Uswisi imeahidi kuendeleza ushirikiano na
Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo huku mkazo mkubwa
ukiuelekeza katika kuendeleza elimu ya mafunzo ya ufundi stadi.
Balozi wa Uswis nchini Tanzania Mhe. Florence Tinguely Mattl akisaini kitabu.
Balozi
wa Uswisi hapa Nchini Mhe.Florence Tinguelly Mattli, amesema hayo
alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.
Balozi Florence amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kuwepo kwa
miradi mingine ambayo nchi hiyo inaendelea kuitekeleza kwa kushirikiana
na Tanzania, katika awamu hii Uswisi itatilia mkazo katika elimu ya
ufundi stadi ili kuwawezesha vijana wanaosoma kuwa na ujuzi
unaowawezesha kuzalisha bidhaa na kujipatia kipato kama ambavyo nchi ya
Uswisi inafanya.
Maeneo mengine ambayo viongozi hao wamezungumzia ni kuimarisha
ushirikiano katika uwekezaji, ambapo Rais Magufuli amewaalika wawekezaji
kutoka Uswisi kufanya biashara na Tanzania, kuimarisha huduma za
bandari na pia kuongeza uwezo katika kukabiliana na vitendo vya Rushwa.
Kuhusu Sekta ya afya, Rais Magufuli ameipongeza Uswisi kwa
kushirikiana na Tanzania kupitia Taasisi ya Afya Ifakara katika
kukabiliana na changamoto mbali mbali za kiafya ikiwemo kukabiliana na
ugonjwa wa Malaria na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuitumia taasisi
hiyo ili kusaidia juhudi za kukabiliana na magonjwa.
Wakati Huo Huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa
Nchini Mheshimiwa Jasem Al Najem Ikulu, Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo, Balozi Al Najem amewasilisha salamu za mfalme
wa Kuwait Mheshimiwa Sabah Al Ahamad Al Jaber al Sabah kwa Rais
Magufuli, ambaye amempongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano
na amemhakikishia kuwa Kuwait itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
maendeleo ikiwemo kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali katika
sekta za ujenzi, Maji na Kilimo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa ujenzi wa barabara ya Chaya -
Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 kwa kiwango cha lami ambapo Tanzania
imeomba ufadhili wa dola milioni 85, Mradi wa Maji wa Same - Mwanga -
Korogwe ambapo Tanzania imeomba ufadhili wa dola milioni 20 na Mradi
mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Mhongo na Luhiche
Mkoani Kigoma ambapo Kuwait imeonesha nia ya kuufadhili.
Aidha, Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Kuwait kwa salamu zake za
pongezi na amewaalika wafanyabiashara wa Kuwait kushirikiana na Tanzania
katika biashara na uwekezaji.
Katika Hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mhe.
Louise Mushikiwabo aliyetumwa kuleta ujumbe maalum wa Rais Paul Kagame
wa Rwanda.
Katika Ujumbe huo, Mheshimiwa Kagame amemuhakikishia Rais Magufuli
kuwa Rwanda itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali
za kiuchumi, kisiasa na kijamii hasa ikizingatiwa kuwa licha ya kuwa ni
nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda ni marafiki na
ndugu wa Tanzania.
Rais Kagame pia amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri
aliounesha katika siku za mwanzo za uongozi wake wa awamu ya tano ambao
amesema anauunga mkono.
Pamoja na kupokea salamu za Rais Kagame, Rais Magufuli na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Rwanda wamezungumzia mgogoro wa kisiasa unaoendelea
nchini Burundi na wote kwa pamoja wameona ni muhimu kupata suluhisho kwa
njia ya mazungumzo ili wananchi waweze kuishi kwa amani na kuendelea na
shughuli zao maendeleo
No comments:
Post a Comment