Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Ally Simba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na makampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Airtel, Halotel na Zantel na Smart kwa kuto kukidhi vigezo. Pia amesema kuwa Makampuni hayo yamepigwa faini ya shilingi milioni 25 kwa mamlaka ya mawasiliano Tanzania kabla ya Januari 29 mwakani.
Mwanasheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Elizabeth Zagi akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Ally Simba jijini Dar es Salaam leo.
JAMHURI YA YA MUUNGANO YA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
HATUA ZA KISHERIA NA KIUDHIBITI
KWA MAKAMPUNI YA SIMU YALIYOSHINDWA KULINDA WATEJA WAKE KITEKNOLOJIA NA
KISHERIA KUHAKIKISHA USALAMA WA MAWASILIANO YAO
1. Katika shughuili zake za udhibiti wa
huduma za mawasiliano nchini, Mamlaka ya Mawasilaino Tanzania imepokea
malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi ya kuwepo
mazingira yasiyo salama katika huduma za mawasiliano na hivyo
kusababisha kufanyika kwa vitendo vya utapeli unaofanywa kwa kutuma
jumbe za udanganyifu na kulaghai, hivyo kusababisha watu kujipatia pesa
kwa njia ya udanganyifu. Kwa mfano kupokea ujumbe kutoka namba
unayoifahamu ukikuagiza utume fedha au ujumbe wa kashfa au matusi wakati
hautoki kwa mhusika mwenye namba. Mamlaka imepokea malalamiko mengi
kutoka kwa wateja na malalamiko mengine hupelekwa Polisi. Kwa miezi
miwili tu, matukio 42 yameripotiwa Polisi pamoja na TCRA ambayo tukio
moja tu linakuwa na ulaghai wa takribani milioni 25 peke yake.
2. Tarehe 16 Oktoba, 2015 Mamlaka
iliwakumbusha watoa huduma za simu nchini juu ya wajibu wao kuchukua
hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya utumaji wa
jumbe za kilaghai na kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao
kutumika kutuma jumbe za udanganyifu na kulaghai. Kwa mujibu wa
uchunguzi uliofanywa na Mamlaka tarehe 16 Desemba, 2015 Mamlaka ilibaini
kuwa kampuni za Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart),
MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo), Airtel Tanzania Limited,
Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel) and Zanzibar
Telecom Limited inayojulikana kama Zantel) zimeshindwa, zimepuuzia na
zimekataa kufuata maagizo ya Mamlaka kuchukua hatua mara moja kuzuia
mitandao yao kutumika kutuma jumbe za kilaghai kinyume na Kanuni Na.8(a)
ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011 [the
Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team)
Regulations, 2011].
3. Tarehe 18 Disemba, 2015 Mamlaka
iliwaamuru watoa huduma za mawasiliano waliotajwa hapo juu kufika mbele
ya Mamlaka na kujieleza kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi
yao kwa kuvunja sheria na kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya
Kielectroniki na Postal ya Mwaka 2011 [the Electronic and Postal
Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011] kwa
kushindwa kuweka mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za
mawasiliano.
4. Watoa huduma walifika na kutoa maelezo ya utetezi kati ya tarehe 21 na 23 Desemba, 2015.
5. Baada ya kuwasikiliza na kutilia
maanani utetezi wa watoa huduma na kwa mujibu wa uchunguzi na majaribio
uliofanywa na Mamlaka, Mamlaka imejiridhisha kuwa mitandao ya watoa
huduma waliotajwa hapo juu haikuwa salama na kuwa watoa huduma hao
walishindwa kufuata maelekezo ya Mamlaka juu ya kuweka mazingira salama
katika huduma wanazotoa. Hivyo Mamlaka imejiridhisha kuwa watoa huduma
wamekiuka matakwa ya Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya
Kielectroniki na Postal ya mwaka 2011 (The Electronic and Postal
Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011)
inayowataka watoa huduma kuweka mazingira ya mitandao salama kwa
kuchukua hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya
uhalifu ikiwa ni pamoja na utumaji wa jumbe za kilaghai kupitia mitandao
yao.
6. Kwa mujibu wa Kifungu cha 17 cha
Jedwali la Pili katika Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta,
Sura ya 306 ya Sheria za Nchi, kinachoipa Mamlaka uwezo wa kutoa adhabu
kwa Wenye Leseni dhidi ya uvunjifu wa Sheria, Kanuni na Masharti ya
Leseni, Mamlaka ya Mawasiliano imetoa:
A. Onyo kali kwa Kampuni za:
(i) Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart),
(ii) MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo),
(iii) Airtel Tanzania Limited,
(iv) Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel), na
(v) Zanzibar Telecom Limited (inayojulikana kama Zantel).
kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Kanuni
ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Postal ya mwaka
2011 [the Electronic and Postal Communications (Computer Emergency
Response Team) Regulations, 2011] kwa kushindwa kuweza mazingira salama
kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.
B. Imeamuru Kila Kampuni husika:
(i) Kuhakikisha kuwa, kuanzia siku ya
kutolewa kwa amri hii, inaweka mazingira salama katika mtandao wake
yatakayozuia utumaji wa jumbe za kilaghai (yaani ‘spoofed messages’) na
matishio mengine ya kiusalama;
(ii) Kulipa faini ya Shilingi za
Kitanzania Milioni Ishirini na Tano (Shs 25,000,000.00) kwa Mamlaka ya
Mawasiliano kabla ya tarehe 29 Januari, 2016; na
(iii) Endapo Makamuni haya yatashindwa
kutimiza amri Na.2 hapo juu, Mamlaka itachukua hatua zaidi za kisheria
na kiudhibiti dhidi ya Kampuni ya Simu husika.
7. Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania inapeda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi kuwa
makini na jumbe za kuwataka kutuma fedha bila ya kuwa na uhakika.
Inashauriwa kuhakiki ujumbe husika kwa kupiga simu na kuongea na mhusika
kabla ya kufanya maamuzi ya kutuma fedha hata kama namba inayotumika
unaijua. Vilevile wawe makini wanapopokea jumbe zinazoonesha zinatoka
kwa mtu fulani wanayemjua kumbe ni matapeli wanaotumia ulaghai kwa njia
hii ya “spoofing”.
IMETOLEWA NA
Dkt. Ally Y. Simba
Dkt. Ally Y. Simba
MKURUGENZI MKUU
30 Disemba, 2015
No comments:
Post a Comment