MBUNGE wa Jimbo la Kawe jijini Dar na Mwenyekiti wa
Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha),
Halima James Mdee ambaye aliwekwa Mahabusu ya Gereza la Segerea, Dar kwa
saa kumi na mbili amesimulia mambo matano mazito aliyokumbana nayo hali
iliyomfanya atokwe machozi.
Mbunge wa Jimbo la Kawe jijini Dar na
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Bawacha), Halima James Mdee.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii mwishomi mwa wiki iliyopita,
Mdee licha ya kuponda utendaji kazi mbovu wa serikali kuhusu mahabusu,
aliyataja mambo hayo kama ifuatavyo:
HAUSIGELI NA KESI NDOGONDOGO
Alisema alipofika mahabusu aliwakuta wasichana wadogo ambao baadhi yao
ni mahausigeli wakamlalamikia kwamba wamekaa ndani kwa muda mrefu bila
kesi zao kusikilizwa.
Alisema kwa uchunguzi wake alibaini kuwa wasichana hao wa kazi za
ndani, kesi zao zilifunguliwa kwa kubambikwa na mabosi wao pale
wanapodai malipo, hivyo wao husingiziwa wizi au kosa lolote.
UBOVU WA CHAKULA
Pia Mdee alisema chakula cha mahabusu hakiridhishi kutokana na kupikwa
bila kiwango na kuwa na michanga, wakati mwingine hakiivi.
MAHABUSU KUKAA MUDA MREFU BILA KESI KUSIKILIZWA
Jambo jingine alilodai kukumbana nalo Segerea ni mahabusu kukaa kwa muda
mrefu kati ya miaka 4 hadi 7 bila kesi zao kusikilizwa kwa kisingizio
cha upelelezi kutokamilika.
MACHANGUDOA KUWASHAWISHI MABINTI
Katika sakata lingine, Mdee alisema wanawake wengi waliokamatwa kwa
makosa ya kujiuza usiku (machangu) wanaopelekwa mahabusu wamekuwa
wakiwashawishi wasichana wadogo, hasa mahausigeli wanaofikishwa humo.
“Wasichana hao huwashawishi mahausigeli kiasi kwamba wanapotoka mle
mahabusu na wao wanakwenda kujihusisha na ukahaba na biashara ya madawa
ya kulevya kwa vile baada ya kutoka hawapewi nafasi na mabosi wao
kuendelea na kazi,” alisema Mdee.
MAHABUSU WA KIKE KUADHIBIWA NA ASKARI WA KIUME
Jambo lingine aliloligundua Mheshimiwa Mdee ni kitendo cha askari wa
kiume kutoa adhabu kwa maabusu wa kike badala ya kuadhibiwa na wanawake
wenzao kitendo ambacho alisema kimekuwa kikiwadhalilisha mahabusu hao.
Hata hinyo, Mdee alimuomba Waziri wa Sheria na Katiba, Asharose
Migiro kuanzisha utaratibu wa safari za kushtukiza magerezani na
kuzungumza na mahabusu ili kusikiliza kero zao na kuzitatua.
Jumanne iliyopita, Mdee alifikishwa katika gereza hilo saa 11 jioni
ambako alilala hadi kesho yake saa 1 asubuhi kwa madai ya kufanya
maandamano haramu kwenda Ikulu ya Dar.
No comments:
Post a Comment