupitia kwa kina iliona uamuzi iliochukua haukuwa wa haki kutokana na kupotoshwa na Tiboroha, tena aliendelea kuipotosha kamati kwa makusudi kutokana na kuficha nyaraka hizo ili Niyonzima afukuzwe kwa kuonekana hakuomba radhi. Tulifikia maamuzi Tiboroha alikuwa na ajenda yake binafsi.”
Aidha, Manji alimtuhumu Tiboroha kuwa na tabia ya kuvujisha siri za Yanga na kusema hakufikia kabisa malengo ambayo aliwekewa na kamati ya utendaji ikiwa ni sehemu ya maendeleo ya Yanga huku akisema alishangazwa kuona anatetewa na mwenyekiti wa Matawi wa Yanga, Said Msumi aliyesema cheo chake hakipo katika katiba ya Yanga.
“Tiboroha alikuwa mwajiriwa, alikuwa akilipwa mshahara. Angalia mimi na wajumbe wa kamati ya utendaji, hata posho tu hatupati,” alisema Manji na kuongeza:
“Karibu kila kizuri cha Tiboroha alichofanya yalikuwa ni maelekezo au maagizo yangu au kamati ya utendaji, lakini ilionekana yeye ndiye amefanya hilo na wengi wakamsifia.”
 
Aidha, Manji alizungumzia suala la kushuka kwa mapato na kupanda kwa matumizi ndani ya miezi 12.
“Matumizi ya Yanga yalikuwa Sh milioni 500 kwa mwaka, sasa yamepanda mara nne zaidi na kufikia takriban Sh bilioni 2 katika kipindi chake akiwa katibu mkuu. Kabla hajaja klabuni, tulikuwa tumekaribia kujikomboa na kuanza kujitegemea,” alisema Manji.
“Pia kuna wakati Fifa iliialika Yanga kwenye semina ya mafunzo nchini Ghana, Tiboroha akajichagua na kwenda yeye, ukifuata weledi hili si jambo sahihi. Achana na hilo, hivi karibuni Yanga tuliajiri daktari mpya kwa mapendekezo yake, siku chache baadaye ikagundulika kupitia kamati ya mashindano kuwa yule ni daktari mwenye kadi ya Simba, tukamfukuza.”

Zaidi ya hapo, Manji alimshutumu Tiboroha kushindwa kuonyesha weledi kwa kumtaarifu mshambuliaji Donald Ngoma anatakiwa kufanya majaribio Uturuki bila kuwasiliana na kamati ya utendaji, tena ikiwa ni siku chache kabla ya kwenda kwenye michuano ya Mapinduzi.
“Mwalimu alilalamika kwamba hilo lilichangia Ngoma kutocheza vizuri kwenye michuano ya Mapinduzi kule Zanzibar.
“Hadi leo tunawadai BDF ya Botswana dola 5,000. Hatujui ziko wapi, hakuna taarifa na mambo yamekuwa yakifichwa tu. Huyu Tiboroha amekuwa akifanya mambo mengi ya kukiuka utaratibu pia kwenda nje ya weledi. Mfano kuajiri katibu muhtasi na mtu mwingine hata bila kuieleza kamati ya utendaji. Hii inaonyesha alikuwa akifanya anavyotaka tu na kutaka kujijengea sifa ya “umungu mtu”.
 
“Niwe mkweli, Tiboroha hakuwa Yanga kwa maslahi ya klabu, alikuwa akiitetea TFF dhidi ya Yanga, alikubali mambo kibao na mengine yamechangia kushusha mapato ya Yanga. Aliamua waziwazi kumkandamiza msemaji wa klabu, Jerry Muro wakati wa kesi yake na TFF, alifanya hivyo akihofia namna Jerry alivyokuwa anakubalika kwa kasi na wanachama,” alisema Manji.
“Alipoona mengi yamegundulika. Januari 14, mwaka huu aliandika barua kuomba radhi kwangu, akikiri kufanya makosa na kusema alikuwa akiyajutia. Mimi na kamati ya utendaji hatukukubaliana na msamaha kwa hofu ya matendo yake, tulimshauri aandike barua ya kujiuzulu ili aachane na Yanga kwa amani. Kweli akafanya hivyo Januari 22 lakini ajabu, amekuwa akianzisha chokochoko zinazopelekea kuwepo na misigano ya wanachama,” alisisitiza Manji.
 
Pamoja na hilo la Tiboroha, Manji alizungumzia uchaguzi na kusema: “Kumekuwa na maneno ya chinichini kwamba mimi ninaogopa uchaguzi, mimi sijawahi kushindwa uchaguzi na ndiyo nimekuwa nikiagiza kamati ya uchaguzi ihakikishe inaitisha. Nilimweleza mwenyekiti wake afanye hivyo haraka au ajiuzulu, bahati mbaya anauguliwa na baba yake mzazi, ameamua kujiuzulu.
“Tayari nimeomba majina kwenye kamati ya utendaji ili mchakato uendelee na huu ni wakati mzuri kwa wanaompenda Tiboroha kumpa kura naye awe mwenyekiti, lakini nami wanipe uhuru wangu wa kuendelea na mambo yangu mengine, ambayo yapo karibu na moyo wangu kama vile kusaidia maendeleo ya Mbagala Kuu.
 
“Hata hivyo, kimsingi nimeamua kugombea tena, tuache demokrasia itawale, ingawa sidhani kama nitamaliza kipindi chote cha uongozi iwapo nitashinda kwa kuwa kutoka awali niliieleza Yanga kuwa mafanikio ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini hilo halitawezekana bila ya klabu kumiliki uwanja wake binafsi pale Jangwani,” alisema Manji.

No comments:

Post a Comment