Tume ya Taifa ya Haki za Kibinadamu (KNHRC)
imesema imeshangaza sana na video na picha ambazo zinaenea kwenye
mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri wakati wa
maandamano hayo.
Picha hizo zinawaonesha polisi wakiwakabili waandamanaji kwa marungu.
Baadhi
ya wakenya mtandaoni pia wamekuwa wakiwashutumu maafisa wa polisi na
kitambulisha mada #StopPoliceBrutality (Komesha Ukatili wa Polisi)
kinavuma Kenya.
Maandamano ya upinzani Nairobi
Kwa mujibu wa
kituo cha redio cha Capital FM jijini Nairobi, mmoja wa waliokabiliwa na
polisi alifariki baadaye akipokea matibabu.
"Kikosi cha Polisi ni
kikosi cha nidhamu na si kikosi cha kutumia nguvu. Kanuni ziko wazi
kuhusu jinsi ya kuwashughulikia raia wakati wa maandamanaji,” tume hiyo
imesema kupitia Twitter.
Mamlaka huru ya kiraia inayofuatilia
shughuli za polisi (IPOA) pia imeshutumu vitendo vya maafisa wa polisi
na kusema walivuka mipaka.
Mwenyekiti wa mamlaka hiyo Bw Macharia Njeru amewaambia wanahabari kwamba polisi walitumia nguvu kupita kiasi.
Amesema
maafisa wa mamlaka hiyo wanakamilisha uchunguzi na watawasilisha ripoti
kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili hatua zichukuliwe dhidi ya
maafisa husika.
Muungano wa upinzani CORD umekuwa ukifanya
maandamano Jumatatu kila wiki kuwashinikiza maafisa wakuu wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (IEBC) wajiuzulu.
Viongozi wa CORD wamesema maafisa hao hawawezi kusimamia uchaguzi huru na wa haki wakati wa uchaguzi mkuu ujao 2017.
Wameahidi kuendelea na maandamano hayo hadi maafisa hao watakapong’atuka.
No comments:
Post a Comment