Watu wengi hususani katika jamii za Kiafrika
wamekuwa na mtazamo kuwa mtu mwenye ulemavu hawezi kufanya kitu
chochote, ambacho kinaweza kuwa na manufaa katika jamii.
Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa walemavu
wengi kuishi katika umaskini, huku hata baadhi yao wakiamini kuwa hakuna
mchango wowote wanaoweza kuutoa katika jamii, matokeo yake ni kuishia
kuombaomba barabarani.
Hata hivyo kwa wenzetu wa mataifa yaliyoendelea
ulemavu siyo sababu ya kumfanya mtu ashindwe kufanya shughuli za kijamii
au kutoa huduma pale inapohitajika, tena kwa usahihi zaidi wakati
mwingine kuliko hata mtu asiyekuwa na ulemavu.
Hilo limedhihirishwa na Ted Rummel raia wa
Uingereza ambaye licha ya kupooza mwili wake mpaka kufikia hatua ya
kutembelea baiskeli ya wagonjwa, lakini bado ni daktari tegemezi kwenye
idara ya upasuaji katika hospitali za Progress West na Barnes Jewish
St Peters nchini humo.
Daktari huyo ambaye amepooza kuanzia kiunoni mpaka
miguuni, ameonyesha kuwa taaluma yake haiwezi kupotea kwa sababu ya
ulemavu, alioupata ukubwani hivyo kuamua kuendelea na kazi hiyo katika
mazingira magumu.
Licha ya kuishi katika hali ya kupooza kwa muda wa
miaka mitatu sasa, Rummel anamudu kuhudumia wagonjwa na kuwafanyia
upasuaji ilhali akiwa kwenye kigari maalumu.
Hali ya kupooza mwili haijapunguza ufanisi wa kazi
ya Rummel, kwani licha ya kukumbana na changamoto ya kushindwa kusogeza
miguu bado ana uwezo mkubwa katika kufanya upasuaji.
Hali hiyo ilivyoanza
Tofauti na watu wengi Rummel alizaliwa mzima
kabisa lakini mwaka 2009 akaanza kupatwa na maumivu katika nyonga zake,
ingawa hakufikiria kuwa hali hiyo ingeendelea kumsumbua kwa muda mrefu.
Katika mahojiano yake na gazeti la Daily Mail la
Uingereza, Rummel anaeleza kuwa aliendelea kuishi na maumivu hayo mpaka
Septemba 2010, ambapo ndipo hali ya kupooza ilipoanza rasmi na kujikuta
mwili wake ukikosa mawasiliano. Ikamlazimu kuachana na kazi hiyo kwa
muda ili apate matibabu na mapumziko ambayo yalichukua kipindi cha miaka
miwili, licha ya kutibiwa viungo.
Muda wote aliokuwa katika matibabu Rummel alikuwa
karibu sana na familia yake, pamoja na wafanyakazi wengine hali iliyompa
faraja na kujikuta akitamani apone haraka ili aweze kurejea kwenye kazi
yake.
“Wakati matatizo haya yananikuta nilikuwa tayari
nina taaluma na elimu ya kutosha lakini najua wapo wengine ambao
yanawakuta wakiwa katika hali mbaya zaidi, ndiyo maana nataka kutumia
nguvu na taaluma yangu kuwasaidia,” anasema Rummel na kuongeza;
“Nashukuru familia yangu hata wafanyakazi wenzangu walikuwa
karibu na mimi na muda wote walinionyesha upendo, hapo ndipo nikafikiria
na kujiapiza kuwa lazima nipone ili niweze kuwasaidia wengine.”
Maisha mapya ya Dk Rummel
Anasema hata baada ya kubaini kuwa viungo vyake
vimepooza akaona hakuna haja ya kuachana na taaluma yake ambayo
ameifanya kwa muda mrefu na inasaidia kuokoa maisha ya watu wengi,
hivyo mchango wake bado unaendelea kuhitajika.
“Kitu cha kwanza kukifikiria ilikuwa ni taaluma
yangu na namna ambavyo watu wengi wangekosa huduma yangu, hivyo nikaamua
nitajitahidi kwa namna yoyote ile nirudi kwa mara nyingine katika
chumba cha upasuaji,” anasema Rummel.
Hatimaye dhamira yake ilitimia akarudi hospitali
na upasuaji wake wa kwanza aliufanya chini ya uangalizi wa daktari
mwingine, ambaye alikuwepo katika chumba cha upasuaji kumsaidia endapo
angehitaji msaada lakini alifanikiwa kufanya upasuaji huo bila kuhitaji
msaada.
Kabla ya kupata maradhi hayo Dk Rummel alikuwa na
uwezo wa kuhudumia wagonjwa 60 kwa siku na kufanikiwa kuwashughulikia
wagonjwa wasiopungua 1,000 kwa mwaka, hali iliyosababisha pengo lake
kuonekana kipindi chote alichokuwa katika mapumziko ya matibabu.
Anakiri kuwa anakumbana na changamoto mbalimbali
wakati wa kufanya upasuaji akiwa katika hali hiyo, kutokana na kushindwa
kusimama na kumudu kumzunguka mgonjwa wakati wa upasuaji kama
ilivyokuwa awali.
Sasa hivi analazimika kufanya upasuaji akiwa
amekaa kwenye kiti cha umeme, ambacho humsaidia kunyanyuka na kumzunguka
katika eneo analolifanyia upasuaji.
Kwa upande mwingine Rummel anasema kuwa hali hiyo
imemfanya kuwa karibu sana na wagonjwa na kujua hali zao na namna
ambavyo wanajisikia wakiwa katika maumivu.
“Sasa hivi namwelewa sana mgonjwa najiweka katika
nafasi yake na kuhisi ambavyo anajisikia, hivyo inakuwa rahisi kumpatia
matibabu sahihi,” anasema.
No comments:
Post a Comment