TTCL

EQUITY

Sunday, April 24, 2016

Mafanikio ya ziara ya wafanyabiashara wa Oman nchini


  MAFANIKIO YA ZIARA YA WAFANYABIASHARA WA OMAN NCHINI



Tanzania na Oman zimesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce  na Oman Chambers of Commerce ili  kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment (OTIC) kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji zilizoko Tanzania na Oman.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bibi. Mindi Kasiga  amesema kuwa mkataba huo ni matokeo ya ziara ya siku tatu ya Waziri Viwanda na biashara wa  Oman , Dkt. Ally Mohamed Al Sunaidy, pamoja na ujumbe wa wafanyabiashara 108 na maafisa wa Serikali ya Oman iliyofanyika nchini mwezi Aprili mwaka huu.

Amesema lengo la ziara hiyo lilikua kuwawezesha wafanyabishara wa Oman na Tanzania  kushiriki kongamamo la biashara la uwekezaji lililowawezesha wafanya bishara hao kubaini fursa za uwekezaji zilizoko nchini Tanzania na Oman.

Amesema tayari  Serikali ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera kilichopo mjini Morogoro ambacho  kitazalisha tani laki nne za sukari  itakayouzwa hapa nchini huku Tanzania ikitarajia kuzalisha  spiriti na hamira itakayouzwa nchini Oman pamoja na nchi za Mashariki ya kati.
‘’ Wafanyabishara wetu na wale wa Oman kupitia makubaliano haya watanufaika na fursa za uwekezaji kwa kupata mikopo mbalimbali na tayari mtaji wa Dola za Marekani milioni 25 zitatumika kwa wawekezaji hao’’ Amesema Bibi. Kasiga.

Aidha,amesema Wafanyabiashara  kutoka Oman tayari wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, viwanda na biashara, kilimo, utalii  pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Ameongeza kuwa uwekezaji  utaongeza  ajira akitoa mfano wa  kiwanda cha Sukari cha Kagera kitakachozalisha ajira 500 pamoja na kuongeza wigo wa soko.

Katika hatua  amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa itawapeleka watumishi 105 wa ngazi mbalimbali katika Balozi 35 zilizo katika nchi mbalimbali duniani  na kuwarudisha  nyumbani watumishi 79.

Bibi Mindi, ametaja sababu za kurudishwa kwa watumishi hao kuwa ni pamoja kuisha kwa muda wao wa kuhudumu nje ya nchi ambao ni miaka minne(tour on duty) pamoja, kustaafu na sababu mbalimbali.
Amezitaja Kada za watumishi wanaorudishwa nchini kuwa ni mabalozi, wahasibu, makatibu muhktasi na maofisa wa ngazi mbalimbali.

Hata hivyo, hadi kufikia sasa tayari mabalozi watatu wamerudishwa nchini ambao ni Balozi Peter Kalaghe aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na Balozi Batilda Burian aliyekuwa Japan kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe  Magufuli alilolitoa Januari 25, 2016 kuitaka wizara hiyo kuwarudisha nchini mabalozi waliomaliza muda wao wa kuhudumu ili wapangiwe kazi nyingine.

No comments:

Post a Comment