Mmiliki wa Kliniki ya Tiba Asilia ya Fore Plan iliyopo Ilala Bungoni, Dar, Dk. Juma Mwaka ‘JJ Mwaka’.
SIRI nje! Sakata la mmiliki wa Kliniki ya Tiba Asilia ya Fore Plan
iliyopo Ilala Bungoni, Dar, Dk. Juma Mwaka ‘JJ Mwaka’ kufanyiwa ziara ya
kushtukiza na baadaye kudaiwa kumkimbia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla limechukua sura
mpya huku mambo mengi yaliyomponza yakifichuka.
SOO LILIVYOKUWA
Siku chache baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri, Dk. Kigwangalla
alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho kinachosifika kwa kutoa
tiba ya asili badala ya hospitali (tiba mbadala), hasa kwa wanawake
wanaosumbuliwa na matatizo ya uzazi.
Katika hali ya kushangaza, matatibu na manesi waliokuwa kazini
walitokomea kusikojulikana na kuwatelekeza wagonjwa, wakikwepa kuonana
na waziri huyo ambaye akiwa na msafara wake, walifanya ukaguzi wa kina
kwenye kituo hicho.
Kufuatia kitendo cha Dk. Mwaka na wenzake kuingia mitini, Waziri
Kigwangalla alitoa amri ya kufungwa kwa muda kwa kituo hicho mpaka
uchunguzi wa kina utakapokamilika ili kuona kama huduma zinazotolewa
zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.
MITANDAO YAMCHOMA
Simulizi ya jinsi tabibu huyo alivyosimamishwa kutoa huduma ili
kupisha uchunguzi na ukaguzi wa kina, inaanzia mbali ambapo kwa mujibu
wa vyanzo vyetu vya kuaminika, chokochoko kuhusu huduma zake zilianzia
kwenye mitandao ya kijamii.
“Kwa kipindi kirefu kulikuwa na makundi mawili yanayoshindana kwenye
mitandao ya kijamii. Kundi la kwanza ni wale waliowahi kutibiwa katika
kliniki hiyo na kufanikiwa kupona matatizo yao.
“Hawa
walikuwa wakimtetea kwamba anatoa huduma sahihi lakini kundi jingine ni
wale waliotibiwa na kupoteza fedha nyingi bila kupona matatizo
yaliyokuwa yakiwasumbua.
“Hawa ndiyo waliochangia kwa kiasi kikubwa kuifumbua macho Serikali
ya Rais John Pombe Magufuli kwani walitaka dawa na huduma za Dk. Mwaka
zichunguzwe kwa vile walishapoteza imani naye,” kilisema chanzo chetu
makini kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Gari la Dk. Mwaka, aina ya Range Rover - Sport SE
KUANIKA MAISHA YAKE MTANDAONI
Kwa mujibu wa chanzo kingine, tabia ya Dk. Mwaka kupenda kuanika
maisha yake kwenye mitandao ya kijamii ni suala jingine lililomponza na
kufanya watu waanze kutilia shaka utajiri wake.
“Unajua Dk. Mwaka na mkewe wamekuwa wakiposti kwenye mitandao ya
kijamii, hasa Instagram picha za magari yao ya kifahari anayomiliki
likiwemo Range Rover-Sport SE na hekalu (jumba kubwa la ghorofa)
analoishi, lipo Mbezi (Dar).
“Pia walikuwa na kawaida ya kujisifia wanaposafiri kwenda nje ya nchi
kufanya shopping, hasa Dubai. Hicho pia kimemponza sana maana watu
walianza kufuatilia utajiri wao na pengine ndiyo waliomchongea
serikalini,” kilisema chanzo hicho kilicho karibu na familia hiyo.
VIPINDI RUNINGANI
Sababu nyingine inayotajwa na vyanzo vyetu kwamba imemponza tabibu
huyo, ni ile kawaida yake ya kuendesha vipindi kwenye runinga, akieleza
huduma anazozitoa kwa lengo la kupata wateja wengi.
“Unajua Dokta Mwaka ndiye anayeongoza kwa kuwa na vipindi vingi vya
runinga kwenye televisheni mbalimbali nchini. Kama unavyojua kipindi
kimoja cha runinga kulipia kinagharimu fedha nyingi sana. Sasa watu
wakawa wanajiuliza anapata wapi fedha za kulipia gharama hizo? Ni kutoka
kwa wateja wake kweli?” kilisema chanzo chetu.
KUPUUZA AGIZO LA WIZARA
Pia, habari za ndani zinadai kuwa, mwaka jana wizara husika iliwaita wataalam wote wanaotoa tiba mbadala na kuwapa masharti.
Masharti hayo ni kutovaa koti jeupe, kutoning’iniza shingoni chombo
cha kusikilizia mapafu/mapigo ya moyo (stethoscope) na kutojiita
madaktari wakitakiwa kutumia utambulisho wa tabibu masharti ambayo
karibu wote wameyapuuza.
KUNA KOSA KUJITANGAZA?
Katika utafiti uliofanywa na gazeti hili na kutiliwa nguvu na Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
imebainika kwamba, kwa mujibu wa viapo wanavyokula madaktari na matabibu
ni makosa kujitangaza kwenye redio, runinga au mitandao kwa lengo la
kuwavuta wagonjwa.
“Changamoto iliyopo kwetu ni kwamba matangazo wanayoyatoa ni kinyume
na kanuni lakini tumebaini kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
ambayo inasimamia sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini ndiyo
inayoruhusu. Tumejipanga kukutana nao ili kujadili jambo hili,” alisema
Mwalimu.
SIYO MARA YA KWANZA KUFUNGIWA
Tukio hili la kusimamishwa kutoa huduma, si la kwanza kumtokea Dk.
Mwaka ambapo mwaka jana, maafisa kutoka wizara ya afya walifika kwenye
kliniki hiyo kwa kushtukiza, wakiwa wameongozana na waandishi wa habari
na kufanya ukaguzi ambapo kutokana na kutoridhishwa na mazingira
waliyoyakuta, walilazimika kuifunga kliniki hiyo kwa muda usiojulikana.
Hata hivyo, wiki kadhaa baadaye, Dk. Mwaka alifungua kesi mahakamani kupinga kufungiwa huko na kushinda kesi.
No comments:
Post a Comment