TTCL

EQUITY

Saturday, January 30, 2016

Arusha kupata bil. 28/- za ujenzi soko jipya

 
HALMASHAURI ya Jiji la Arusha inakamilisha mchakato wa kupata Sh bilioni 28 za mkopo kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa ajili ujenzi wa soko jipya la Kilombero.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa jiji hili, Juma Idd wakati alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, miundombinu ya soko hilo kwa sasa imechakaa na imefikia mwisho wa uhai wake.
Idd alisema, soko hilo halifai kukarabatiwa hivyo hatua iliyopo ni kubomolewa na kujengwa soko jipya litakalokuwa na miundombinu bora kuliko ilivyo sasa.
Alisema wanamalizia uboreshaji wa miundombinu ya Soko la Shuma lililopo kata ya Elerai ambalo kuanzia sasa litakuwa likitumika kushushia bidhaa zote zikiwemo matunda, samaki na vitunguu, na wafanyabiashara watakuwa wakitumia magari madogo kubeba bidhaa zao hadi soko la Kilombero.
Mkurugenzi huyo alisema, magari yote ya mizigo ya biashara hayaruhusiwi kushusha wala kupakia mizigo ndani ya soko la Kilombero na hayo ni maandalizi ya kulibomoa soko hilo ili lijengwe upya.
Akijibu swali la kuondoa harufu ya maji taka na uchafu inayotoka kwenye chemba za kusafirishia maji taka na kusambaa maeneo mbalimbali ya jiji, alisisitiza kuwa hilo ni jukumu la Mamlaka ya Maji Safi na Taka Arusha (AUWSA).
Alisema AUWSA inapochelewa kushughulikia uondoaji wa maji taka Halmashauri ya Jiji imekuwa ikiwatoza faini ambayo ni adhabu kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao.
Aliongeza kuwa, AUWSA imekamilisha mchakato wa kupata mkopo wa fedha Sh bilioni 200 kwa ajili ya kukarabati miundombinu yake ikiwemo usafirishaji wa maji taka, kuhamisha mabwawa ya maji taka kutoka eneo la Lemara kuyapeleka Terat kwenye eneo lililotengwa.

No comments:

Post a Comment