TTCL

EQUITY

Monday, December 1, 2014

Naibu IGP aonya matumizi ya nguvu uchaguzi wa mitaa

Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna, Abdurahman Kaniki

Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna, Abdurahman Kaniki (pichani), ameonya matumizi ya nguvu kutumika wakati wa uchaguzi wa serikali za Mitaa Desemba 14 mwaka huu,.

Wakati Kaniki alitoa angalizo hilo juzi ikiwa siku ya mwisho ya kuandikisha wapiga kura  kwa ajili ya kupiga kura ya kuwachagua viongozi wa mitaa.

Alitoa mwongozo huo mjini hapa wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo wa jeshi hilo kwa vyeo vya Staff Sergeant na Koplo, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA).

“Katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa tusitumie nguvu kupita kiasi, ingawa ni ukweli usiopingika kwamba kwa mujibu wa sheria za nchi, tunaruhusiwa kutimia nguvu. Lazima tuheshimu na kuzingatia haki za binadamu kabla ya kufanya hivyo,” alisisitiza.

Aidha, alisema Polisi hawapaswi kushiriki au kujihusisha kwa namna yeyote ile kwenye masuala ya siasa licha ya kuruhusiwa kupiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Kwa mujibu wa sheria, askari wa ngazi zote na katika mchakato wa kisiasa, majukumu yetu ni mawili yaani kutoa huduma ya ulinzi na usalama pamoja na kupiga kura. Kuna chaguzi mbalimbali ambazo ziko mbele yetu ambazo ni kura ya maoni, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ule wa serikali za mitaa utakaofanyika Desemba 14 mwaka huu… Kamwe Polisi msiingie katika masuala ya kisiasa kwa sababu nikiwafahamu sitawaacha,” alionya Kamishna Kaniki.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limebariki askari wake wenye nia ya kujiendeleza kitaaluma kufanya uamuzi mapema kwa kuwa hata wahalifu nao wamegundua njia pekee ya kufanikisha mambo yao ni kupata maarifa mapya darasani.

“Uhalifu ambao unatokea sasa hivi ni ule wa kisasa zaidi. Wahalifu wanakaa kitako kutizama watakavyowakabili polisi. Wanatumia makosa yetu ya kutopenda kujiendeleza kufanya uhalifu wa kimtandao.
Jamani uhalifu wa zamani umepigwa teke na kama wahalifu wanatembea sisi tunatakiwa tukimbie,” alisema.