UTAMADUNI uliotukuka na kujengwa kwa miaka mingi na Watanzania wa
kuishi kwa amani, utulivu, upendo na mshikamano bila kujali tofauti za
kidini, kikabila, rangi na itikadi, umedhihirika tena jana kwa
Watanzania kushuhudia Dk John Magufuli akiapishwa katika Uwanja wa
Uhuru, jijini Dar es Salaam kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.Hongera na karibu sana Rais Dk Magufuli.
Hakuna ubishi kwamba ulipitia safari ndefu yenye milima na mabonde
hadi kufikia hatua hii ya kuwa mfanyakazi nambari moja wa Serikali ya
Awamu ya Tano.
Mliowania nafasi hiyo kupitia chama chako, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
mlikuwa 38 lakini hatimaye wewe ndiye uliyeibuka kuwa mshindi wa
kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo
na wagombea wengine saba kutoka vyama vya upinzani.
Mkaingia kwenye mchakato wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa
kuteuliwa rasmi kuwania nafasi hiyo, mkaanza kampeni zilizokuwa na
ushindani wa hali ya juu kuliko chaguzi nyingine nne za vyama vingi
zilizopita.
Kura zikapigwa na hatimaye ukaibuka mshindi, ukakabidhiwa cheti cha
ushindi na kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka
mitano ijayo.
Mambo hayo yote yalifanyika kwa uwazi, umakini na kwa amani na
usalama wa hali ya juu kiasi cha sisi kama Watanzania kusikia wenzetu wa
nchi mbalimbali waliotuma waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kupitia
taasisi na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania,
wakitumwagia sifa lukuki.
Tumedhihirisha kwa vitendo kwa mara nyingine tena bila kufanya ajizi
kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani kwa kubadilishana madaraka ya juu
kabisa ya kitaifa kwa amani huku viongozi kutoka nchi mbalimbali za
Afrika na nje ya bara hili wakishuhudia kwa nderemo na vifijo uwanjani.
Ni utamaduni ambao nchi za wenzetu wanashindwa kuufikia na siyo
kwamba hawataki lakini wamekosa namna ya kuujenga na kuuendeleza
utamaduni huu mzuri kwa kila taifa lenye kutaka ustawi na haki kwa watu
wake wote bila kubaguana.
Kama ulivyozungumza baada ya kuapishwa kwako Rais Magufuli kwamba
uchaguzi umekwisha na Watanzania wote kwa ujumla wake wakiwemo
washindani wako, na siyo wapinzani wako katika kinyang’anyiro cha urais
kwamba sasa turejee katika hali kulijenga taifa letu baada ya
kuhitimisha uchaguzi salama. Hiki ndicho kikubwa tunachotarajia.
Kwa rais wetu mstaafu aliyekuachia kijiti cha uongozi, Dk Jakaya
Kikwete, Mungu akuzidishie kila la heri katika maisha yako ya kustaafu
baada ya kulitumikia taifa hili, kwa umakini wa hali ya juu hadi kufikia
kukabidhi jahazi hilo kwa amani na usalama kwa mujibu wa sheria na
taratibu zetu tulizojiwekea wenyewe.
Tunajisikia fahari kuona kwamba unaungana na marais wenzako wastaafu
wawili, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuwa raia waandamizi wa nchi
yetu mliosimamia kwa umakini misingi ya kubadilishana uongozi wa ngazi
ya juu wa taifa letu bila mifarakano kwa kufuata sheria na Katiba ya
nchi yetu. Mungu Ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment