Chande Abdallah na Denis Mtima, Mwanza
KATIKA
hali ya kushangaza, mwanaume mmoja, Maige Masyome (29) amechomwa kisu
na mwenzake, Amosi Anthony kwa kosa la kukataa kumnunulia pombe ya
kienyeji, tukio lililotokea Novemba 10, mwaka huu, Kigonga, Nyamunge
mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wetu akiwa hoi katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Maige alisema siku ya tukio alikutana na Amosi kwenye kilabu
cha pombe ya kienyeji maarufu kama Kwa Mama Mung’ori ambapo mwenzake
huyo alimtaka amnunulie pombe lakini akakataa.
Alidai Amosi
alibadilika na kuanza kumlazimisha na alipozidi kukataa alinyamaza
lakini wakati akiinuka kuondoka zake eneo hilo, Amosi alimchoma kisu
shingoni.
“Nilishangaa baada ya kuona anazidi kunizonga
nimnunulie pombe, nilipokataa akakaa kimya. Sasa wakati nainuka
nilishangaa jamaa anasimama na kunichoma kisu shingoni,” alisema Maige
kwa taabu.
Kwa upande wake, kaka wa mgonjwa huyo aitwaye Wambura,
alisema walifungua kesi katika Kituo cha Polisi cha Nyamango kwa jalada
NYM/RB/3291/2013 na kuongeza kuwa wamepata taarifa kuwa mtuhumiwa bado
yupo uraiani akitembea bila wasiwasi wakati ndugu yao anateseka
hospitali.
“Nimepata taarifa kuwa mtuhumiwa anatembea bila
wasiwasi mtaani wakati mdogo wangu anateseka hapa ndani. Ninaomba
mtuhumiwa akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Wambura.
Hadi
sasa Maige amelazwa katika Hospitali ya Bugando akiendelea na matibabu
huku akiwa amepooza sehemu ya mwili wake kuanzia kifuani hadi miguuni.
No comments:
Post a Comment