TTCL

EQUITY

Sunday, November 30, 2014

Kijiji cha Litembo na utajiri wa utalii wa kiutamaduni


SEKTA ya utalii inachangia pato kubwa la taifa kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya utali vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini kama vile mbuga za wanyamapori, maziwa ,fukwe mbalimbali , maeneo ya kihistoria, mapango ya kale, maporomoko ya mito pamoja na vivutio vingine vingi.

Utalii katika Tanzania hauonekani katika wanyamapori pekee kama inavyodhaniwa na wengi,kwa kuwa yapo mambo  mengi ya kustaajabisha yakiwemo makumbusho ya maisha ya watu wa kale,fukwe,mawe ya kale,mapango na sura mbalimbali ya dunia kama vile milima na mabonde yenye kuvutia.


Mapato yanayotokana na utalii hapa nchini yanaweza kuongezeka zaidi endapo vivutio vilivyopo vitaibuliwa kuboreshwa na kutangazwa kwa nguvu zote ndani na nje ya nchi ili kuwavutia watalii wengi.

Uchunguzi umebaini kuwa wananchi wa mikoa ya kusini bado hawajanufaika katika sekta ya utalii, moja ya sababu kubwa ni kwamba wananchi wa mikoa ya kusini hawajapata elimu sahihi kuhusu utalii,aina za utalii pamoja na faida zake kiuchumi na kijamii.


Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa ya kusini mwa Tanzania ambao umebahatika kuwa na vivutio lukuki vya utalii vikiwemo mbuga za wanyamapori,milima,ziwa Nyasa,mawe ya ajabu,fukwe,majengo ya kihistoria ,ngoma za asili pamoja na samaki wa mapambo.


Moja ya vivutio ambavyo hivi sasa vinawavutia watalii wengi ni makumbusho ya taifa ya Majimaji yaliopo mjini Songea ambayo karibu kila siku yamekuwa yakitembelewa na watalii wa ndani na nje ya nchi ili kujifunza historia ya mashujaa wa vita vya majimaji.

Hata hivyo katika hali ya kuchochea utalii wa kishujaa na kihistoria katika mkoa wa Ruvuma imebainika kuwa katika kijiji cha Litembo kilichopo kilometa 40 kutoka wilayani Mbinga kimebeba utalii wa kishujaa na kihistoria katika vita  dhidi ya wakoloni wa kijerumani ambavyo vilipiganwa na wananchi wa kabila la wamatengo mwaka 1902.

Katibu wa Baraza la mila kata ya Litembo Remigius Hyera anabainisha kuwa kiongozi wa wajerumani aliyeitwa Korongo kutokana na ukatili wake alimtumia ujumbe kiongozi wa kabila la wamatengo mwaka 1902 kuwa anataka kuingia katika eneo hilo na kuwataka viongozi hao wa jadi kumuunga mkono ili kuwa chini yake.

Hyera anabainisha kuwa kiongozi wa wamatengo baada ya kupata ujumbe huo alipiga ngoma kubwa kwa ajili ya kuwakusanya wananchi ambao aliwaeleza kuhusu ujumbe huo wa Korongo ambapo kwa pamoja wananchi hao walikataa kuwa chini ya wakoloni wa kijerumani hivyo Korongo aliamua kuwapeleka wapiganaji wakiwa na bunduki 19 ili kupigana na mashujaa wa kabila la wamatengo.

Mababu zetu hawakuogopa walijipanga wakiwa wamejitokeza kwa mamia kwa kutumia silaha za jadi walijipanga nyuma ya jiwe linaloitwa Litembo na kuanza kupambana na wakoloni wa kijerumani,hata hivyo wajerumani walitumia risasi za moto kuwauwa mashujaa hao wa kimatengo inakadiriwa watu 800 waliuwawa kikatili’’,anasema Hyera.

Kwa mujibu wa katibu huyo wa Baraza la mila,mashujaa wa kabila la wamatengo walionusurika walikimbilia kwenye pango la jiwe la Litembo ambalo limepewa jina hilo kutokana na kufanana na mnyama tembo na kwamba hata jina la kijiji hicho limetokana na jiwe hilo.

Hyera anasema damu za mashujaa wa kabila la wamatengo waliouwawa na wajerumani zilichuruzika kwenye mto ambao unaanzia kwenye milima ya Umatengo na iliendelea hadi kwenye m ziwa Nyasa ambapo mashujaa walionusurika waliingia kwenye pango la jiwe la Litembo ambalo linachukua saa mbili na kutokea upande wa pili.

Hata hivyo anasema kiongozi wa wajerumani baada ya kuwauwa mashujaa hao akiwa na wenzake aliamua  kuchoma nyumba zote moto pamoja na vyakula vyote viliteketezwa na kufanya uharibifu mkubwa  katika eneo hilo la wamatengo.

Alois Mpengouturu ni mzee wa mila wa kabila la wamatengo aliyechaguliwa tangu mwaka 1958 anasema mara baada ya mashujaa hao kuuwawa  walizikwa katika makaburi ya kishujaa katika eneo la Litembo ambapo makaburi hayo yamehifadhiwa na yanatunzwa kimila ambapo serikali ya wilaya ya Mbinga inatarajia kuanzisha makumbusho ya mashujaa.

Anasema wazee wa mila wametenga maeneo yote ya kumbukumbu ya mashujaa katika eneo hilo kwa kujenga alama mbalimbali  na kwamba wanapata wageni wanaokwenda kutembelea makuburi ya mashujaa,kuona eneo ambalo waliuwawa mashujaa 800 na nyumba nne za kabila la wamatengo.


Kwa upande wake Fabian Ndunguru mmoja wa wazee wa mila katika kabila la wamatengo akizungumzia nyumba nne za kabila la wamatengo anasema katika historia ya kabila hilo wamatengo wameweza kuishi katika nyumba za aina nne ambazo ni nyumba ya mawe,miti,udongo na tofali za kuchoma.

“Nyumba ya kwanza ya asili ya kabila la wamatengo ni nyumba ya mawe ,nyumba ya pili ni ya miti,udongo ni nyumba ya tatu na hivi sasa wamatengo wanaishi katika nyumba bora ya tofali za kuchoma ilioezekwa kwa bati,katika mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla wamatengo ndiyo wanaoongoza kwa kuwa na nyumba bora’’,anasisitiza Ndunguru.

Mwenyekiti wa kijiji cha Litembo Paulo Mwingira anasema serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na wazee wa mila wa kabila la wamatengo wamejipanga ili kuhakikisha kuwa vivutio vyote vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo katika eneo hilo vinalindwa na kuendelezwa kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Hata hivyo anasema baadhi ya vijana wamekuwa wakifanya uharibifu katika maeneo hayo ya kihistoria ikiwemo kujisaidia haja ndogo na kubwa ovyo hali ambayo inaleta uchafuzi wa mazingira na kuwa kero kwa wageni wanaotembelea kuangalia vivutio hivyo vya utalii.

Mtendaji wa kijiji cha Litembo Falis Kapinga anasema serikali ya kijiji imeomba fedha kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya kufanya uboreshaji wa maeneo yote ya utalii katika kijiji hicho yakiwemo maeneo yenye makaburi ya mashujaa,eneo lenye unyayo wa kale wa binadamu,nyumba nne za asili  za kabila la wamatengo pamoja na kuboresha nyumba nne za asili za kabila la wamatengo.


Issa Sariko ni meneja mkuu wa mradi katika pori la wanyama la Liparamba wilayani Mbinga mara baada ya kutembelea eneo hilo la mashujaa wa Litembo ameshauri vivutio vilivyopo kuibuliwa,kuendelezwa na kutangazwa ili kuwavutia watalii kutembelea eneo hilo.

“Watalii wakitoka katika hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba wanaweza pia kuja hapa katika eneo la Litembo ili kuona vivutio vya utalii wa kishujaa na kihistoria pamoja na kujionea mila za kabila la wamatengo zikiwemo ngoma za asili pamoja na vyakula’’,anasema.

Hata hivyo Sariko anasisitiza wadau wa utalii na mazingira kujikita zaidi katika kutoa elimu sahihi ya utalii  jambo ambalo anasema litawezesha watanzania kuutambua utalii .

Mbunge wa viti maalum wanawake  na mjumbe katika Bodi ya utalii katika mkoa wa Ruvuma Injinia Stella Manyanya anasema matangazo ya vivutio mbalimbali vya utalii  katika vyombo mbalimbali vikiwemo vya ndani ya nchi na vyombo vya kimataifa yatawezesha vivutio hivyo kufahamika kitaifa na kimataifa hivyo idadi ya watalii kuendelea kuongezeka mwaka  hadi mwaka na kuliingizia taifa mapato makubwa.

Injinia Manyanya anasema tafiti zinaonesha kuwa ni watanzania wachache  ambao wanaonekana kuwa na tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini,mbali ya wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo bado watu wengi hawajaonesha kipaumbele katika sekta ya utalii.

No comments:

Post a Comment