Mkurugenzi Mtendaji TGNP Afungua Mafunzo ya Ukatili wa Jinsia
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya (mbele) akifungua semina hiyo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya
amefungua mafunzo ya Ukatili wa Kijinsia na Haki za Binadamu kwa kundi
la washiriki kutoka mikoa na taasisi anuai za umma na binafsi ili
kuwajengea uwezo juu ya mapambano ya masuala upiganiaji haki kwa jamii.
Akizungumza na washiriki wa semina hiyo, Bi. Mallya aliwataka washiriki
kutumia nafasi waliopata ipasavyo kwa kuhakikisha wanafuatilia mafunzo
vizuri ili kila mmoja atoke kama malozi wa chachu ya mapambano juu ya
vitendo vyote vya kikatili kwa jamii na masuala ya haki za binadamu.
Aliwaeleza washiriki kila mmoja kwa nafasi aliyonayo sasa anaweza kuwa
chachu ya mabadiliko endapo atatimiza wajibu wake kwenye eneo alipo.
Alisema suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka nchini kwani
limeenea karibuni kila eneo la nchi, hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha
mapambano dhidi yake.
"...Kwa kweli suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka kwenye
maeneo yote ya nchi yetu, twakwimu za kitaifa zinatuambia takribani
asilimia 40 ya wanawake wote wamekwisha fanyiwa ukatili wa namna moja
ama nyingine, kwa kila wanawake wawili mmoja ameshafanyiwa ukatili wa
kijinsia...wengine tumepigwa, wengine tumefanyiwa ukatili wa kiuchumi,
kisaikolojia...," alisema Mallya.
Aidha Mallya aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia kwa sasa katika mfumo wa
utandawazi lipo kila upande bila kujali ni kwa wanawake au wanaume,
kwani kila mmoja anaathirika na suala hilo. Alisema lengo la mafunzo
kama hayo ni kuona mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu
haki za makundi yote, yaani haki za watoto, haki za kijamii, haki za
watu wenye ulemavu, haki za wanawake haki za vijana n.k.
Alisema kuwa nchi nyingi za Bara la Afrika zinapambana na mifumo miwili
mikubwa, ambayo ni mfumo wa kitabaka unaoongeza nafasi kati ya matajiri
na masikini (walio nacho na wasionacho) na mfumo dume ambao nao umekuwa
ukiwakandamiza wanawake katika jamii.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) ambacho
kilianzishwa na TGNP ili kuratibu mafunzo anuai ya jinsia chini ya
mwamvuli wa TGNP. Miongoni mwa washiriki katika semina hiyo ni
wawakilishi kutoka madawati ya jinsia ya Jeshi la Polisi, mahakama,
idara ya ustawi wa jamii, washiriki kutoka asasi za watu wenye ulemavu
na wasio na ulemavu na baadhi ya wajumbe kutoka mikoa kadhaa ya
Tanzania.
No comments:
Post a Comment