TTCL

EQUITY

Saturday, August 17, 2013

SAKATA LA PICHA ZA UFUSKA KANISANI LAZIDI KUZUA MAPYA

WAKATI viongozi wa Kanisa la Orthodox jijini Dar es Salaam wakidai kuwa hawataki Klabu ya British Legion of Tanganyika kuendesha shughuli zao katika eneo wanalodai ni lao kwa madai ya kuwepo kwa picha chafu na ulevi, sakata hilo limeibua mapya baada ya maaskofu kudai kuwa wamekashifiwa.

Baadhi ya picha za ufuska zilizopo katika klabu iliyopo ndani ya eneo la kanisa.

Maaskofu wa kanisa hilo, wamedai kukashifiwa na kudhalilishwa na Mwenyekiti wa Klabu, Abdul Mtiro Sisco kutokana na kiongozi huyo kuwaambia waandishi wa habari kuwa eneo la klabu yao linataka kuuzwa na kanisa kutokana na dhiki waliyonayo Wagiriki.

Mtiro alidai kwa waandishi wa habari kuwa kutokana na matatizo ya kiuchumi nchini kwao, Wagiriki hao wanataka kuliuza eneo hilo ili wapeleke fedha kwao.

Mwenyekiti wa Klabu, Abdul Mtiro Sisco.

“Wanadai kuwa hapa sisi tunafanya uhuni wakati watu wanaokuja hapa si wahuni…Hawa Wagiriki kwa sababu ya matatizo ya uchumi nchini kwao, wanataka kuuza eneo hili ili wawapelekee fedha ndugu zao…” alidai Mtiro.

Mtiro alidai klabu yao ipo hapo tangu mwaka 1970 kama British Legion of Tanganyika ambapo awali ilikuwa ni ya wanajeshi wa Uingereza lakini baadaye Waafrika wakaingia lakini ugomvi wao ulianza mwaka 1990 walipoambiwa watoke eneo hilo.

Kuhusu madai ya kuwepo picha za utupu ndani ya klabu hiyo, Mtiro alisema si kweli, hata hivyo, akasema kwamba hiyo ni klabu binafsi.

Habari zinasema kauli hiyo imewaudhi maaskofu wa kanisa hilo na kuwafanya kuwasiliana na wanasheria wao ili kuona jinsi ya kushughulikia hicho wanachodai kuwa ni kashfa kwao.


Baadhi ya viongozi wa kanisa.

Askofu mmoja wa kanisa hilo amesema hawakubaliani na madai ya Mtiro kwa sababu ndani ya klabu hiyo kulikuwa na picha za utupu na wanafanya biashara ya pombe eneo la kanisa.“Lengo letu sisi ni kuwafundisha watu wamfuate Mungu waende Mbinguni na tunaomba maeneo yote ya kanisa yaheshimiwe,” alisema askofu mmoja.

Wakati hayo yakiendelea, sakata la kugombea eneo hilo tayari limefikishwa Mahakama Kuu chini ya Jaji John Mgetta ambapo upande wa kanisa, Wakili Edward Chuwa amedai kuwa wamezuia kuingia wanachama wa klabu hiyo kwa sababu hawawajui na hakuna mahali panapoonesha wanachama ni akina nani.

Upande wa klabu ukiongozwa na Wakili Evod Mmanda katika kesi hiyo namba 178/2013, wamedai mbele ya jaji huyo kuwa kanisa lisiwepo katika eneo hilo na wanachama waruhusiwe kuingia katika klabu yao wakati shauri likiendelea kusikilizwa mpaka hapo mahakama itakapotoa uamuzi.

Jaji Mgetta alitembelea eneo hilo Jumanne iliyopita na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Agosti 21, mwaka huu ambapo mahakama itasikiliza pingamizi lililowekwa na kanisa

Soma zaidi: http://mwanahabariuswazi.blogspot.com/2013/08/mapya-yaibuka-kuhusu-sakata-la-picha-za.html#ixzz2cDUAHrMt

No comments:

Post a Comment