BILA shaka mpenzi msomaji wa safu hii uko vizuri. Ni wiki nyingine tunakutana katika uwanja wetu maridhawa kuweza kujinasibu na kupeana mawilimatatu yahusuyo maisha ya mahusiano.Kama mada inavyojieleza hapo juu, nimepokea kesi nyingi sana za watu tofauti wakiomba ushauri kwamba wanashindwa kudumu katika mapenzi kutokana na mwenzake kujifanya anajua kila kitu.
Anataka kusikilizwa kwa kila kitu, anajua kuhusu maisha, mapenzi, tabia za watu na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.
Msomaji mmoja aliniambia kwamba, mpenzi wake ni mtu wa kujishaua. Anajifanya anajua kila kitu hivyo wamekuwa wakishindwa kusikilizana maana na yeye anapojaribu kumwelewesha, mpenzi wake naye anamuona yeye anajifana anajua kuliko yeye.
“Ubishi kwenye maisha yetu ndiyo umetawala. Anakwambia kitu ambacho yeye anaamini yupo sahihi. Ukimwambia kwamba haupo sahihi anapinga, anaamini yeye ndiyo yupo sahihi. Mtabishana wee mwisho wa siku hakuna muafaka.
“Na mimi huwa namkatalia maana naamini nipo sahihi katika jambo ambalo nalisimamia. Tena mbaya zaidi nampa mifano hai yenye ukweli juu ya kile ambacho nakiamini lakini bado mwenzangu anakuwa hanielewi. Najisikia vibaya maana imefika wakati hata marafiki zake wanamsema juu ya hilo lakini wapi, habadiliki. Ni king’ang’anizi hatari ananifanya nishindwe kufurahia kabisa mapenzi,” alilalamika mmoja wa msomaji.
Kwenye mfano huo wa msomaji tunapata kuona ni jinsi gani watu wapendanao wanahitaji kusikilizana ili waweze kudumu penzini.Athari za kujifanya kila mmoja anajua ni ugomvi wa kila siku. Kama ni wanandoa, kila mmoja atakuwa haitamani nyumba.
Hapo ndipo unapokuta wanaume wanachelewa kurudi nyumbani. Wanaamua kuchelewa makusudi ili kuepuka kelele za nyumbani.Mwanamke naye hataki kushindwa, ishu ya jana ataikumbushia na mabishano kuchukua nafasi tena, mume naye hakubali kushindwa, mjadala unaendelea.
Matokeo chanya ya kila mmoja kujifanya anajua hususan kwa wanandoa huwa ni mchepuko.
Ni rahisi mwanandoa kuchepuka nje ambako atapata tulizo la moyo. Kama ndani ya ndoa anapakosa amani, unafikiri nini kitatokea pale atakapokutana na wasiojifanya wanajua.
Huko nje wapo ambao wao kujifanya wanajua ni mwiko. Utakachomwambia yeye anasema hewala baba au mama. Hana kiburi, mcheshi na mpole, si mtu wa kunyanyua kinywa chake na kutamka maneno machafu au kujifanya anajua kwa ampendaye.
Jibu ni rahisi tu hapo. Mhusika atashawishika kuanguka penzini tena mbaya zaidi ataanza kujiongeza kwa kukulinganisha wewe na huyo mchepuko mwenye sifa lukuki zenye kumpendeza. Kwa kipimo cha akili zake akigundua amekuzidi, imekula kwako, anaweka kijiwe.
Ataamini kijiwe hicho kitamsaidia kuvusha ule muda wa kurudi mapema nyumbani. Atahakikisha anarudi muda ambao ni wa kujibwaga, alale. Hataki kusikia kelele, akizidi kukolea na mambo ya nje upo uwezekano kabisa ashindwe kurudi nyumbani na ndoa ndiyo itakuwa inapumilia mashine.
Kumbe basi, ni vyema wapendanao ambao wameingia katika tatizo hili kubadilika. Kama wanataka kuishi pamoja, kila mmoja anapaswa kujishusha kwa mwenzake. Kila mmoja ajifanye mjinga kwa mwenzake, msikikilizane, mtadumu.
Hakuna haja ya kutafuta mbadala, ng’ang’ania ulipo kwa kujisahihisha tabia ya ujuaji huku pia ukimuomba mwenzako kwa lugha ya upolea naye abadilike.
No comments:
Post a Comment