TTCL

EQUITY

Wednesday, December 24, 2014

BAADA YA KUMALIZA KIDATO CHA NNE SASA ATEMBEA KWA MAKALIO

Na Makongoro Oging’


Nyinyiga Raphael (27) ni kijana, mkazi wa Yombo Machimbo wilaya ya Temeke ambaye ndoto zake za kuendelea na masomo zilikatika baada ya kupatwa na maradhi ambayo yanamtesa kwa kipindi cha miaka saba sasa bila kutembea kwa miguu kama ilivyokuwa awali.

Nyinyiga Raphael akitembea kwa kutumia makalio.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake huko Yombo, mama mzazi wa kijana huyo alikuwa na haya ya kusema:“Mwanangu kwa sasa hali yake siyo nzuri kwani amekuwa mtu wa kuumwa magonjwa mengi kupita kiasi licha ya kupooza miguu na mikono na kumfanya asitembee kama zamani, anaishi na kutembea kwa kutumia makalio yaani kujiburuza.

LINI ALIANZA KUUMWA?
“Nilimzaa Nyinyiga bila kuwa na tatizo lolote, alikuwa na afya njema na alikuwa akifanya vizuri shuleni katika masomo yake, tatizo lilimuanza mara alipomaliza kidato cha nne mwaka 2008, ilimuanza kama homa, tulipompeleka Hospitali ya Temeke walidai kuwa ana ‘taifodi’, alipewa dawa lakini hakukuwa na mafanikio, masikio yakawa hayasikii.

ALICHAGULIWA KIDATO CHA TANO
“Wakati yanatoka matokeo ya kidato cha nne alichaguliwa kuendelea na masomo kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Musoma lakini alishindwa kwenda kwa vile alikuwa akiumwa sana.

Nyinyiga Raphael akiwa na mama yake.

BABA YAKE AFARIKI DUNIA
“Wakati huo baba yake naye alikuwa ameanza kuugua na ilipofika Desemba 16, mwaka 2011 akafariki dunia.“Alifanyiwa vipimo kwa mara ya pili na iligundulika ana tatizo katika uti wa mgongo, alipatiwa tiba lakini haikusaidia, tulimhamishia Hospitali ya Matembele, alipimwa na ikabainika kuwa mishipa haina nguvu ya kusukuma damu hadi miguuni, tuliambiwa tulipe shilingi laki moja na nusu ya matibabu na akimaliza dozi atapona, fedha hizo sikuwa nazo, nilimrudisha nyumbani na kwa sasa namchuwa kwa mafuta ya karafuu lakini hakuna mabadiliko.

MUHIMBILI KWA DALADALA
“Sina kazi huku fedha za kununua dawa zinahitajika hata ya chakula ni shida, wakati mwingine tunalala bila kula, hali ya mwanangu ilibadilika nilimchukua na kumweka katika daladala hadi Hospitali ya Muhimbili ambapo walisema kuwa anasumbuliwa na malaria, alipewa dawa lakini hakupata nafuu, tukawa tunampa panado.

ANACHOUMWA SASA
“Mwanangu anapata maumivu hasa katika kifua, tumbo, alielezwa kuwa ana vidonda vya tumbo, ninawaomba Watanzania wanisaidie fedha ya matibabu, chakula. Mimi mwenyewe naumwa sana hapa nilipo, nashindwa kutembea, nimekuwa nikitembea hapa nyumba za jirani kuomba chakula, wakati fulani nakosa tunabaki tukitazamana na mwanangu.

...Akiwa amejipumzisha.

NATAMANI BIASHARA 
“Kwa sasa hatuna maisha mazuri, nikimpata mtu akinisaidia mtaji wa biashara nitashukuru, natamani kufanya kazi hiyo kwani naamini itatusaidia lakini pia nawaombeni nauli shilingi laki nne ya kwenda kwetu Musoma.

“Ninapata shida sana kwa vile sina ndugu hapa Dar, mume wangu alifariki akifuatilia mafao yake Tazara, nami nimefuatilia lakini sijapata, sina nguvu ya kuzifuatilia tena kwani ni kazi sana na nimekuwa nikipigwa kalenda hadi nimechoka.”Mama huyu anaishi maisha ya dhiki na mateso makali kwa yeyote mwenye nia na huruma ya kumsaidia awasiliane naye kwa namba 0767-682 385 au 0653-784 088.

No comments:

Post a Comment