RAIS KIKWETE AWEKA SAHIHI MPANGO WA UMOJA WA MATAIFA LEO
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini Mpango wa Umoja
wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo wakati wa hafla hiyo maalumu iliyofanyika makao
makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 24,
2013.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo Februari
24, 2013 ameungana na Wakuu wenzake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa
Makuu kutia saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na
Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Addis
Ababa, Ethiopia.
Mhe. Rais Kikwete
alisema mara baada ya utiwaji saini wa Mpango huo kwamba: “Hii
ni siku kubwa na ya kihistoria kwa watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, jirani zake na Ukanda wote wa Maziwa Makuu. Ni siku ya
kukumbukwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),
Afrika, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Jumuiya yote ya
Kimataifa.
“Watu wa
Kongo wameteseka kwa muda mrefu sana. Wanastahili kupumua sasa.
Wanastahili kuishi maisha bora; maisha ambayo usalama wao
umehakikishiwa na kuthibitishwa; maisha ambayo yatawafanya waendeshe
maisha yao kwa kufanya mambo ya maana zaidi katika kuboresha maisha
yao ya kila siku.
“Saini
tulizotia kwa Mpango huo leo ni kielelezo cha dhati na ahadi ya
utekelezwaji wa yale yanayotarajiwa na watu wa Kongo na Ukanda wa
Maziwa Makuu kwa ajili ya Amani, Usalama na Ushirikiano.
“Kwa niaba
ya Serikali na Watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naahidi kwamba
sisi tutatekeleza kwa dhati yale yote yanayotarajiwa kwa upande
wetu”, alisema.
Mpango huo umetiwa
saini na viongozi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola,
Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki-moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja
wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma, pamoja na wenyeviti wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Ukanda wa Maziwa
Makuu (ICGLR) wametia saini Mpango huo kama mashahidi na wadhamini.
Mpango huo una nia
ya kuchangia juhudi ambazo zimefanywa na ICGLR na SADC katika
kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda wote wa Maziwa Makuu kwa
ujumla.
Mpango huo pia
umetilia maanani mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya
mashauriano kati ya wakuu wa nchi za ICGLR na SADCna Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa.
Mapendekezo ya
mpango huo ni pamoja na kuboresha sekta ya Ulinzi na usalama, hususan
jeshi la polisi, Kuimarisha mamlaka ya nchi hasa mashariki ya Kongo;
na kuendeleza ajenda kuhusu maelewano, kuvumiliana na kudumisha
demokrasia nchini humo.
Vile vile, nchi za
Kanda zimetakiwa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi jirani, kututoa
msaada wowote wa vikundi vya waasi, kuheshimu utawala na maeneo ya
nchi jirani na kuimarisha mahusiano ya Kanda.
Hali kadhalika,
Jumuiya ya Kimataifa imetakiwa kuisaidia DRC na Kanda yote ya Maziwa
Makuu kwa ujumla katika utekelezaji wa miradi muhimu pamoja na
mkataba wa Amani, Usalama na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aidha, Mpango huo
unapendekeza kuwepo kwa chombo cha usimamizi (Oversight Mechanism)
ambacho kitaundwa na viongozi wote wa nchi 11 pamoja na Umoja wa
Mataifa, SADC na ICGLR.
No comments:
Post a Comment