MWENYEKITI wa Taasisi ya MO Dewji,
Mohammed Dewji kwa kushirikiana na kampuni ya Darecha Limited leo
wamezindua shindano la Mo Mjasiriamali lenye lengo la kusaidia kukuza
ujasiriamali miongoni mwa vijana.
Shindano
la Mo Mjasiriamali litatoa fursa ya ukuzaji wa mitaji, ulezi wa
wajasiriamali na mitandao ya biashara kuongeza mwanga, ujasiri na
kuzalisha wajasiriamali Tanzania.
“Mimi
kama Mjasiriamali kijana na mzaliwa wa Singida vijijini, sikufikiria
hata mara moja kama leo ningekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa moja ya
makampuni yaliyofanikiwa sana katika nchi yetu na hata barani Afrika.”
Inasema taarifa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MeTL kwa vyombo vya habari
mwishoni mwa wiki.
Aidha
alisema Afrika ni moja ya bara linalokua kwa haraka na lenye ukuaji
imara wa uchumi na amini vijana wa Tanzania wana nafasi kubwa ya kutumia
fursa hizo ili kujiletea uchumi endelevu.
Lakini
pamoja na ukweli huo changamoto kama za ukosefu wa mitaji, ukuzaji
ujasiriamali na mitandao ya biashara zimekatisha tamaa vijana wengi
kukuza kwa mafanikio makampuni yao hapa Tanzania na hivyo kupunguza kasi
ya ukuaji wa uchumi kwa watu wa kipato cha kati.
Kwa
mujibu wa takwimu zilizotolewa na Benki ya maendeleo ya Afrika (ADB),
watu wenye kipato cha kati katika bara la Afrika wataongezeka na kufikia
watu bilioni 1.1 ifikapo mwaka 2060.
Watu wa kipato cha kati ndio wanaochagiza ukuaji wa uchumi kutokana na mahitaji yao na pia ari ya ujasirimali.
Pamoja
na ukweli huo kunachangamoto nyingi zinawakabili watu hao wa kipato cha
kati. Mathalani nchini Tanzania changamoto kubwa kwa vijana
wajasirimali ni gharama za kutafuta mtaji kwa kazi hizo.
“Kuna
haja kubwa ya kuhakikisha kwamba vijana hawa wanaondolewa tatizo la
ujasirimali ili waweze kusukuma mbele uchumi wa Tanzania.” inafafanua
taarifa hiyo.
Aidha
kwa kuwa Tanzania inaelezwa kuwa ni nchi ya 19 katika bara la Afrika
kuhusiana na fursa na ujasirimali ipo haja ya kusaidia ili kuiondoa
katika nafasi hiyo. Taarifa ya nafasi ya Tanzania imo katika ripoti yake
ya mwaka 2014 ya Africa Prosperity Report.
Taarifa ilifafanua zaidi kwamba kutokana na haja hiyo Taasisi ya Mo Dewji
na Darecha Limited wameungana pamoja na kuanzisha shindano la Mo
Entrepreneurs ili kutambua na kuuenzi mchango wa wajasirimali chipukizi
na kufanikisha ndoto zao.
Ili
kufanikisha nia ya kuwa na wajasiriamali wengi, shindano hilo
linatarajiwa kuwa daraja kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji, Mohammed Dewji
(MeTL Group na Mwenyekiti wa Mo Dewji Foundation)
ambapo vijana ambao wanaonekana wana kitu cha kufanya, lakini hawana
msaada watashiriki kwa lengo la kupata msaada katika mfumo wa mtaji,
mtandao na usimamizi wa ukuaji wa shughuli wanayofanya au kutaka
kuifanya ili kuianzisha na kuikuza.
Mambo
hayo yatatekelezwa katika mfumo wa shindano litakalogusa wajasiriamali
ambao wana ari na nia ya dhati ya kuendeleza shughuli walizofikiria na
kuzianzisha kwa lengo la kuinua uchumi wao binafsi na wa taifa.
Washindi
watatu watakaotangazwa Aprili mwaka huu watapatiwa mtaji wa kuanzia au
kuendeleza, pia watapatiwa maarifa ya kuendeleza shughuli zao na
kuanzishwa mtandao wa kibiashara na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa MeTL
Group na mwenyekiti wa Mo Dewji Foundation, Mohammed Dewji.
Wakati
akipewa tuzo ya Forbes ya mwaka 2015, Mohammed Dewji aliitoa kwa
heshima ya vijana akiwatakia kila la heri waking’aa, kuvunja nira ya
woga, kukabili changamoto na kuendelea katika ujasiriamali kwa lengo la
kufanya dunia yetu mahali bora pa kuishi.
Kwa habari zaidi tembelea: http://www.modewjifoundation.org/mo-entrepreneurs-competition
No comments:
Post a Comment