
RAIS
Jakaya Kikwete, amesema kuanzia Juni mwakani kila kinachofanyika katika
jiji la Dar es Salaam kinaonekana katika mitambo itakayokuwapo kila
mahali.
Alisema kutokana na kufungwa kwa mitambo hiyo waharibifu wa miundombinu, vibaka na wahalifu hawatoweza kufisha matendo yao.
Rais
Kikwete alitoa kauli hiyo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya
kufungua barabara ya Tegeta – Mwenge iliyojengwa kwa kiwango cha lami
huku ikiwa na urefu wa kilometa 12.9.
Alisema
inasikitisha kuona serikali ikiingia gharama kubwa katika kutengeneza
barabara halafu watu wasiokuwa na uchungu na fedha hizo za walipa kodi
wakiharibu miundombinu hiyo kwa maslahi ya matumbo yao.
“Tumeshaongea
vya kutosha jamani katika hili sasa dawa ya watu wa aina hii ipo jikoni
na Juni mwakani watu wote hawa tutawakamata kirahisi tu hawatakuwa na
pa kukimbilia,”alisema.
Hata
hivyo Rais Kikwete, hakuwa tayari kueleza ni mitambo ya aina gani
itakayofungwa lakini katika nchi mbalimbali kumekuwa na kamera katika
mitaa ambazo zinarekodi kila kinachofanyika.
Aliongeza
kuwa ujenzi wa barabara ya Tegeta-Mwenge, itasaidia kupunguza
msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na hii ni baada ya
kukaribia kumalizika kwa barabara ya Msata Bagamoyo.
Alisema
kutokana na tatizo la foleni lililopo katika Jiji hilo, ambapo hata
mihadi ya watu kukutana siku hizi imekuwa ni taabu, Serikali imekuwa
ikijitahidi kutafuta njia mbalimbali za kutatua kero hiyo ikiwemo
kuboresha vyombo vya usafiri wa umma na utengenezaji wa barabara za
mchepuko.
Hata
hivyo aliwataka wananchi kujua kuwa tatizo la foleni halipo tu Dar es
Salaam bali hata kwanye nchi zilizoendelea ikiwemo Newyork Marekani na
China.
Rais
Kikwete, alisema hii inachangiwa na kukua kwa maendeleo ambapo kwa
Tanzania mwaka 1980 magari yaliyokuwa yakipita barabarani ni yale ya
Serikali na kwa watu binafsi ilikuwa lazima uombe kibali kabla ya
kununua gari.
“Lakini
hivi sasa familia nyingi zinamiliki magari na nyingine zimeenda mbali
zaidi ambapo baba ana gari lake, mama na watoto na bado watu wataendelea
kumiliki magari siku za baadaye yote hii imechangiwa na kubadilika kwa
mfumo wa maisha na nchi kupiga hatua ya maendeleo kwa watu
wake,”alisema.
Alisema
ameziagiza Mamlaka husika kuboresha usafiri wa reli kwa kuongeza njia
za reli katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuleta
mabehewa yatakayoendana mahitaji.
Alisema
pia serikali ipo mbioni kuanzisha kivuko kitakachotoa huduma kwa wakazi
wa Bagamoyo na Tegeta na kujenga miji mingine nje ya mji ili huduma
zinazofuatwa mjini zipatikane huko huko walipo.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Alhaj Mussa Iyombe, alisema barabara
hiyo imetengenezwa kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Japan ambako
shilingi bilioni 99.6 zimetumika kukamilisha mradi huo.
Naye
Balozi wa Japan hapa nchini, Masaki Okada, alisema Serikali yake
inaamini kuwa barabara ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa uchumi na
kipaumbele chake cha kwanza ni ujenzi wa barabara.
No comments:
Post a Comment