Nderemo na furaha zatawala
Dar es Salaam. Shangwe, vifijo, vigelegele na
ngoma jana vilitawala Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na
mitaa kadhaa ya Jiji la Dare s Salaam, wakati maelfu ya Watanzania
walipojumuika na Rais Jakaya Kikwete kumpokea Rais wa Marekani, Barack
Obama.
Ndege iliyombeba Rais Obama, ijulikanayo kama Air
Force One, iligusa ardhi ya Tanzania saa 4:40 asubuhi na Rais Obama
alitokea katika mlango wa ndege hiyo mnamo saa 8.43 na kuamsha shangwe
na hoihoi kutoka kwa watu waliofika uwanjani hapo.
Alipokanyaga ardhi ya Tanzania, Obama alimkuta
mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, akiwa tayari kumpokea akiwa
ameambatana na mkewe, Mama Salma Kikwete.
Tofauti na ilivyo kwa misafara ya viongozi wengine
kutoka nje ya nchi, jana kulikuwa na viongozi wachache sana wa Serikali
waliofika uwanjani hapo kumpokea Obama. Walioambatana na Rais Kikwete
ni viongozi tisa tu ambao ndiy o walishikana mikono na Rais Obama na
mkewe.
Hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed
Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.
Wengine ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu
Ameir Kificho, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick na Meya
wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi, Mkuu wa Majeshi, Jenerali
Davis Mwamunyange na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema.
Kama ilivyotarajiwa, ulinzi wa uwanjani hapo
ulisimamiwa na makachero kutoka Marekani ambao walikagua watu, vifaa na
magari yote yaliyowasili uwanjani hapo kwa ajili ya mapokezi hayo.
Hata magari maalumu mawili ambayo Rais Obama
aliyatumia pamoja na familia yake walipoondoka uwanjani hapo,
yalikaguliwa vikali na askari hao wa Marekani wakiwa na mbwa na vifaa
vingine vya kielektroniki kabla hayajaruhusiwa kupaki nje ya uwanja huo
na kisha baadaye kuruhusiwa kuingia ndani ya uwanja.
Makachero hao walikagua pia njia ya kurukia ndege
kwa kutumia gari lao maalumu walilokuja nalo kutoka Marekani. Mara ya
pili walikagua njia hiyo ya kurukia ndege kwa kutumia gari aina ya Noah
lililokuwa limewabeba makachero wa Marekani.
Gari hili lilitembea kwenye njia ya kurukia ndege
kutoka upande mmoja wa uwanja hadi upande wa pili na kurudi lilikotokea.
Wakati fulani, makachero hao waliizuia Land Rover la Polisi ambayo
ilionekana kuelekea katika sehemu ya ndege ikielekea au kutoka kwenye
njia ya kurukia.
Baada ya kupokewa na mwenyeji wake, Rais Obama na
mkewe walikabidhiwa mashada ya maua na watoto kisha Rais Kikwete
alimwelekeza mgeni wake kwenye jukwaa maalumu ambako walipigiwa nyimbo
za taifa zilizoambatana na mizinga 21.
Baada ya hapo Rais Obama alikagua gwaride
lililoandaliwa uwanjani hapo kwa ajili yake kabla gwaride hilo
halijapita kwa heshima kwa mwendo wa haraka mbele yake. Kisha Kikwete
alimwelekeza Obama vilipokuwa vikundi vya ngoma ambavyo vilitumbuiza.
Rais Obama na mkewe walionekana kuvutiwa sana na ngoma hizo, hasa ngoma
ya mganda na kuwafanya waanze kutikisa vichwa vyao kulingana na midundo
ya ngoma. Rais Obama alishindwa kujizuia na kujikuta akicheza sambamba na wachezaji wengine.
No comments:
Post a Comment