Katika dunia ya leo, ili kila mtu aweze kuboresha maisha yake ni lazima
awe na elimu. Elimu ndiyo inayomwezesha mtu kujitambua na kujimiliki
yeye mwenyewe kwanza, pia kuzikabili changamoto zinazomsonga, kuyatawala
na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake.
Ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika Kusini, amewahi kusisitiza
umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii, kwa kusema kuwa: “elimu ni
injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa
mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa
mgodini anakuwa mkuu wa mgodi, na mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa
rais wa taifa kubwa.”
Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo, ni lazima iwe
elimu bora ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri,
kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo
mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii.
Elimu ni ukombozi iwapo italenga kumpatia mtu uwezo wa kupambana na
changamoto zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla. Elimu inamjenga mtu
kuwa raia makini na mzalishaji ndani ya nchi yake.
Historia ya elimu nchini inatukumbusha malengo ya msingi ya elimu
Tanzania. Ukiacha elimu ya kibaguzi iliyokuwa inatolewa kabla ya uhuru,
elimu ya Tanzania baada ya uhuru ililenga kumjenga mtu katika nyanja
zote ili awe mzalishaji mzuri katika nchi yake.
Ndiyo maana elimu na kazi vilisisitizwa, na vyuo vya ufundi pamoja na
kazi za mikono vilipewa msisitizo mkubwa, huku suala la usawa, haki na
misingi ya umoja wa kitaifa vikichanua na kushamiri kwenye nyaraka za
serikali na kwenye vichwa vya watu.
Dhamira hii ikaleta maboresho makubwa yakiwamo ongezeko kubwa la
uandikishaji, kutaifishwa kwa shule za binafsi na kufanywa za umma na
kuzaliwa kwa Azimio la Arusha lililokuja kuwa dira ya kusimamia misingi
ya haki, usawa, udugu na utu.
Solomon Eliufoo ndiye aliyeongoza michakato hii kama Waziri wa Elimu kutoka mwaka 1962 hadi 1965.
Katika kipindi chake, Eliufoo alipiga marufuku ada kwa wanafunzi wa
sekondari, kuendeleza ujenzi wa shule za msingi na sekondari na upanuzi
wa mafunzo kwa walimu wa daraja A na C na elimu ya watu wazima.
Pia ndani ya miaka hii mabadiliko mengine tuliyoshuhudia ni kuruhusiwa
kwa Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi
na Kiingereza kwas sekondari, kupinga ubaguzi wa rangi katika elimu na
elimu ya msingi kutangazwa kutolewa kwa miaka minane.
Kipindi cha 1965 hadi 1970 chini ya Waziri Chediel Mgonja, kilishuhudia
uamuzi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Kambarage Nyerere, akitangaza
rasmi falsafa mpya ya elimu iliyojulikana kwa jina la Elimu ya
Kujitegemea, kuanzishwa kwa Taasisi ya Elimu na uundwaji wa Baraza la
Mitihani la Afrika Mashariki.
Mabadiliko mengine katika kipindi hiki yalihusu kutungwa kwa Sheria ya
Elimu ya mwaka 1969, shule za msingi kufundishwa na Watanzania pekee na
kuimarishwa kwa kisomo cha watu wazima na chenye manufaa.
Elimu ya watu wazima ndiyo iliyojenga nchi na kuiweka kwenye hadhi ya
juu katika medani za kimataifa, hasa kwenye suala la upunguzaji wa
ujinga.
Hadi kufikia mwaka 1986 kiwango cha Watanzania kujua kusoma na kuandika
kilikuwa ni asilimia 91, tofauti na sasa ambapo kimeshuka hadi asilimia
69 kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya HakiEilmu mwaka 2001
na 2010. Miaka ya 1975 hadi 1980 ilishuhudia mabadiliko mengi tu kwenye
mfumo wa elimu yetu.
Ni kati ya miaka hiyo, ujenzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi
ulifanyika, kutolewa kwa Tamko la Elimu ya Msingi kwa wote, ujenzi wa
vituo vya ufundi kwa wahitimu wa elimu ya msingi na kuzuiwa kwa mtihani
wa darasa la nne.
Pia Taasisi ya Ukuzaji Mitaala na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima
vilianzishwa. Na mwaka 1978 ndiyo kipindi ilipotungwa Sheria ya Elimu
namba 25 chini ya Waziri Nicholas Kuhanga.
Kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, mengi yamefanyika ikiwamo kuanza kwa
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP), kuanza kwa Mpango wa
Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya
Sekondari (MMES).
Mipango hii ndiyo inayoshika hatamu za kuiendesha elimu yetu kuelekea
kwenye ubora na fursa sawa kwa wote. Je, tija ya mabadiliko haya tangu
uhuru ina mwelekeo gani kwa Taifa? Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025,
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA), Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), Mpango wa Maendeleo.
Taarifa ya idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika aliyoitoa Naibu
Waziri wa Elimu, Philip Mulugo bungeni Februari 15, 2011 ya Elimu ya
Sekondari (MMMES) na Sera ya Elimu na Mafunzo vyote vinabainisha ukweli
huu kuwa ili Tanzania ipige hatua kali za kimaendeleo ni lazima wananchi
wake wapate elimu bora iliyokamilika.
Lakini je, elimu inayotolewa hapa Tanzania inakidhi haya yote? Ama ni
kwa kiasi gani inawawezesha watoto na vijana kufikia malengo hayo? Hili
ndilo swali la msingi linalopaswa kutuongoza kuelekea kwenye mipango na
vitendo vinavyoipeleka mbele elimu yetu na siyo kuirudisha nyuma.
Hivi karibuni tumesikia mengi kutoka kwa viongozi wetu kuhusu elimu
hapa nchini akiwamo Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli,
akisemea kutoa elimu bure kwa watoto kuanzia awali hadi kidato cha nne.
Watanzania wanapenda elimu yenye ubora na siyo tu kwa kuwa itatolewa
bure iwe chini ya kiwango, tunaamini kuwa “vya bure havina thamani”
lakini hatutarajii kuona upuuzi huu ukiendelea.
Imekuwa kawaida kuwaona wanafunzi waliohitimu darasa la saba wakiwa
hawajui kusoma na kuandika. Masikio ya Watanzania na macho wanatamani
kuiona kauli ya “elimu bure” ikifanyiwa utekelezaji mapema Januari mwaka
ujao.
Hadi mwaka 2010 zaidi ya watoto milioni 8 (ambao ni zaidi ya asilimia
90 ya uandikishaji halisi) wameandikishwa shule za msingi na zaidi ya
wanafunzi 1,638,699 wako sekondari.
No comments:
Post a Comment