Simon Manase akiuguza majeraha katika Hospitalini ya Berega mkoani Morogoro.
Simon Manase (22) ambaye ni dereva wa bodaboda, mkazi wa Kijiji cha Nguyami, wilayani Gairo mkoani hapa amecharangwa mapanga mwilini na kukatwa mkono wa kulia na mtu aliyetajwa kwa jina la Frank akidai kumfumania na mkewe vichakani.
Ishu hiyo inadaiwa kujiri usiku mnene wa Oktoba 31, mwaka huu kwenye Kijiji cha Nembo mpakani mwa Gairo na Kilosa katika muziki wa mitaani maarufu kwa jina la ‘kigodoro’.Mwandishi wetu alipiga gia hadi kwenye eneo la tukio na kufanikiwa kuzungumza na mashuhuda, viongozi wa kata, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Berega na Mkuu wa Kituo cha Polisi Dumila.
“Siku ya tukio tulikuwa kwenye shereha ya mwenzetu, mwanae amevunja ungo hivyo nyumbani kwake aliweka muziki wa kigodoro, cha ajabu ilipofika saa sita usiku DJ wa muziki, Alex Munga alitutangazia kwamba kuna watu wanapigana mapanga baada ya kufumaniana kwenye kichaka.
“Tulikimbilia kule. Kufika tukamkuta Frank akimcharanga mapanga Simon akidai amemfumania na mkewe ,”alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth Joseph.Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nembo, Musa Bruno alikiri kutokea kwa tukio hilo kwenye kijiji chake.
“Ni kweli, siku hiyo, mimi na msaidizi wangu, Daudi Kisonela na mgambo wa kijiji tulifika eneo la tukio na kushuhudia Simon akivuja damu mwilini huku mkono wake wa kulia ukining’inia nusu hadi mfupa wa ndani ukionekana baada ya kupigwa mapanga na Frank akidai kamfumania na mkewe,” alisema mtendaji huyo.
Akaendelea: “Tuliwaweka kikao, tulimhoji mke akasema mumewe alikurupuka kumcharanga mapanga mtuhumiwa kwani si kweli.
“Kwa kauli ya mama huyo tulimtia hatiani Frank, tukamkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Dumila, cha ajabu wakati sisi tukitafuta usafiri, huku nyuma mtendaji wa kata alimuachia huru Frank huku akitukabidhi panga lenye damu kama ushahidi.”Akizungumza kwa tabu na mwandishi wetu katika wodi ya wanaume Hospital ya Misheni ya Berega, Gairo, Simon alisema:
”Siku ya tukio nilifika kwenye kigodoro kwa lengo la kusaka abiria, mtu mmoja aliniambia nimkodishe pikipiki aendeshe mwenyewe, kuna watu anataka kwenda kuwafuata baada ya makubaliano ya bei nikamkabidhi pikipiki yangu na mimi nikamsubiri palepale.
“Ilipotimu saa 6 nikaona jamaa harudi, nikaamua kuondoka nikiamini nitakutana naye njiani. Nilipofika mbali kidogo nikamuona Frank akiwa na panga mkononi huku akinishutumu kwamba natembea na mkewe, nilijaribu kubisha, akarusha panga la kichwa katika hatua ya kujihami nililipanchi na mkono ambapo alinikata mkono.
“Mkewe naye alikuwepo, alipojibu si kweli alimpiga,”alisema kijana huyo.
Juhui za mwandishi wetu kutaka kuzungumza na Frank zilikwama kufuatia mtuhumiwa huyo kutimua mbio akiogopa chombo cha habari.
Mganga mkuu wa hospitali aliyolazwa Simon, Alfred Chiponda alithibitisha kumpokea mgongwa huyo.
Mkuu wa kituo cha polisi, afande James Charles alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema vijana wake wanamsaka Frank.
No comments:
Post a Comment