Mjasiriamali Daniel Julias, akikagua mzigo
uliofikishwa katika eneo lake la biashara, kwa ajili ya kuupima.
Kuna kasumba dhidi ya biashara ndogo zikionekana
hazina maana na zinadharauliwa, ingawa uk0weli upo katika upande wa pili
kwamba, kwa kiasi kikubwa zinainua maisha ya baadhi ya watu kiuchumi.
Moja ya maeneo hayo ni ujasiriamali wa kuokota na kuuza chupa za
plastiki jijini Dar es salaam, ambao watu wengi hawajaupa nafasi katika
kubadilisha maisha ya wengi katika maendeleo.
Hilo limejidhihirisha kwa maisha ya kijana, Daniel Julias,
anayejishughulisha na ujasiriamali wa kuokota na kuuza chupa za plastiki
jijini Dar es salaam.
Julias anasema, biashara hiyo imemsaidia kuhudumia familia yake
aliyoiacha kijijini kwao alikotaja ni mkoani Tanga, hata akafanikiwa
kununua tofali kwa ajili ya ujenzi, huku akiwasaidia wazazi wake
kuendesha kilimo.
“Mimi nilivyokuja Dar es Salaam, nilihangaika sana kutafuta
maisha, lakini namshukuru Mungu, kwani ujasiriamali huu unanipatia
kipato ambacho kinanisaidia mimi na familia yangu iliyopo kijijini,”
anasema Julias.
Anasema, imezoeleka kwa baadhi ya watu wanapoonekana kuokota chupa
jalalani na barabarani, wanahisiwa wamechanganyikiwa au wahuni, dai
analolipinga kwa kila namna.
Julias anajigamba, hiyo ni biashara inayowaingizia kipato kikubwa na wakati mwingine katika kiwango cha kuwazidi waajiriwa.
Julias, mkazi wa Keko jijini Dar es Salaam, ambaye shughuli zake za
kuokota na kuuza chupa anaziendesha katika eneo la Kimara Baruti,
anasema katika kazi hiyo wapo watu anaowaita ‘wasiojitambua.
Anawatafsiri watu hao kuwa wanatafuta fedha za kwenda kunywa pombe
na kutumia dawa za kulevya kupitia biashara ya ukusanyaji chupa, lakini
katika sura ya pili, wapo wanaojitambua na wamefanikiwa kimaisha.
HOFU YA DHARAU
Anasema, waokota na wauza chupa za palstiki wengi, hawafanyi hivyo
katika maeneo wanayoishi, kwa kuhofia kuchekwa na kudharauliwa, kutokana
na jamii kukosa uelewa sahihi kuhusu kazi hiyo.
Tino Fantaeli, ambaye ni mfanyabiashara wa kuokota na kuuza chupa
na mkazi wa Makumbusho Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, anayefanya
biashara zake eneo la Kimara Baruti, anaeleza:
“Mimi nikiondoka nyumbani kwangu, watu wanajua nafanya kazi katika
ofisi ya maana, kwani nakuwa nimevaa vizuri, tofauti na hivi
unavyoniona.”
Anaeleza kuwa, kutokana na tabia hiyo ya jamii kuwadharau, wamekuwa
wakifanya biashara hiyo wakitawaliwa na hofu ya kuchekwa na
kudharauliwa.
Julias anafafanua kuwa, jamii inapaswa kufahamu kuwa, mbali na
kuokota chupa na kuuza, pia ni wadau bora wa kusafisha mazingira kwa
kuokota chupa zinazozagaa kama takataka.
GHARAMA ZA CHUPA
Anasema, mtu anayefanya biashara hiyo na anajituma ipasavyo, anaweza kutanua wigo wao wa kipato.
“Sikudanganyi, mtu akijitahidi na akiwa na malengo, anaweza
kuingiza hata zaidi ya sh.60, 000 kwa siku, kwani kwa siku tunauza mara
tatu; asubuhi, mchana na jioni. Sasa hapo mtu akijitahidi anafikia
malengo,” anajigamba Julias.
Anaongeza kuwa, huwa wanauza kilo moja ya chupa za plastiki kwa bei
ya sh. 200, mifuko ya pkastiki sh.150 na ndoo zilizoharibika sh.300.
Julias anaongeza kuwa, baada ya kuwauiza wanunuzi wao ambao huwa
wanaenda kuziuza chupa hizo katika viwanda vikubwa katika maeneo ya
Tegeta, Mwenge, Kurasini na Mbagala, ambako huwauzia raia wa kigeni
anaowataja kuwa Wachina, kwa bei ya kati ya sh. 450 hadi 500 kwa kilo.
Anasema, wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa, mara nyingi huingia
kwenye masoko makubwa ya chupa na kupeleka katika mikoa kama vile
Morogoro na nchi jirani ya Kenya, zinakochukuliwa kama malighafi ya
viwandani na kuyeyushwa ili kutumiwa tena.
FAIDA ALIZOPATA
Akieleza faida anazozipata tangu aanze biashara hiyo kwa muda wa
miaka miwili, anataja ni pamoja na kumsaidia kulipa kodi ya nyumba
anayoishi na kuwasaidia wazazi wake waliopo kijijini.
“Unajua Dar es Salaam sio kwetu, hivyo ninavyopata fedha, naangalia
kuwekeza nyumbani, kwani hivi sasa nimenunua matofali kwa ajili ya
kujenga nyumba yangu na huwa nawasaidia wazazi wangu kulipia wafanyakazi
wa shambani katika msimu wa kilimo,” anasema.
Katika eneo la Mwenge Mlalakuwa jijini Dar es Salaam, mwandishi wa
makala hii alikutana na mwanamke mzee aliyejitambulisha kwa jina la
Maria Mwangosongo (87), akiwa amebeba mzigo mgongoni uliokuwa na chupa
za plastiki.
Bibi huyo anaeleza, kwa kawaida anazipeleka chupa hizo ili kuziuza,
apate fedha za kujikimu kimaisha, yeye na wajukuu wake wanaoishi
pamoja.
“Mimi ni mjasiriamali, mjukuu wangu hizi chupa nilishinda jana huku
naokota mitaani, hapa nikienda kuuza najipatia fedha na kwenda kununua
chakula nile na wadogo zako (wajukuu wake)nyumbani,” anajieleza mwanamke
huyo mzee.
Anasema, kazi hiyo ya kuokota na kuuza chupa za plastiki, aliianza
baada ya kubaini hana msaada kutoka kwa ndugu na watoto wake,
waliomwachia watoto zao, pasipo kumwelekezea kipato chochote.
“Mimi ni mjasiriamali mjukuu wangu. Hizi chupa nilishinda jana huku
naokota mitaani hapa, nikienda kuuza najipatia fedha na kwenda kununua
chakula nile na wadogo zako nyumbani (wajukuu wake),” anasema.
Anafafanua, amekuwa akipata changamoto wakati wa kuokota chupa,
kwani mara nyingi wanapenda kwenda jalalani sehemu za starehe, kwani
huko ndiko kuna watumiaji wa vinywaji vya plastiki.
Bibi huyo naye anajigamba kuwa, biashara hiyo imesaidia kuweka
mazingira ya jiji la Dar es Salaam safi na kuyatunza, kwani iwapo
kusingekuwepo, wafanyabishara wanaonunua chupa, jiji lingebaki chafu.
DHANA POTOFU
Hata hivyo, wakati kuna kundi la wafanyabishara wa kuokota na kuuza
chupa za plastiki jijini, bado katika jamii kuna dhana potofu
inayowahusu.
Mjasiriamali aliyejitambulisha kwa jina moja la ‘Mangi’ wa eneo la
Kimara, jijini Dar es Salaam, anasema watu anaowatafsiri ni
wafanyabiashara hiyo, kumbe katika uhalisia ama wana matatizo ya akili
au walevi wa pombe kupindukia.
Anasema, jambo linalomkatisha tamaa mara nyingi ni kitendo cha
baadhi ya watu katika jamii kumdharau pale anapoonekana akiokota chupa,
kununua na hata kuzibeba katika maeneo mbalimbali ya jiji.
“Wengi wakiniona naokota chupa, wanadhani mimi ‘Chizi’. Huwa
nachukia sana, kwani sina uwezo wa kuwabadilisha mtazamo wao,” anasema.
Anakiri, kuna kundi la anaowaita ‘mateja’ kwa maana ya watumiaji wa
dawa za kulevya, wanaofanya kazi hiyo, ndio ambao mara nyingi
wanawaharibia sifa zao.
Julias anaeleza kuwa, jamii inapaswa iwatambue na kuwathamini wanaokusanya makopo, kama wanaharakati wa utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment