Wafuasi wa Chadema wakipinga Madiwani kutoka Zanzibar kupiga kura katika uchaguzi wa Meya wa Kinondoni
BAADA ya uchaguzi wa Mameya wa Halmashauri mbili za Ilala na
Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuahirishwa katika mazingira yaliyojaa
utata, sasa madiwani wa Ilala na Kinondoni wametangaziwa uchaguzi
kufanyika kesho Januari 16.
Awali, uchaguzi huo ulitakiwa kufanyika Januari 9
mwaka huu, lakini ulizuiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatia
kesi iliyotajwa kufunguliwa na kada wa CCM aitwae Elias Nawela akiomba
mahakama itoe zuio la uchaguzi.
Shauri la Nawela lilisikilizwa juzi na Hakimu Mkazi Mwandamizi,
Respicius Mwijage akaondoa zuio ikiwa na maana kuruhusu uchaguzi huo
kufanyika.
Hakimu Mwijage alisema mlalamikaji aliishangaza mahakama kwa
kushindwa kuwasilisha hati ya madai ili kukidhi matakwa ya kisheria na
kujenga uhalali wa uharaka wa kesi hiyo kama alivyoomba.
“Mlalamikaji alikuwa anajua uhalali wa kesi yake na hajaonyesha
sababu yoyote ya msingi iliyomfanya kushindwa kuwasilisha hati ya madai
kwa upande wa mlalamikiwa hadi leo hii (Jumatano) kesi ilipokuja hapa
kwa ajili ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Mwijage.
Hatua hiyo imekuja wakati upande wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA), walikimbilia mahakamani nao kuomba kuunganishwa
katika kesi aliyoifungua Nawela.
Uchaguzi uliahirishwa siku ambayo maandalizi yalikuwa tayari
kuwezesha uchaguzi kufanyika. Ghafla Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala
na pia wa Kinondoni walisoma zuio la mahakama kutaka uchaguzi
usifanyike.
Uamuzi huo ulizusha mtafaruku kwa kuwa ilionekana ni mbinu ya CCM
kutaka kujipanga upya baada ya kuona mpango wake wa kuongeza mamluki wa
kupiga kura kama madiwani, kushindikana.
CCM iliingiza mamluki siku ya kwanza ya uchaguzi, wakazuiwa na
uchaguzi ukashindikana. Januari 9 ikawa siku nyingine uchaguzi ndio
ukaingia kikwazo kwa kuwa hata UKAWA nao waliingiza mamluki.
“Hakuna kesi ya maana mahakamani. Hizi ni mbinu tu za CCM kutaka
kuvuruga ili washinde umeya. Leo wameona tumewazidi idadi ya madiwani
kwa kuwa nasisi tumeleta madiwani wa viti maalum kutoka Pemba. Tupo
mbele kuliko wao,” alisema mmoja wa madiwani wa Ukawa jijini Dar es
Salaam.
Kuahirishwa kwa uchaguzi kwa sababu ya zuio la mahakama, kulimsukuma
Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene kumuagiza
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki kuhakikisha uchaguzi uwe
umefanyika ifikapo Januari 16, mwaka huu.
Jana baada ya kufahamika kwamba mahakama imeondoa zuio la uchaguzi,
viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walisema
watashiriki uchaguzi na wamejipanga kushinda kwa kuwa wana madiwani wa
kutosha kuliko CCM.
Walisema uchaguzi utawezekana iwapo Mkurugenzi wa Halmashauri
atafuata sheria ikiwemo agizo la Waziri Simbachawene kwamba kisheria,
madiwani wanaopaswa kushiriki uchaguzi huo ni wale ambao wakati wa
uchaguzi mkuu, vyama vyao viliwapitisha kugombea maeneo wanayoshiriki
kuchagua mameya.
No comments:
Post a Comment