UNAMKUMBUKA Salma Moshi? Yule mwanamama aliyevuma DDC Kibisa akiwa na
kikundi chake cha maonyesho ya sanaa cha Ujamaa Theatre Troupe? Ni
kweli amepotea nchini lakini anafanya mengi Marekani sasa akiwa kada wa
CCM na Mtanzania. Raia Tanzania ilimtafuta na kufanya mahojiano naye kwa
njia ya simu akiwa huko na yafuatayo ndiyo yaliyojiri:
Paparazi: Uliondoka nchini lini na kwa madhumuni gani?
Salma: Niliondoka nchini mwaka 2003 kwa mwaliko wa
kushiriki kwenye tamasha. Wakati huo nilipata mialiko miwili. Wa
Ufaransa na Marekani.
Paparazi: Ehee, baada ya tamasha nini kiliendelea?
Salma: Baada ya tamasha ambalo lilifanyika Miami
Florida hapo tukaweza connection (kuunganisha) nyingine mbazo ziko
Washington DC, kwa hivyo tukaja Washington DC.
Paparazi: Safi, sasa unaishije huko?
Salma: Naishi kama kawaida sasa. Mwanzoni inakupa shida hasa kuhusu
kwenda nyumbani na kurudi na kuhusu kazi lakini ukishakamilisha inakuwa
vizuri zaidi duniani kote ndiyo maana nataraji kuja nyumbani hivi
karibuni.
Paparazi: Hivi sasa unajishughulisha na nini? Ni sanaa au…..?
Salma: Naipenda sana siasa. Napenda kuwa mwanasiasa
kuwatumikia watu, kazi ya utumishi. Nipo katika Chama cha Mapinduzi ni
katibu mwenezi na pia huwa nafanya sanaa ingawa mara nyingine inakuwa
taabu. Wengi huku wanakwambia wanaona haya kucheza sanaa, nawashawishi
nawapata lakini inakuwa sio mara zote, ni tofauti na nyumbani. Pia
nafanya kazi za kawaida kujikimu katika maisha ya kila siku.
Raia Tanzania: Sanaa za maoyesho Tanzania ni kama zinakufa.
Hakuna tena vikundi kama vya DDC Kibisa ulichowaji kukiongoza wala
Ujamaa Theatre Troup ulichowahi kukimiliki. Muda si mrefu tumefiwa na
Mzee Small Said Ngamba na Salum Tambalizeni. Ukiombwa leo kufufua sanaa
za maonyesho kwa kuanzisha kikundi cha taifa na ukahakikishiwa kuungwa mkono na Serikali utakubali kurudi?
Salma: Mimi sanaa iko kwenye damu. Ninapatwa na
uchungu kuona sanaa za maonyesho zinapotea wakati wasanii ndio
tumetumika tokea enzi za uhuru. Nikimbukumba Mzee Mwinamila, Mzee
Mayagilo, Mzee Morris na wengi wazee wetu. Nikikumbuka wakati
tunashindana na John Komba akipiga DDC Kondoa napiga DDC Kariakoo na
kumbi zinajaa. Si kweli kwamba watu hawapendi sanaa hata kidogo naamini
sanaa ikifanyika kikamilifu watu watakuja tu. Mashirika mengi yameacha
kudhamini kama Bima na majeshi. Vikundi havina msisimko. Napenda vizuri
kumzungumzia Tambalizeni. Nilichangia kwa kiasi kikubwa kukuza kipaji
chake. Nilimuona Manzese, nikasikiliza ngonjera yake nikamchukua mwaka
1983.
Nikamfanyia mpango RTD alikuwa anatoka kila siku watu wakampenda ,
akaenda kusoma Kivukoni. Alizunguka na Rais Mkapa Tanzania nzima wakati
wa kampeni. Niko tayari kuja kuanzisha kikundi cha taifa. Ninapinga
vikali sherehe zote zinazofanyika bila kuashirikisha wasanii wa sanaa
za maonyesho. Mashirika na serikali kila mara wamekuwa wanaalika Bongo
Fleva au taarab. Hata siku moja hawajawahi kuchukua vikundi vya ngoma
ambavyo ndivyo vinaonyesha utamaduni wetu. Matamasha yapo lakini kwetu
sisi hawapelekwi walengwa, unaona vikundi kutoka Zimbabwe, Afrika
Kusini, Burundi wanazitumia nafasi hizo. Wasanii wetu wamekuwa masikini
wanatumwa tu uwanja wa ndege na sehemu ambazo hazina kipato.
Raia Tanzania: Nini maoni yako kuhusu utaratibu wa
Serikali kama tulivyoona hivi karibuni kwa Waziri wa maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu kumpeleka mwigizaji wa filamu Aunty Ezekiel
kwenda kutangaza Utalii Marekani badala ya wasanii wa sanaa za
maonyesho?
Salma: Kusema kweli katika suala la utalii au sherehe za uhuru, watu wa
nje watapenda kuja kuona utamaduni wetu halisi na kuutangaza na siyo
kuona watu kama Naomi Campbell ambao wako wengi kwao. Nilitarajia
vikundi vya sanaa kutumika kwa lengo la kuutangaza utalii na vivutio vya
utalii ni ngoma za asili siyo kuja kumuona mtu kama Naomi Campbell
ambaye kwa utalii wa kwetu hana nafasi.
Raia Tanzania: Bado unaonyesha sanaa ya kucheza na nyoka huko Marekani?
Salma: Huku si sana. Nyoka waliopo huku si wakubwa, ni
wadogo. Mazingira ya kuwaweka na masharti kuhusu wanyama ni mambo
yanayonifanya nifanye sanaa hiyo mara chache sana. Sanaa zingine kama
maigizo na ngoma nazipenda sana. Nilicheza siku moja wazungu
wakaniambia mimi ni msanii halisi, walifurahi sana.
Raia Tanzania: Hivi ukikaa na kuwaza, huoni
kwamba ulipata bahati ya mtende kwenda huko Marekani? Sanaa za
maonyesho zilivyodorora sasa maisha yako yangekuwaje?
Salma: Nashukuru sana kupata bahati ya kuja huku.
Kutoka nje kumenisaidia sana kujua tamaduni za wenzetu na kujifunza
mengi kuhusu sanaa. Najua sasa ni kwanini wasanii wa nje wanakuwa
matajiri. Ukweli ni kwamba wanajituma na kuwapo kwa hakimiliki
kunawasaidia. Wanakuwa makini mno na shughuli zao kwa kuwa na mameneja
wa uhakika na wanasheria. Naamini ningekuwa Tanzania ningekuwa mbali
zaidi katika sanaa kwa sababu ningejituma kupambana na hali iliyoko.
Raia Tanzania: Unawashauri nini vijana wenye
damu ya kisanii katika sanaa za maonyesho hapa nchini. Je, watafute
shughuli nyingine za kufanya au kuna matumaini ya sanaa za maonyesho
kufufuka na kuwa kama zamani?
Salma: matumaini yapo, tena kwa sanaa kama ngoma ni
rahisi sana. Matamasha mengi yapo. Wapewe wakashiriki wakajifunze na
kuongeza kipato. Serikali kupitia BASATA (Baraza la Sanaa la Taifa)
lisaidie kuhamasisha mashirika na watu binafsi kuinua sanaa. Kuna
kipindi Tanzania Breweries ilidhamini wasanii kutangaza kampuni.
Raia Tanzania: Unajisikiaje unapowaona wasanii kama wa Botswana
wanapocheza makhirikhiri na kutamba kimataifa na huku nyumbani Tanzania
hakuna kikundi au ngoma yoyote kati ya makabila zaidi ya 120 inayofua
dafu wakati zipo nyingi zinazovutia kama Sindimba na Lizombe?
Salma: Ngoma za Botswana zimepata Promotion (kutangazwa). Haziwezi
kuchuana na ngoma za kwetu kama Sindimba, Lizombe, Mkwaju ngoma na
nyingi ngingine nzuri. Nikiwa huku nilipata kanda ya dvd ya ngoma
kutoka Botswana. Nikaangalia nikaona tunaweza ni kusaidia tu katika
kurekodi.
Raia Tanzania: Wewe kwa maoni yako, wa kulaumiwa hasa ni nani? Wasanii wenyewe au Serikali?
Salma: Sehemu ambazo zinazostahili kubeba lawama ni
Serikali kupitia wizara yake ya utamaduni na BASATA. Wasanii wengi
tunao tena wenye vipaji. Wanabanwa na utaratibu na kujikuta
wanakatishwa tamaa kwamba si kazi yenye tija. Vibali vinatolewa kwa
mapromota lakini mapromota waliopo wengi si mapromota bali ni
wafanyabiashara wanaua sanaa. Anamtumia msanii na kumkuacha. Hawapeleki
wataalam ambao wako ofisini kuwasaidia wasanii na wakati mwingine
waliopo kwenye nafasi nyeti za kuwasaidia wasanii wakati mwingine
hukalia mialiko inayokuja. Hawaipeleki kwa wasanii au kuitangaza. Wageni
wengi wanaokuja hawawekewi programu wapi watakwenda kuona utamaduni
wetu. Mimi nakumbuka kwa macho yangu kuna msanii alipewa mwaliko tarehe
ya tamasha imepita. Tatizo jingine ni kwamba wasomi wa sanaa hawajikiti
kusimamia sanaa za maonyesho. Hata wakiwa kwenye makundi wanajichagua
wenyewe. Niliona wakati ule walianzisha mzee Godwin Kaduma (marehemu)
na Mgunga Mnywenyela kama taasisi ya utamaduni ilikuwa pale Kariakoo na
haikushirikisha wasanii wa kawaida. Wasanii wa kawaida hawapaswi
kulaumiwa, mtiririko wa sanaa unawaumiza.
Kama kuna mradi wa fedha kama ule uliokuwapo wa kutafsiri kwa Kiswahili
filamu ya Neria utakuta wanachaguana wenyewe wasomi, hawashirikishi
wasanii wa kawaida.
Nakumbuka kuna wakati unatakiwa kwenda airport au kwenye sherehe bure
na usipokwenda kikundi chako kunafungiwa, inaumiza sana.
Raia Tanzania: Ni juhudi za mwanasiasa gani ambazo unazikumbuka ziliendeleza sanaa nchini?
Salma: Juhudi kubwa za mwanasiasa ambazo nazikumbuka
kwa kujituma ye binafsi katika sanaa ni za Mzee Moses Nnauye (marehemu).
Mwansiasa huyu alikwenda kwenye majeshi na kuwahamasisha wasanii. Ndiye
aliyemvumbua kapteni John Komba (marehemu). Akamwingiza jeshini
akaanza kufanya vitu vyake kwa kutunga nyimbo nzuri.
Mzee Nnauye alikuwa anatunga nyimbo anagawa kwa wasanii, anaingia
jukwaani, anashiriki na anakwenda vijijini kusaka vipaji. Mimi binafsi
nimefanya naye kazi. Alikuwa akija DDC Kariakoo na kwenye kumbi
mbalimbali. Mpaka leo huwa najiuliza kwanini hakupewa Wizara ya
Utamaduni. Angekuwapo hadi leo asingekubali kuona sanaa za maonyesho
zinapotea hivi hivi.
Raia Tanzania: Ni msanii gani mkongwe ambaye unadhani alikuwa kama ni alama ya taifa?
Salma: Msanii mkongwe ambaye nadhani alikuwa alama ya
taifa ni mzee Morris Nyanyusa. Ngoma zake zimetumika sana kwenye
taarifa ya habari. Ilikuwa ukisikia tu unajua sasa ni taarifa ya habari,
sijui kama alilipwa inavyostahili au ilikuwa sifa tu anazopewa.
Alisafiri nchi tofauti duniani na alikuwa kivutio kikubwa Japan. Licha
ya kuwa alikuwa mlemavu wa macho, aliweza kupiga ngoma kumi. Watu
wakija kutoka nje walikuwa wanataka kuchukua notii (wasome alama za
mipigo ya ngoma zake) wakapige kwao kama yeye. Hapa (Marekani) kuna
msanii Steve Wonder amekuwa kivutio kikubwa kama mzee Morris.
Paparazi: Ungepata nafasi ya kuwa Waziri wa Utamaduni, ni vitu gani ambavyo ungerekebisha au kuvianzisha?
Salma: Ningekuwa waziri wa utamaduni ningebadilisha
sera. Tunataka sanaa itambuliwe kama kazi na pia kama biashara. Wasanii
wanufaike na mtindo wa mameneja au mapromota kuwa ndio wasemaji wa
wasanii, hapana. Tunataka wasanii wenyewe waseme. Nakumbuka Bagamoyo
marehemu Muhidin Mwalimu aliwahi kumkalisha mtu chini. Tulikuwa kwenye
semina ya wasanii marehemu akamwuliza huyo mtu uko kwenye kikundi gani
unapiga chombo gani, akababaika kujibu akamwambia kaa chini, tunataka
wasanii. Nitahakikisha BASATA, COSOTA (chama kinachohusika na
hatimiliki za wasanii) vinafanya kazi kwa kushirikiana na wasanii na
kuwasikiliza.
Paparazi: Ukipata nafasi ya kukifufua kikundi chako cha
Ujamaa Ngoma Theatre ungekiendesha vile vile au au ungefanya mabadiliko?
Salma: Nitafanya mabadiliko. Nitaongeza vyombo vya kisasa, mavazi
mazuri, kuwa na ukumbi wetu wenyewe. Tunakutana na kujiwekea mafao kama
bima za ugonjwa, vifo, kuwa na hisa, kutafuta mikataba nje na kuwasaidia
kwenye mikataba yao binafsi. Pia kuboresha maisha yao ili jina la
kikundi liwe sawa na jinsi tunavyosaidiana.
Paparazi: Unajuta kujikita kwenye sanaa kwamba ulipotea njia?
Salma: Swali kama hilo niliulizwa pia na mwandishi
mmoja kutoka Uingereza. Alipotambulishwa alitaka aandike Mama Salma
anasema sanaa imekufa na anajuta. Nikamweleza sanaa haijafa Tanzania,
bado ipo. Ingawa tunaona hivyo wasanii wenye moyo wapo. Mimi sijuti
kabisa kujiingiza kwenye sanaa. Nashukuru nimeweza kuiwakilisha nchi
yangu, India, Zambia na Marekani. Pia sanaa imenipa umaarufu mkubwa.
Naamini hili suala la kunyonywa wasanii litaondoka, wasanii watafurahia
jasho lao.
Paparazi: Una ndoto za kuingia kwenye siasa kuwa mbunge au Rais?
Salma: Napenda siasa. Napenda sana kazi za uongozi.
Katika maisha yangu yote nimekuwa kiongozi. Hata nilipotoka nyumbani
nilikuwa kiongozi wa Mtaa na huku ni Katibu wa Uenezi. Nina ndoto ya
kuwa mbunge na hata kuwa Waziri wa Utamaduni. Kuwa Rais siwezi kukataa
nikiombwa na wananchi.
Paparazi: Wewe ni miongoni mwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Nini maoni yako kuhusu uraia pacha?
Salma: Suala la uraia pacha ni muhimu kote kote.
Kwanza ieleweke kwamba hakuna mtu anayetaka kuikana nchi yake. Watu
wengi wanachukua uraia wa kigeni kwa kutaka kupata unafuu wa maisha na
hasa kazi katika nchi walizohamia. Kuna kazi ukiwa raia ni rahisi
kuipata na hata kusomeshwa na ndiyo utakuta zenye maslahi mazuri
zaidi. Unapata unafuu wa maisha, unapunguziwa gharama. Ukiwa raia
unafuu ule ndiyo unaoutumia kupeleka chochote nyumbani. Watu wengi
wanataka kuwekeza nyumbani lakini tatizo wanajua kwamba watachukuliwa
kama wageni. Watoto waliozaliwa huku wakitaka kuja nyumbani itawapa
shida. Kuna Mtanzania mmoja alisimama kumwuliza kiongozi mmoja kwenye
mkutano, tutaongozwaje na Mmarekani na sisi ni Watanzania. Yule mhusika
akahamaki, utanambiaje Mmarekani na mimi kitovu changu kimezikwa
Barabara ya 18 Tanga? Kusema kweli, watu wengi wanataka waje wawekeze
nyumbani. Ningependa kuwa raia wa Marekani na Tanzania kwa pamoja iwapo
itapitishwa sasa. lakini kwa vile haijapitishwa nitabaki kuwa raia wa
Tanzania na kuwezesha kushawishi wawekezaji.
Paparazi: Kama katibu wa uenezi nini shughuli zako?
Salma: Kama katibu wa uenezi na pia Mtanzania,
shughuli zangu ni nyingi hapa Marekani. Kwanza mimi ni kiunganishi
muhimu cha Watanzania waliopo hapa. Tunaishi kama ndugu. Kila siku
tunajadili mambo muhimu yanayofanyika nyumbani au hata hapa Marekani na
duniani kwa ujumla. Tunasaidiana kwa hali na mali na kupashana habari
sana sana za nyumbani. Nimeanzisha kundi kwenye mtando wa simu wa
whatsapp ambalo ni maalum kwa ajili ya Watanznaia waishio ughaibuni na
tumewashirikisha pia hata walioko nyumbani wakiwemo viongozi wa ngazi
mbalimbali na wasanii. Kwa kweli tunakwenda vizuri sana na nafurahi
kwamba mijadala yetu inakuwa mizuri kwani kila mmoja huchangia kwa lengo
la kujenga kama Mtanzania. Analaumu panapostahili na kusifia pia
panapostahili na hata kutoa mawazo yake mambo gani yanafaa
kurekebishwa.
Mengi tumefanya. Kwa mfano majuzi yaliyopotokea maafa ya kisiwani
Pemba hivi majuzi tulichakarika kuchangisha fedha na kampeni yetu
ilikuwa na mafanikio ya kuridhisha.
Kaika misiba na sherehe zote za kitaifa huko nyumbani huwa atunakuwa na
wawkilishi wetu ambao hutujuza kila kinachojiri. Kwakweli inapendeza.PapaWanapokuja viongozi wa kitaifa na wa vyama mbali mbali hapa huwa
tunafanya juhudi za kukutana nao. Tunafanya mkutano na kuwauliza maswali
ambayo tunadhani yanahitaji ufafanuzi wao kuhusiana na misimamo yao
binafsi na vyama vyao juu ya mustakabali wa nchi yetu.
No comments:
Post a Comment