TTCL

EQUITY

Friday, October 31, 2014

Wabunge tisa wajiuzulu kumpinga Shy-Rose

Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (Eala) umechukua sura mpya baada ya wabunge tisa, wakiwamo makamishna watano na wenyeviti wanne wa kamati za Bunge hilo, kuwasilisha barua za kujiuzulu nafasi zao hizo, ikiwa ni matokeo ya sakata linalomhusisha mbunge mwenzao kutoka Tanzania, Shy-Rose Bhanji (pichani).
Kutokana na hali hiyo, Bunge hilo ambalo lilikutana kwa wiki mbili huko Kigali, Rwanda liliahirishwa jana kwa muda usiojulikana, muda mfupi baada ya kushindwa kufanya uamuzi wa kumwadhibu Bhanji ambaye anakabiliwa na tuhuma mbalimbali za utovu wa nidhamu.
Mgogoro huo ulisababisha Eala kwa wiki mbili, kushindwa kufanya lolote lililokuwa limepangwa kwenye kalenda yake, kwani kila lilipokutana, wabunge walitoa hoja liahirishwe hadi pale suala la nidhamu dhidi ya Bhanji litakapotolewa uamuzi.
Mbunge huyo anatuhumiwa kutoa maneno yasiyokuwa na staha kwa wenzake, kuwakashifu na kuwatukana baadhi ya viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wa ziara ya ujumbe wa Eala katika nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), Ubelgiji.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana na baadaye kuthibitishwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Eala, Bobi Odiko zinasema makamishna na wenyeviti tisa waliwasilisha barua rasmi za kuachia ngazi kwa Spika wa Eala, Dk Margaret Zziwa... “Ndiyo, naweza kuthibitisha kwamba wamejiuzulu nafasi zao kwa kuandika barua rasmi kwa spika… bado nafuatilia nyaraka husika na baadaye nitatoa taarifa rasmi.”
Baadaye Odiko, alitoa taarifa rasmi ambayo pamoja na mambo mengine, ilitaja majina ya makamishna waliojiuzulu kuwa ni Abubakar Ogle (Kenya), Christophe Bazivamo (Rwanda), Hafsa Mossi (Burundi) na Jeremy Ngendakumana (Burundi), Patricia Hajabakiga (Rwanda).
“Hii sasa inamaanisha kwamba ili tume iweze kufanya kazi yoyote, lazima iundwe upya kwa mujibu wa kipengele cha tatu cha Sheria ya Uendeshaji wa Bunge la Afrika Mashariki,” anasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Alipoulizwa kuhusu majina ya wenyeviti ambao wamejiuzulu, Odiko alisema asingeweza kuyataja na kwamba alikuwa akifuatilia taarifa zao katika ofisi ya spika. Eala ina makamishna 10; wawili kutoka kila nchi na wenyeviti sita wa kamati.
Kwa maana hiyo kushindwa kufanya kazi kwa Tume ya Eala hivi sasa kunatokana na kujiuzulu kwa makamishna wote wa Rwanda na Burundi, hivyo tume haiwezi kukutana bila uwakilishi wa nchi hizo.
Hata hivyo, Odiko hakueleza sababu za wabunge hao kujiuzulu lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema walisema hawawezi kufanya kazi chini ya uongozi wa Spika Zziwa kwani amekuwa akibadili uamuzi wanaoufikia kwenye vikao.
Miongoni mwa mifano waliyoitaja ni kushindwa kuwasilishwa katika Bunge hilo, ripoti ya ziara ya makamishna na wenyeviti wa kamati wa Eala nchini Ubelgiji, huku wakidai kwamba kutowasilishwa kwake kulilenga kufunika madhambi yaliyofanywa na Bhanji.
Mmoja wa waliojiuzulu, Ogle wa Kenya aliliambia gazeti hili juzi jioni kwamba asingeweza kuendelea kufanya kazi katika tume ambayo mmoja wa wajumbe wake amekuwa akiwatusi, huku Spika akishindwa kuchukua hatua.

No comments:

Post a Comment