Miaka mitatu iliyopita Mwanasheria maarufu nchini, Mabere Marando
alitoa kauli ambayo si mimi tu, bali Watanzania wengi hatukumwelewa.
Kauli yenyewe ilikuwa hivi: “Tanzania ni nchi yenye bahati. Ni nchi pekee duniani inayojiendesha bila Rais.”
Wapo walioichukulia kama vijembe vya kisiasa, na mimi ni mmoja wao, ila
kadri siku zinavyopita na hasa baada ya Rais Dk. John Pombe Magufuli
kuingia madarakani, kauli ile inadhihiri usahihi wake.
Sitanii, Novemba 20, 2015 wakati anazindua Bunge, Rais Dk. Magufuli
alisema baadhi ya watu wamesafiri nje ya nchi mara nyingi kuliko
walivyokwenda vijijini kwao kuwaona wazazi wao.
Bila shaka alitumia diplomasia, lakini uhalisia alikuwa akimsema Rais
mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye wanaharakati wanasema ametumia muda
mwingi nje ya nchi katika kipindi cha uongozi wake.
Nimeamini kuwa maneno ya wahenga, si ya kubeza. Walisema sikio la kufa
halisikii dawa. Wapo wanaosema Kikwete tangu ametoka madarakani
amesafiri mara sita nje ya nchi, ila mimi nilizo na uhakika nazo ni nne.
Amekwenda Ethiopia, Afrika Kusini, Comoro na wiki iliyopita Uingereza.
Anafanya ziara hizo, bila hata kuona aibu kutokana na agizo la Rais
Magufuli, hata kama yeye si mtumishi wa umma tena.
Mbunge wa Kibamba (CHADEMA), wakati huo akiwa Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika, alisema Rais ni dhaifu. Ameshindwa kusimamia Serikali na
watumishi wa umma wanafanya kila wapendalo.
Kilichomkuta baada ya kauli hiyo ni kufukuzwa bungeni kama adhabu ya
kutoa lugha ya kukera. Hata hivyo, waliokuwa wakifuatilia hali halisi ya
utendaji wa Serikali, walibaki wanasikitika.
Leo nchi yetu ina kipindupindu kila kona. Maeneo kama Mkoa wa Kagera,
tangu enzi za Mkoloni hayajawahi kupata kipindupindu. Vyanzo vya maji
vilikuwa vya kutosha. Usafi ulikuwa wa hali ya juu. Wenyeji walimiliki
mashamba makubwa yenye kuruhusu hewa safi kusambaa na yalipaliliwa na
hata wasiokuwa na choo, walitumia zana ya asili (omushote).
Ingawa maji ya bomba ni msamiati kwa maeneo mengi ya Kagera, ila maeneo
kama Mlima wa Kibeta, Rugambwa, Kahororo, Ihyungo, Nshambya na Nyangoye
hayakuwa makazi ya watu.
Kwa sasa watu wamejenga milimani sawa na walivyofanya Mwanza. Hawa
waliojenga milima hiyo hawana mahala pa kuchimba mashimo ya vyoo au
mashimo ya maji taka (septic tanks).
Wengi wanatumia mapipa au vyoo vilivyojengwa kwenye mawe. Mvua
zikinyesha vinatiririsha maji taka katika mto Kanoni. Mto Kanoni
unasukuma uchafu mpaka Ziwa Victoria. Pale Bakoba yanapochukuliwa maji
ya bomba, ni jirani na mto Kanoni unapomwagia maji ziwani. Niulize
kinachofuata. Maji ya ziwa yanavutwa na kuingizwa kwenye matangi, na
sina uhakika kama yanatibiwa vyema kuua wadudu.
Sitanii, ni wakati wa Serikali ya Kikwete tumeshuhudia ujenzi holela.
Kwa mji wa Bukoba kama hakuna kitakachofanyika juu ya wakazi wa Manispaa
waliojenga kwenye mawe maeneo niliyoyataja ikiwamo Buyekela kwa juu,
basi tujue kipindupindu imefika si mgeni wa kupita. Mkuu wa Mkoa wa
Kagera asimamie ujenzi wa mfumo wa maji taka kwa gharama ya wakazi wa
milimani.
Nashauri ujengwe mfereji mmoja mkubwa, hata ikibidi kwa gharama za
wakazi wa milima hiyo, na mfereji huo wa maji taka utoe fursa ya wenye
nyumba kuunganisha vyoo vyao kwenye mfereji huu kisha kwa chini maeneo
ya Buyekela au Kashozi Road lichimbwe shimo kubwa la maji taka, mfereji
huyo utumike kukusanya uchafu na ufyonzwe baadaye kupelekwa katika dampo
huko Kata Nyanga. Bila kufanya hivyo, kipindupindu kitakuwa cha kudumu
Bukoba.
Alipokutana na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam,
Rais Dk. Magufuli amlitoa kauli iliyopasua moyo wangu, kwa kusema: “Sijui
kama mnafahamu, lakini ukweli ni kwamba tangu Bajeti Kuu ya Serikali ya
mwaka 2015/2016 ipitishwe Juni 30, mwaka huu, hakuna fedha yoyote
iliyokwisha kutolewa kwenye wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Kama kutolewa, basi tutakuwa tumeanza kuzitoa kwenye wizara kuanzia
mwezi huu (Novemba 2015), Katibu Mkuu Kiongozi yuko hapa, aseme. Miezi
sita tangu bajeti hiyo ipitishwe, hakuna hata senti kwa ajili ya
maendeleo iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya wizara yoyote, bali
zilizokuwa zikitolewa ni zile za mishahara tu na kwenye shughuli
nyingine.
“Kwa hiyo, ninapojaribu kusema haya na kusisitiza umuhimu wa ninyi
kulipa kodi, hatufanyi haya kwa sababu ya jeuri, bali kwa nia njema ili
malengo ya Watanzania yaweze kutimia. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu
zangu.” Maneno haya yamenifanya nilowane mwili mzima. Nikakumbuka bajeti
zilizopita na Rais aliyemaliza muda asivyoona aibu.
Zipo wizara kwa miaka mitano mfululizo zimepata asilimia 20 ya fedha
zilizotengwa. Huduma za jamii zimezorota kwa kiwango kikubwa, kwa sababu
kuu moja tu. Rais wetu aliyemaliza muda amekuwa akienda nje ya nchi
kubembeleza tupewe misaada. Mmoja wa misaada iliyolidhalilisha taifa
letu ni huu wa MCC. Kwa miaka miwili sasa Wamarekani wanasema utatolewa.
Haujatolewa.
Rais Dk. Magufuli umeyaona na unayafahamu haya. Hotuba yako
tumeichapisha yote kwenye gazeti letu. Hayo unayoyashuhudia ndiyo
yamewafanya Watanzania wengi kuichukia CCM. Ukisema fedha za maendeleo
hazijapelekwa wizarani, hii inamaanisha wakandarasi na wazabuni wote wa
Serikali hawajalipwa kwa kazi walizozifanya kwa muda wa miezi sita au
zaidi.
Mniwie radhi naomba niliseme hili. Hazina ya Tanzania inategemea zaidi
uimara wa waziri wa fedha. Hata kama tunalenga kutoa kipaumbele kwa
jinsia, tuangalie nani tunamkabidhi nini. Hii dhana ya 50 kwa 50
haikuletwa iangamize mataifa machanga. Dhana hii imeletwa kwa nia njema
kuwezesha kinamama, ila si kwa mtindo aliofanya Kikwete.
Wapo waliomshambulia Profesa Ibrahim Lilpumba aliposema Waziri wa Fedha
aliyemaliza muda, Saada Mkuya hakuwa ameiva kushika wadhifa kama huo
ambao ni roho ya nchi. Mimi ni mmoja wa walioamini hivyo, ila hoja ya
Profesa Lipumba ilipotoshwa na wanaharakati wakasema Waziri wa Fedha
hakustahili kuwa Mwanamke.
Yapo mambo sikubaliani na Lipumba, lakini hili la kusema Saada Mkuya
hakuwa na sifa za kushika wadhifa huu, nitakuwa wa mwisho kupingana
naye. Narudia, wapo wanawake mahiri, kama Dk. Asha Rose Migiro, Samia
Suluhu Hassan, Amina Salum Ali, Getrud Mongela na wengine wengi wenye
sifa za kutosha kushika wadhifa mzito kama huu.
Nazikumbuka vyema bajeti za Basil Mramba akiwa Waziri wa Fedha katika
Serikali ya Rais Benjamin Mkapa. Mramba pamoja na makosa yake ya
kiubinadamu kwamba sasa hivi ‘anachezea ndoo’ lupango, lakini mtakumbuka
wakati wa Rais Mkapa nchi hii uchumi ulivyosimama. Serikali ilifika
mahala ikarejesha heshima kwa wafanyakazi.
Nchi ilifika mahala ikaweza kujitegemea katika mambo mengi. Hapo juu
nimezungumzia kipindupindu, lakini Mkapa akiwa Rais alimshinikiza na
kumwezesha Waziri wa Maji wakati huo, Edward Ngoyai Lowassa miradi
mikubwa ya maji ikajengwa. Tulishuhudia mradi wa maji kutoka Ziwa
Victoria hadi Shinyanga na Kahama. Maji yalipofika Shinyanga
kipindupindu ikafutika.
Mkapa alikuwa akiimba sera ya maji mita 400 kutoka mlango wa kila
familia kwa aliye mbali. Mramba ilikuwa ukimhoji anakwambia fedha zipo,
tatizo ni watu kushindwa kuzitumia (absorption capacity). Rais Magufuli
ikiwa gazeti hili litaingia mtaani kabla ya kutangaza Baraza la Mawaziri
chondechonde nakusihi. Heshimu jinsia, lakini tanguliza masilahi ya
taifa kwanza.
Mwanaume asiye na uwezo usimweke katika Baraza la Mawaziri. Mwanamke
asiye na uwezo, usimweke katika Baraza la Mawaziri. Baraza si darasa. Si
mahala pa kufundishia uongozi. Kaulimbiu yako ya HAPA KAZI TU, ianzie
kwenye Baraza. Sitarajii upeleke watu kwenye semina elekezi ambazo
zimefanyika nyingi katika serikali zilizopita, lakini hakuna lolote
zilicholifanyia taifa.
Hivi hata kazi ya kukamata makontena ya wafanyabiashara uliowataja
inahitaji semina elekezi? Hivi hata kufanya usafi lazima Rais aunde
Kamati au Tume ya kuchunguza kwa nini usafi haufanyiki? Nakuhakikishia
Mheshimiwa Magufuli, agizo lako la watu kufanya usafi linatelekezeka.
Nimeshuhudia Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela alivyowabana wakazi wa
Kagera. Watu wamechimba vyoo wanalia!
Sitanii, hata kwenye vijiwe vya kahawa au baa, leo unaona kuwa watu
wanawaza kuwa Serikali ipo. Ni masikitiko makubwa kuwa mtangulizi wako
hata alipoaga kuwa angetembelea wizara, mkoa au taasisi fulani,
watumishi kitu pekee waliochokuwa wanafanya ni kuandaa hotuba nzuri,
chai na… Akifika, wanapiga picha, hotuba inatolewa, kisha anapongezwa
kwa kazi!
Naomba kuhitimisha makala hii kwa ushauri. Kama ulikuwa unawaza hili,
basi kuanzia leo lifute. Kitu kinachoitwa misaada nchi yetu haiwezi
kuendelea kwa misaada. Wawezeshe Watanzania wenye nia ya kufanya
biashara na kuwekeza, wafanye kazi. Watanzania wakiwekeza, watalipa
kodi, wataajiri Watanzania na hata fedha zao watakazopata hizo za kigeni
baada ya kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi, zitabaki kwenye benki za
hapa ndani.
Rais Dk. Magufuli wezesha wazawa, nchi ipige hatua, ukitegemea misaada,
utasubiri sana. Yote hayo na mengine ninayowaza, sasa yananifanya
nikubaliane na Marando, kuwa kweli inawezekana Tanzania imejiendesha
miaka 10 bila Rais, ambayo ni bahati ya pekee. Je, Magufuli ungependa
nawe uingie katika mkondo wa Kikwete? Kupanga ni kuchagua.
No comments:
Post a Comment