TTCL

EQUITY

Tuesday, December 15, 2015

Ukosefu wa maadili chanzo cha migogoro- Mabula

Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Mh. Angelina Mabula amesema kuwa tatizo la watumishi wa serikali kutofuata matumizi bora ya ardhi pamoja na mipaka yao ya kazi ni moja kati ya mambo makubwa yanayosababisha migogoro mingi ya ardhi.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Mh. Angelina Mabula
Waziri Mabula amebainisha hayo wakati akifanya mahojiano na kituo cha habari cha EATV kuhusu migogoro ya ardhi ya mara kwa mara ukiwemo na ule wa hivi karibuni uliotokea mkoani Morogoro, ambapo mtu mmoja aliuawa na ng'ombe 74 kukatwakatwa mapanga, na kusema kuwa watendaji wa serikali hasa wenyeviti wa vijiji na maafisa ardhi, wanatakiwa kuwa makini sana kwenye suala la ardhi.
''Wenyeviti wa vijiji wana uwezo wa wa kugawa ardhi hadi hekari 50 na kwa kufuata sheria na taratibu na vikao halali vya vijiji, ila kama wasipo acha sehemu za kulishia mifugo sehemu za kupitia hiyo mifugo pamoja na maeneo ya wakulima hapa lazima migogoro itokee, kitakacho toa suluhu kwa mazingira kama haya ni watendaji na wananchi kufuata sheria na kuzingatia rekodi mbalimbali za ardhi katika maeneo hayo, pia wawekezaji kutumia matumizi bora ya ardhi kama walivyobainisha wakati wa kuyachukua", alisema Mh. Mabula.
Aidha Mh. Mabula ametoa rai kwa wananchi na viongozi wa serikali kufuata sheria na taratibu hasa kwa kuangalia sheria ya ardhi ya mwaka 1999 sheria namba tano, ambayo inabainisha vizuri namna nzuri ya matumizi ya ardhi, pia waandae utaratibu mzuri wa kutatua kero za wananchi kwa wakati muafaka.
Kuhusu matatizo ya kero za wananchi wa jimbo la Ilemela Mwanza ambapo Bi Mabula ndiye Mbunge wa jimbo hilo, amesema kwamba atajikita kwenye mambo muhimu aliyoahidi wakati wa kampeni na kuyatekeleza kwa wakati husika.
''Kuna tatizo la maji na hadi mwezi mei katika jimbo la Ilemela itakuwa historia, kwani tuna fedha kutoka jumuiya ya Ulaya na zinaendelea kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji na maeneo kadhaa yameanza kupata maji, mfano eneo la Kitangiri pamoja na Mji mwema wananchi wameanza kunufaika na miradi hiyo'' alisema Waziri Mabula
Kuhusu suala la barabara Mh. Mabula amesema kuwa kwa sasa nyingi hazipitiki kutokana na mvua inayoendelea kunyesha hasa katika maeneo ya visiwani, na serikali inalitambua tatizo hilo, na kwamba muda mfupi ujao serikali itahakikisha inatatua tatizo la barabara kulingana na mahitaji ya maeneo husika.

No comments:

Post a Comment