Sakata la dawa za kulevya jana lilitikisa Bunge mjini hapa baada ya
wabunge kutaka orodha ya ‘wauza unga’ ambayo Rais mstaafu Jakaya Kikwete
alisema anayo ili ifanyiwe kazi na mrithi wake, John Magufuli.
Akichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Ukimwi na ile ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema
Rais Kikwete aliwahi kuutangazia umma kuwa anayo orodha ya vigogo wa
dawa za kulevya hivyo alitaka wakamatwe ili watumiaji waachiwe.
“Kikwete alisema anayo orodha ya wauza dawa za kulevya. Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi (Mwigulu Nchemba) amfuate kule Msoga ili ampe hiyo
orodha. Naamini watumiaji wataachiwa,” alisema.
“Vita ya dawa za kulevya siyo ya Paul Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam), hii ni vita ya Serikali na naamini itamuunga mkono. Mtu
akipimwa akionekana ni mtumiaji atusaidie kumpata muuzaji,” alisema.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alimtaka Rais Magufuli kuacha
kuendesha nchi kwa sanaa na kutafuta habari zake zipewe uzito katika
vyombo vya habari, badala ya kushughulika na tatizo.
Mbunge huyo alisema kwa mwaka 2016/2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za
Kulevya nchini ambayo ndiyo yenye dhamana ya vita hiyo haikupata fedha
za maendeleo. “Leo bajeti ya tume ni sifuri halafu anasimama mkuu wa
nchi anasema vita ipiganwe. Tuache kutafuta vichwa vya habari kwenye
vyombo habari,” alisema Mdee.
Aliongeza, “Vita hii inahitaji utashi wa kisiasa. Kikwete alisema
anawajua wauza unga kwamba ana orodha. Alipoondoka Ikulu si aliacha
mafaili? Orodha unayo hapo Ikulu tusicheze na akili za Watanzania,”
alisema.
No comments:
Post a Comment