Mathayo George (61) anayeugua ugonjwa wa kuota magamba.
MKE na mume wa familia moja, Mathayo George (61) na Beatus Mathayo (49) wakazi wa Nachingwea mkoani Lindi wamejikuta kwa nyakati tofauti wakikumbwa na magonjwa ya ajabu ambapo mume ameota magamba huku mke akipata upofu.
MUME ALIANZA KUPATA VIPELE
Akizungumza na waandishi wetu jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mathayo alisema kuwa alianza kuugua ugonjwa huo mwaka 2010 kwa kuanza vipele vidogovidogo vyenye muwasho.Alifafanua kuwa vipele hivyo baadaye vilibadilika na kuwa magamba magumu yanaoambatana na maumivu makali ambayo yalimfanya akose usingizi.
“Nilijaribu kwenda hospitali na zahanati mbalimbali za Mkoa wa Lindi kutibiwa, ikashindikana na sasa nimeshauriwa niende Hospitali ya KCMC, Moshi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi lakini kutokana na hali yangu kuwa duni nimeshindwa kabisa kwenda huko kwa kuwa sina fedha ya nauli na matibabu,” alisema Mathayo.
Magamba yakiwa mikononi mwa Bw. Mathayo George.
MKE NAYE AKAPOFUKA
Kama hiyo haitoshi Mathayo aliyekuwa mkulima mashuhuri wa korosho amejikuta akikosa msaada kwa kuwa kabla ya kupata matatizo hayo yeye ndiye alikuwa msaada kwa mkewe Beatus.
Alisema sasa mambo yamebadilika kwa kuwa mke wake alipata upofu ghafla tangu mwaka 1998 ambapo sasa hawezi kufanya shughuli yoyote ya kumuingizia kipato na amebaki kuwa mtu wa kusaidiwa kwa kila kitu.
Bw. Mathayo George akiwa na mkewe Beatus Mathayo (katikati).
YEYE NA MKEWE WANA MAISHA MAGUMU
Aliongeza kuwa yeye na mkewe sasa wamejikuta wakiishi katika maisha magumu bila kujua hatima yao na anaona giza nene ambalo hajui mwanga atapataje.
“Kutokana na hali hivyo, nawaomba Watanzania wenye huruma watusaidie ili niweze kwenda huko KCMC kupata matibabu, bila msaada wenu naamini tutapoteza maisha,” alisema.
Kwa yeyote aliyeguswa na Mathayo anaweza kuwasiliana naye kwa mawasiliano ya simu, anapatikana kwa namba:
+255 652 006 910 au +255 752 264 127 au +255 688 354 444.
No comments:
Post a Comment